3374; Uvivu na kushindwa.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Watu wengi wamekuwa hawafanyi yale ambayo wanapaswa kufanya kwa kisingizio cha hofu ya kushindwa.
Lakini ukweli ni kwamba kinachowazuia siyo kushindwa, bali uvivu.
Ni rahisi kuwa mvivu kuliko kushindwa.
Kwa sababu kushindwa kunakutaka ufanye kitu, wakati kwa uvivu hakuna chochote unachohitajika kufanya.
Kwenye kushindwa, angalau unakuwa umejua nini hakifanyi kazi na hivyo kuweza kuboresha wakati mwingine.
Lakini kwenye uvivu, hakuna chochote unachokuwa umejifunza, kwa sababu hakuna unachokuwa umefanya.
Wengi wanasema kinachowakwamisha kwenye maisha ni kushindwa, lakini siyo kweli.
Wengi sana wanakwamishwa na uvivu kuliko kushindwa.
Una haki ya kutumia kushindwa kama kweli umefanya. Kama hujafanya kabisa, neno pekee la kutumia ni uvivu.
Uzuri ni kwamba, kama umefanya, hata kama umeshindwa kabisa, kuna mengi unakuwa umejifunza, ambapo ukifanya tena, utayaboresha.
Lakini kwenye uvivu hakuna chochote unachojifunza, zaidi ya kuendelea kujijaza hofu kwamba mambo hayawezekani.
Kwa tofauti hiyo ya uvivu na kushindwa, unaona wazi jinsi jamii ilivyojaa watu wengi ambao ni wavivu kuliko ambao wameshindwa.
Kwa wingi huo wa watu wavivu, ni fursa kubwa kwako kufanya makubwa zaidi.
Unahitaji kufanya kidogo sana kuwa mbele ya wengi ambao hakuna chochote wanachofanya kabisa.
Ukiamua tu kuachana na uvivu, njia ya mafanikio makubwa inakuwa wazi mbele yako.
Kwa sababu kuna watu wachache sana walioshindwa ukilinganisha na wengi sana ambao ni wavivu.
Uvivu unaenda hata kwenye mazoea.
Kuendelea kufanya yale uliyozoea kufanya, tena kwa namna ile ile ni aina nyingine ya uvivu.
Unaweza kuonekana unaweka juhudi kubwa sana, lakini kama hakuna mambo mapya unayoyajaribu, kwa kuhofia kushindwa, huo ni uvivu.
Pamoja na juhudi unazoweka, bado matokeo unayoyapata yanakuwa ni yale yale.
Kwa kifupi ni kwamba kama hakuna mapya unayojaribu, kama hakuna maeneo ambayo unashindwa, wewe ni mvivu na hakuna hatua kubwa utakazopiga.
Jamii ina watu wengi sana wanaofanya mambo yao kwa mazoea, wanaojichukulia ni wachapakazi.
Ukweli ni hao wote ni wavivu, wanajificha nyuma ya mazoea wakati uhalisia ni wana uvivu.
Unachohitaji kufanya ili kutoka kwenye kundi hilo la wengi ambao hawawezi kufanikiwa ni kujaribu vitu vipya kila wakati.
Hata kama utapata matokeo ambayo siyo mazuri kwa kujaribu vitu tofauti, bado unakuwa umepiga hatua zaidi.
Amua sasa kuachana na uvivu na kuwa tayari kushindwa ili uweze kupiga hatua kubwa unazotaka kupiga kwenye maisha yako.
Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga kuna dhambi kubwa mbili ambazo mtu unatakiwa kuzikwepa kama ukoma. Dhambi hizo ni UVIVU na UZEMBE.
Uvivu ni kutokufanya kabisa na Uzembe ni kutokufanya kwa usahihi.
Hizo ndiyo dhambi mbili ambazo zimewakwamisha wote ambao hawajafanikiwa.
Unapokuwa tayari kufanya na kila unapofanya ikawa ni kwa ubora zaidi, hakuna namna utabaki pale ulipo.
Ni lazima tu utapiga hatua kubwa na kutoka pale ulipo.
Unapokutana na mtu ambaye hajafanikiwa, unajua kwa uhakika kabisa kuna uvivu au uzembe ambao umehusika hapo.
Kwa kuchagua kuwa ndani ya jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, unakuwa umechagua kutubu dhambi hizo mbili kwa vitendo.
Kwa kila unachopanga, unakifanya kama ulivyopanga.
Na kila unachoanza kufanya, unaendelea kukifanya kwa ubora zaidi kila wakati.
Kwa kwenda hivyo tu, tayari unakuwa mbele ya watu wengi ambao hawafanyi kabisa na hivyo ushindi unakuwa rahisi zaidi kwako.
Je unatubu dhambi yako ya uvivu na uzembe?
Je unaukana uvivu na uzembe kwa kila hali na kuwa tayari kuchukua hatua kwa mwendelezo na ubora?
Anzia hapo na utaweza kufanya makubwa zaidi kwenye maisha yako.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe
-
Pingback: Kuwa Mtu Wa Vitendo Na Siyo Maneno Ili Uwe Muuzaji Bora Na Kufanya Mauzo Makubwa. – AMKA MTANZANIA