Rafiki yangu mpendwa,
Hebu pata picha siku uliyozaliwa ulikuja na kitabu chenye maelekezo kuhusu wewe. Na moja ya maelekezo hayo ni kwamba kwenye maisha yako unaweza kushindwa mara 10 tu. Ukishaaliza mara hizo 10, basi umemaliza nafasi zako za kujaribu kufanikiwa na utabaki bila mafanikio kwa maisha yako yote.
Rafiki, unaona ni jinsi gani utakuwa ni ukomo usio na maana, kwa sababu kwenye maisha yako umekuwa unashindwa kwenye mambo mengi. Lakini sasa, kitu kinachoshangaza ni umekuwa unayaendesha maisha yako kama vile hayo ndiyo maagizo uliyopewa.
Umekuwa na tahadhari sana, huku ukiepuka kabisa kukosea na kushindwa kama vile kuna idadi maalumu ambayo ukishaimaliza basi mchezo wako umeisha. Katika harakati zako za kuepuka kukosea na kushindwa, umekuwa pia unajizuia kupata mafanikio makubwa kwenye maisha .

Rafiki, kama kuna kitu kimoja ambacho tunapaswa kushukuru sana kwa kuwa nacho kwenye maisha ni kutokuwepo kwa ukomo kwenye kushindwa. Yaani unaweza kushindwa mara nyingi na bado ukafanikiwa. Haijalishi umeshindwa mara ngapi, kama utaendelea kujaribu kwa ubora zaidi, lazima utafanikiwa.
Kanuni moja ya mafanikio, ambayo imekuwa haijulikani wala kutumiwa na wengi ni hii; UNAHITAJI KUWA SAHIHI MARA MOJA TU. Hilo ndilo unalohitaji, kupata mafanikio makubwa, unachohitaji ni kuwa sahihi mara moja tu. Hivyo hata kama utashindwa mara elfu moja, unachotafuta ni kuwa sahihi mara moja pekee. Na ukiweza kufika kwenye hiyo mara moja ambayo unakuwa sahihi, utaweza kufanya makubwa sana kwenye maisha yako.
Swali unaloweza kuwa unajiulia ni unapaswa kujaribu mara ngapi kabla ya kuona kwamba kitu hakiwezekani? Na jibu lake ni hakuna idadi, unapaswa kuendelea kujaribu mpaka upate mafanikio. Ambacho utakuwa unafanya ni kujifunza na kuboresha zaidi, kwa sababu huwezi kurudia kufanya yale yale na kutegemea matokeo tofauti.
Mafanikio kwako ni kupata kile unachotaka na hakuna kiwango cha kujaribu ambacho ukishakimaliza basi unakubali huwezi kupata unachotaka. Ukweli ni kwamba, unaweza kupata kile unachotaka, kama utakuwa tayari kuendelea kukipambania licha ya kukosea na kushindwa ambapo utakuwa unapitia. Lakini habari njema ni hakuna ukomo kwenye kushindwa.
SOMA; Siri Kubwa Ya Kukutoa Kwenye Umaskini.
Thomas Edson mara zote amekuwa mfano mzuri kwetu inapokuja kwenye kushindwa na mafanikio. Alifanya majaribio zaidi ya elfu 10 ndiyo akafanikiwa kugundua taa ya umeme, ambapo leo tunazitumia. Waandishi wa habari walimwuliza aliwezaje kuendelea licha ya kushindwa mara nyingi. Jibu la Edson lilikuwa; “Sijashindwa mara elfu 10, bali nimejifunza njia elfu 10 ambazo hazifanyi kazi.”
Rafiki, hebu rudia tena kusoma hilo jibu kwa utulivu mkubwa, maana hapo ndipo penye somo ambalo ukiweza kulielewa na kuliishi kwenye maisha yako, ni lazima utapata mafanikio unayoyataka.
Kila unapokosea au kushindwa, jiambie hivi; SIJASHINDWA, BALI NIMEJUA NJIA NYINGINE AMBAYO HAIFANYI KAZI. Hiyo ni kauli yenye nguvu sana, kwani inakupa nafasi ya kujaribu tena, kwa ubora na utofauti ukilinganisha na awali. Hapo unakuwa unarudia kufanya, lakini kwa njia tofauti na uliyofanya awali, maana hiyo imeshakuonyesha haileti matokeo.
Hebu fikiria kama utayaendesha maisha yako hivyo, ukiendelea kujaribu bila kuchoka na tena ukijaribu kwa ubora zaidi ya awali, ni kitu gani kinachoweza kukuzuia kufanikiwa? Hakipo, labda kama utakufa kabla hujafanikiwa. Lakini kama hutakufa, kama utakuwa hai na ukaendesha mapambano yako hivyo, ni lazima utafanikiwa. Mafanikio kwako yanakuwa ni swala la muda tu, kwa sababu unachohitaji ni kuwa sahihi mara moja na kadiri unavyojaribu mara nyingi, ndivyo unavyoongeza nafasi yako ya kuwa sahihi hiyo mara moja na kupindua kabisa meza.
Karibu kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini uendelee kujifunza kwa kina jinsi ya kutumia kushindwa kujenga mafanikio makubwa unayoyataka. Kila unaposhindwa hupaswi kukata tamaa, bali unapaswa kujua umesogea karibu na mafanikio unayoyataka. Karibu ujifunze.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.