Rafiki yangu mpendwa,

Maisha ni mabadiliko, hakuna kitu kinachobaki kama kilivyokuwa. Tunazaliwa tukiwa watoto wachanga tusioweza kufanya chochote, tunakuwa watu wazima tunaoweza kufanya mengi na hatimaye kuzeeka na kufa. Katika vipindi vyote vya maisha, huwa tunapitia mabadiliko mbalimbali.

Kwa bahati mbaya sana, watu wengi wamekuwa hawanufaiki na mabadiliko wanayokuwa wanayapitia. Zaidi wanakuwa wanaachwa nyuma na mabadiliko, kwa sababu wanapenda kuendelea na mazoea waliyonayo. Na siyo kwamba wengi wamekuwa hawapendi kuendana na mabadiliko, bali wamekuwa hawajui namna sahihi ya kuyakabili mafanikio.

Aliyekuwa mtawala wa Roma na mwanafalsafa wa Ustoa, Marcus Aurelius, kwenye kitabu chake cha saba cha Meditations, aliandika kuhusu tafakari yake ya kukabiliana na mabadiliko.

Kwanza alianza kwa kuangalia upande wa maisha ambao haubadiliki, aliweza kuainisha vitu ambavyo vimekuwa jinsi vilivyo, miaka na miaka bila ya kubadilika. Na hivi ni vile vinavyotokana na kanuni za asili, hizo huwa zinafuatwa jinsi zilivyo bila ya kujaribu kuzibadili. Kanuni za asili ndizo zinayafanya maisha yaweze kwenda vile yanavyoenda na zimekuwa hazibadiliki. Wajibu wetu ni kuzijua kanuni hizo na kuweza kuziishi kwa uhakika.

Upande wa pili wa maisha ni kwenye mambo ambayo yanabadilika wakati wote. Haya ni mambo ambayo kila wakati yanabadilika na huko kubadilika kwake ndiko kunayafanya mambo hayo kuwa na manufaa. Anatoa mfano wa kuwasha moto kwa kutumia kuni, kama kuni hazitabadilika, huwezi kupata moto. Kadhalika unapokula chakula, hakiwezi kuwa na manufaa kwenye mwili kama hakitabadilika, ni lazima kibadilishwe ndiyo kitoe virutubisho kwa mwili.

Changamoto kubwa ambayo watu tunaisababisha kwenye maisha ni kutaka kubadili mambo ambayo hayabadiliki na kukataa kubadilika kwenye yale mambo ambayo yanabadilika mara zote. Watu wengi sana wameingia kwenye matatizo kwa kujaribu kubadili vitu ambavyo havibadiliki, yaani kwenda kinyume na kanuni za asili.

Tumekuwa tunaona zaidi hili kwa watu ambao wanatafuta njia za mkato za kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yao. Hawa wanajaribu kubadili vitu ambavyo haviwezi kubadilika. Kanuni za asili zipo wazi kabisa, tunaona hata kwenye viumbe hai, huwa inachukua muda tangu kuzaliwa mpaka kukua na hakuna njia ya mkato kwenye hilo. Lakini watu wamekuwa wanapuuza kanuni hizo za asili na kuishia kupata maumivu makali.

Inapokuja kwenye mambo ambayo tayari yanabadilika, watu wamekuwa wanang’ang’ana na yale ambayo tayari yanaachwa nyuma. Mfano mzuri hapa tunauona kwenye teknolojia. Kila wakati kuna teknolojia mpya zinazokuja na kurahisisha sana yale ambayo tunayafanya kwenye maisha. Lakini watu wengi kwa uvivu, huwa hawajihangaishi na teknolojia hizo mpya, badala yake wanabaki na yale ambayo wameshazoea kuyafanya, ambayo kwa wakati huo yanakuwa yanawanufaisha, ila baadaye yanakuwa hayawanufaishi tena.

SOMA; Tano Za Juma Kutoka Kitabu; How To Be A Stoic (Jinsi Ya Kuitumia Falsafa Ya Ustoa Kuwa Na Maisha Bora).

Hivyo basi rafiki yangu, kukabiliana na mabadiliko ya maisha kama Mstoa, unapaswa kufanya mambo mawili;

Moja ni kuzijua sheria za asili ambazo hazibadiliki na kuzifuata kama zilivyo. Usijaribu kwenda kinyume na sheria hizo, hata kama utashawishika kiasi gani kwamba mambo yamebadilika. Na ninaposema sheria za asili, elewa ni zile ambazo ni kweli kwenye kila eneo, kwa kila mtu na kila hali. Sheria ambazo hakuna mtu yeyote aliyezitunga, bali tulizikuta. Mfano kitu kinachorushwa kwenda juu, baadaye kitashuka chini, kwa sababu ya sheria ya mvutano ya dunia. Kwenye kila eneo, zielewe sheria za aina hiyo na usizichanganye na sheria za binadamu ambazo nyingi huwa zinabadilika.

Mbili ni badilika wewe kadiri unavyokwenda, kila siku jifunze na jaribu kitu kwenye mambo yote unayojihusisha nayo. Hata kama tayari unapata matokeo mazuri kwenye yale unayofanya, usiache kubadilika, usiache kujifunza na kujaribu vitu vipya. Siku utakayojiambia tayari unajua kila kitu au tayari umemaliza kila kitu, ndiyo siku ambayo utakuwa umeanza kuanguka. Baki na njaa ya kwenda mbali zaidi ya hapo ulipo na kuwa tayari kubadilika ili kuweza kufanya makubwa zaidi.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA tumekuwa na mjadala mzuri kuhusu falsafa ya Ustoa na mabadiliko kwenye maisha. Karibu ufungue kipindi hapo chini uweze kujifunza na kuchukua hatua ili uweze kuyatumia mabadiliko kuwa na maisha bora.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.