Rafiki yangu mpendwa,
Kama unamjua mwigizaji maarufu, Sylivester Stallone au maarufu kwa jina la Rambo, unajua jinsi ambavyo amekuwa akiigiza filamu zenye umaarufu mkubwa. Kwa kuagalia filamu zake na jinsi anavyoigiza, unaweza kuona njia yake ya mafanikio ni rahisi. Amekuwa kwenye kilele cha mafanikio kwenye uigizaji kwa zaidi ya miaka 40. Lakini je unajua amepitia nini mpaka kufika kwenye mafanikio hayo?
Rafiki, hapa tunakwenda kuangalia historia fupi ya maisha ya Rambo na jinsi ung’ang’anizi ulivyoweza kumsaidia kufikia mafanikio makubwa. Ni hadithi inayokwenda kukuonyesha jinsi hata wewe unaweza kujenga mafanikio makubwa licha ya unakoanzia au magumu unayokutana nayo.

Kuzaliwa kwa Rambo kulianza na changamoto, ambapo mama yake alishindwa kujifungua kawaida na hivyo kupelekea avutwe kwa kutumia vyuma. Kwa kuwa vyuma vinavuta kichwa, alipata majeraha kwenye kichwa ambayo yalipelekea awe mzito wa kuongea na mzito wa kujifunza darasani. Hiyo ilipelekea kuwekwa kwenye darasa la watoto wenye mahitaji maalumu, hakuweza kwenda na kasi ya kujifunza ya watoto wa kawaida.
Maisha ya familia yake hayakuwa ya utulivu, kwani wazazi wake waligombana kila mara na hatimaye kufikia kuachana. Baada ya wazazi kuachana Rambo alihangaika na maisha, ikiwa ni pamoja na kukaa kwenye vituo vya watoto wanaotoka kwenye mazingira magumu. Hakuweza kupata makuzi kwenye familia imara na yenye utulivu.
Alipomaliza shule na kujiunga na chuo, alichagua kusomea uigizaji. Baada ya kuhitimu uigizaji, kupata kazi ya kuigiza ilikuwa zoezi gumu kwake. Alihudhuria matamasha mbalimbali ya kusaka waigizaji na aliishia kupata tu nafasi ndogo ndogo za kuigiza. Hakuweza kupata nafasi ya kuwa mmoja wa waigizaji wakuu. Kipato chake kilikuwa kidogo sana kiasi kwamba kila mtu alimwambia aachane na uigizaji na atafute ‘kazi ya maana’ ya kufanya itakayomwingizia kipato. Waliona uigizaji siyo kazi ya maana na kazi za maana zipo nyingi.
Kutokana na ukata wa fedha, Rambo hakuweza kumudu kuwa na mfumo wa kupata joto kwenye nyumba aliyokuwa anakaa. Na kwa mazingira ya nchini kwake, baridi ilikuwa kali sana. Hivyo alitafuta eneo ambalo lina joto na kuwa anatumia muda wake mwingi huko. Alipata maktaba ambayo alienda kukaa kwa muda mrefu na kuanza kusoma vitabu vya uandishi wa hadithi. Kilichompeleka kwenye maktaba ilikuwa ni kupata joto, lakini akiwa pale akaona asome vitabu vya uandishi wa hadithi. Alipata msukumo wa kuanza kuandika hadithi ambazo aliweza kuziuza kwa wazalishaji na waigizaji. Hilo lilimwingizia kipato, japo hakikuwa kikubwa, lakini kulimsaidia kusogeza maisha.
Siku moja akiwa anaangalia pambano la ngumi kati ya Muhammad Ali na Chuck Whepner, alipata wazo la kuandika filamu. Kwa kipindi hicho Muhammad Ali alikuwa bondia mkubwa na maarufu, wakati Chuck Whepner alikuwa bondia mdogo na asiyejulikana (underground). Chuck aliweza kumshinda Muhammad Ali, licha ya udogo wake. tukio hilo lilimfanya Rambo apate wazo la kuandika filamu ya bondia anayeanzia chini kabisa na kupambana sana kiasi cha kuweza kumshinda bondia mkubwa.
SOMA; 2854; Ng’ang’ana mpaka ufanikiwe.
Rambo aliamua filamu hiyo ataicheza yeye kama mwigizaji mkuu na kuwa ndiye bondia anayetoka chini na kufanya makubwa. Alipeleka wazo la filamu hiyo kwa wazalishaji mbalimbali, walilipenda sana. Lakini tatizo likawa moja, hawakuwa tayari Rambo acheze kama mhusika mkuu, kwa sababu hakuwa maarufu. Hivyo walimwambia watamlipa fedha, kiasi kikubwa ambacho hakuwa nacho, ili mhusika mkuu awe mtu mwingine ambaye tayari ni mwigizaji mwenye mafanikio.
Rambo alikataa fedha hizo na kusisitiza anataka yeye ndiye acheze kama mhusika mkuu. Watu walimshangaa kwa nini akatae fedha wakati maisha yake ni magumu. Lakini kwa kusimamia hilo, walikubali kumpa nafasi ya kucheza kama mhusika mkuu. Alipitia changamoto nyingi kwenye kuzalisha filamu hiyo, lakini mwisho aliweza kukamilisha filamu ya ROCKY ambayo ilipata mafanikio makubwa na kumpelekea kuwa mwigizaji mkubwa na mwenye mafanikio makubwa.
Kuna mengi sana ya kujifunza kwa Rambo kuhusu ung’ang’anizi na uvumilivu kwenye safari ya mafanikio, hasa pale unapokuwa unaanzia chini kabisa. Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA tumekuwa na mjadala wa yale tunayoondoka nayo kwenye historia hiyo fupi ya Rambo. Karibu usikilize kipindi uweze kujifunza kutoka kwenye mifano ya watu wengine ili na wewe uweze kung’ang’ana na kupata mafanikio makubwa.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.