Rafiki yangu mpendwa,
Unasoma hapa kwa sababu unataka kufika mbali zaidi ya hapo ulipo sasa. Na mara zote nimekuwa nakuambia hilo linawezekana.
Lakini huenda umekuwa na wasiwasi juu ya hilo ninalokuambia, kwa sababu umekuwa unayataka mafanikio kwa muda mrefu, lakini bado unashindwa kuyapata.
Umekuwa unapambana sana, kwa kuzingatia sheria zote za mafanikio, lakini unaishia kukutana na magumu na changamoto zinazokukwamisha.
Rafiki, unalopitia siyo jipya na wala halitokei kwako tu, limekuwa linatokea kwa watu wote, hata wale unaoona wameweza kujenga mafanikio makubwa.

Rafiki, kuna kitu huenda hujawahi kukijua kwenye kupata mafanikio makubwa, ambacho ndiyo kinakukwamisha. Kitu hicho ni ngazi za kuyataka hayo mafanikio.
Kila mtu anaweza kuyataka mafanikio, lakini wale wanaoyapata ni wanaokuwa ngazi ya juu kabisa ya kutaka, ambayo ndiyo ngazi wewe unapaswa kuwepo.
Kuna ngazi tatu za kuyataka mafanikio.
Ngazi ya kwanza ni kutaka kufanikiwa.
Hii ni ngazi ya chini na rahisi, ambayo inahusisha tu kusema na kujipa matumaini. Kila mtu anaiweza hii ngazi na wengi ndiyo huwa wapo kwenye hii ngazi. Utawaona wakisema kuhusu mafanikio, wakijifunza kuhusu mafanikio, wakifuatilia wale waliofanikiwa, lakini mambo yao yanaishia hapo. Hakuna kikubwa wanachofanya cha kuwapeleka kwenye hayo mafanikio kwa uhalisia.
Ngazi ya pili ni kuchagua kufanikiwa.
Hii ni ngazi ambayo mtu anafanya maamuzi kwamba anakwenda kufanikiwa. Kufanya maamuzi maana yake ni kuchukua hatua za makusudi ili kupata matokeo ambayo hujawahi kuyapata. Ni kuamua kuachana na baadhi ya vitu ili uweze kuchukua hatua kwenye vitu sahihi na kufanikiwa. Baadhi ya watu wamekuwa wanachagua kufanikiwa na angalau wanachukua hatua za tofauti. Japo wengi hawapati mafanikio makubwa sana, ila pia hawashindwi, wanaishia daraja la kati.
SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kupata Unachotaka…
Ngazi ya tatu ni kujitoa kufanikiwa.
Hii ni ngazi ambayo mtu amedhamiria kweli kufanikiwa, hapa mtu anakuwa hana namna nyingine zaidi ya kufanikiwa. Anakuwa amejitoa kweli kweli kufanikiwa. Anakuwa tayari kufanya kila kinachopaswa kufanyika ili aweze kufanikiwa. Mtu huyu hakubali kukwamishwa na chochote kile. Anakuwa amekula kiapo kwamba atayapata mafanikio makubwa au atakufa akiwa anayapambania. Haijalishi wameanguka mara ngapi, watainuka na kuendelea tena. Ngazi hii huwa inafikiwa na watu wachache na ambao huwa wanayapata mafanikio makubwa kadiri ya wanavyotaka.
Rafiki yangu mpendwa, je wewe upo kwenye ngazi ipi kati ya ngazi hizo tatu? Kama bado hujafika pale unapotaka kufika, usijidanganye kwamba upo ngazi ya tatu. Jiambie ukweli ngazi uliyopo, kama ni ya kwanza au ya pili, ili basi uweze kuchukua hatua sahihi za kukupa mafanikio kwa uhakika.
Wajibu niliojipa mimi ni kuhakikisha wewe rafiki yangu unayenifuatilia, kwenye maarifa na miongozo ninayoitoa, unafika ngazi ya tatu ya kujitoa kweli kufanikiwa na unayapata mafanikio makubwa kwenye maisha yako. Karibu sana tufanye kazi pamoja, kwani uhakika wa wewe kufanikiwa ninao kabisa, kama tu utakuwa tayari kufika ngazi ya tatu.
Kwenye huduma mbalimbali ninazotoa, kuna nafasi nzuri kwako wewe kujitoa hasa ili kufanikiwa. Wajibu wako ni kuwa ndani ya huduma hizo na kuchukua hatua kwenye yale tunayoshirikishana. Kuingia kwenye hizo huduma tuwasiliane kwa namba 0678 977 007.
Rafiki, kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimefafanua kwa kina ngazi hizo tatu za kupata mafanikio makubwa. Karibu ujifunze kwenye kipindi ili uweze kuelewa kwa kina na kuchukua hatua sahihi zitakazokunufaisha. Fungua kipindi hapo chini ili kujifunza.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.