Rafiki yangu mpendwa,
Mshauri wa biashara kutoka nchini Marekani alienda mapumzikoni nchini Mexico. Akiwa ufukweni alimwona mvua samaki akiwa na mtumbwi wake na kumwomba ampeleke eneo jingine. Wakiwa kwenye safari, wakawa na mazungumzo kama ifuatavyo;
Mshauri; Hii kazi yako ya uvuvi huwa unaifanya kwa muda gani kwenye siku?
Mvuvi; Huwa navua samaki kwa masaa mawili tu kwenye siku.
Mshauri; Masaa mawili tu unapata samaki wa kutosha kweli?
Mvuvi; Ndiyo, napata wa kunitosha kwa matumizi ya chakula kwa familia yangu na kidogo wa kuuza.
Mshauri; Sasa unakuwa unafanya nini kwenye muda mwingine wa siku yako?
Mvuvi; Mchana napumzika na mke wangu, jioni naenda kilabuni, napiga soga na wenzangu na usiku narudi kulala.
Mshauri; Unajua kama ukiongeza muda kwenye hii kazi yako ya uvuvi, ukaajiri watu wengi zaidi, utaweza kuvua samaki wengi sana, ambao ukiwauza utapata faida kubwa.
Mvuvi; Halafu.
Mshauri; Halafu utaweza kufungua kampuni ya uvuvi na uandaaji wa samaki, utaenda kwenye mji mkubwa, utauza kwa wengi mpaka mataifa ya nje na kutengeneza faida kubwa zaidi.
Mvuvi; Aisee, halafu.
Mshauri; Utaweza kupeleka kampuni yako kwenye soko la hisa na kulipwa fedha nyingi ambazo zitakupa utajiri mkubwa na hapo kuwa huru kuweza hata kustaafu.
Mvuvi; Halafu nikishastaafu nitafanya nini?
Mshauri; Utaweza kupumzika vile unavyotaka, kupiga soga na wengine na usiku kurudi kulala.
Mvuvi; Kwani kwa sasa nafanya nini?
Rafiki, ukisoma simulizi hiyo fupi, unaweza kuona jinsi ambavyo tunahangaika na mambo makubwa na mwisho kurudi pale pale tunapokuwa tunaanzia.

Lengo langu kukushirikisha simulizi hiyo siyo uache kutafuta utajiri mkubwa, NAKUAMBIA WKA SAUTI KUBWA PAMBANA SANA KUJENGA UTAJIRI, lakini ninachotaka kukuambia ni usiache kuishi maisha yako kwa uhuru kwa sababu unajenga utajiri.
Imekuwa ni kasumba ya wengi na baadaye kuwa gereza kwao kwenye utajiri wanaojenga, kwamba wanapoteza uhuru wao wakati wa kujenga utajiri. Hivyo kadiri wanavyokuwa na utajiri mkubwa, ndivyo pia wanavyokosa uhuru.
Unakuta mtu anafanya kazi ya kuajiriwa, anaongeza juhudi zaidi ili kutoa thamani zaidi, anaongezewa kipato na majukumu ya kazi. Hivyo licha ya kipato kuwa kikibwa, anakuwa amezidi kukosa uhuru.
Kadhalika kwenye biashara, mtu anakuwa anaanzia chini kabisa, anapambana kujenga biashara yake kwa kuajiri watu na kufikia wateja wengi zaidi. Lakini biashara inakuwa inamtegemea yeye, hivyo licha ya ukubwa wa biashara, inakuwa haiwezi kabisa kwenda bila ya uwepo wake.
Hivyo ndivyo wengi wamekuwa wanakazana kujenga utajiri ambao unawanyima uhuru. Matokeo yake ni wanakuwa na utajiri, lakini hawayafurahii maisha yao, kwa sababu wanalazimika kufanya vitu ambavyo hawataki au hawapendi kuvifanya.
Kama unataka kuwa na utajiri ambao unakuweka huru kwenye maisha, unapaswa kuanza kuishi kitajiri kabla hata hujawa tajiri. Na hiyo haimaanishi kwamba uwe na matumizi makubwa, bali mambo yote unayoyafanya, hakikisha unaacha nafasi ya uhuru. Usifanye jambo lolote ambalo baadaye litakufunga zaidi.
Hii ni muhimu kuanza nayo kwa sababu baadhi ya magereza ambayo watu wamekuwa wanajijengea wao wenyewe, yanakuja kuwa magumu sana kuyavunja baadaye. Mengine yakivunjwa basi mtu anapoteza kila kitu.
Kama wanavyosema kinga ni bora kuliko tiba, ni bora ujizuie kuingia kwenye gereza kabla ya kujenga utajiri, maana ukishakuwa na utajiri na ukawa kwenye gereza, mateso yake yanakuwa ni makali sana.
Karibu kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA ambapo tumekuwa na mjadala wa jinsi ya kuanza kuishi kitajiri kabla hujawa tajiri ili uweze kuwa na uhuru kamili wa maisha yako. Fungua kipindi hapo chini ujifunze.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.