3371; Inayouma zaidi.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Mara ya kwanza kufanya kitu huwa ni ngumu na inayouma kuliko mwendelezo.
Kwa walio wengi, mara ya kwanza huwa inaishia kuwa ndiyo mara ya mwisho kwa sababu ugumu na maumivu ambayo mtu anakuwa amekutana nayo.
Kukutana na ugumu na maumivu huwa ni kitu ambacho wengi wanakuwa hawajakipangilia.
Hivyo wanapokutana na ugumu na maumivu, wanafanya maamuzi ambayo siyo mazuri.
Unachopaswa kujua ni ugumu na maumivu unayopata kwa mara ya kwanza, sivyo itakavyokuwa milele.
Kadiri unavyokwenda, ugumu na maumivu vinapungua na nafasi ya wewe kupata unachotaka inakuwa kubwa zaidi.
Kuanza biashara kwa mara ya kwanza ni kugumu na kuna maumivu makubwa ambayo mtu unayapitia kadiri unavyokwenda.
Kama utaendelelea bila ya kuishia njiani, unayazoea magumu na maumivu yanapungua.
Hayo yote yanachangia kukupa wewe kile unachotaka.
Mara ya kwanza kuajiri na hata kufukuza wafanyakazi ni ngumu na yenye maumivu makali. Utadanganywa sana na watu ambao watakuwa wanakuambia yale unayotaka kusikia.
Utakuwa na matumaini makubwa juu ya watu na wataishia kukuangusha vibaya.
Mwanzo hutaelewa kwa sababu ya kukosa uzoefu, lakini kadiri unavyokwenda ndiyo utazielewa tabia za watu na hutaweza kudanganyika kirahisi.
Kukosolewa na kukataliwa kwa mara ya kwanza huwa kunaumiza sana.
Kwa sababu una kitu kizuri na chenye manufaa kwa wengine, unashindwa kuelewa kwa nini watu wakikatae.
Pia kwa kukosa uzoefu, unachukulia kukataliwa kama umekataliwa wewe na hivyo kujiona huna thamani.
Ni kadiri muda unavyokwenda ndiyo unazoea na kujua kukataliwa siyo wewe, bali kile unachofanya.
Rafiki, kitu kikubwa sana unachopaswa kukielewa mapema ni kwamba mara ya kwanza kwenye jambo lolote lile huwa ni ngumu na yenye maumivu makali.
Wajibu wako mkubwa ni kuhakikisha mara yako ya kwanza haikuzuii kuendelea na ikawa ndiyo mara ya mwisho kwako kufanya.
Unapaswa kuendelea kufanya, kwani itakuwa rahisi na maumivu kupungua kadiri unavyokwenda.
Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, hutuhusiwi kuacha kitu chochote ambacho umeanza kufanya kwa sababu ya ugumu au maumivu ya mara ya kwanza.
Kwa kila tunachopanga kufanya, tunachukua hatua, tukijua kabisa kwamba siyo rahisi na maumivu yatakuwa makubwa.
Wajibu wetu mkubwa ni kuhakikisha tunaendelea kufanya, kwa muda mrefu zaidi bila kuishia njiani.
Pamoja na magumu na maumivu tunayopitia, tumejitoa kwa kila namna ili kuhakikisha tunaendelea na safari ya kujenga mafanikio makubwa.
Hatukubali kuishia mwanzoni kwa sababu ya ugumu na maumivu.
Hayo tunayategemea na tuna maandalizi ya kuhakikisha tunabuka kila ugumu ili kupata kwa uhakika kila tunachotaka.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe