Rafiki yangu mpendwa,
Huwa kuna kauli ya utani na kuchekesha kwamba mtu amevamia mtumbwi wa vibwengo, pale anapokuwa anahangaika na mambo ambayo hayawezi. Kwenye safari ya mafanikio, wengi sana wamekuwa wanavamia mitumbwi ya vibwengo na wamekuwa wanajuta kwa ule msoto wanaoupata.
Kwa wote ambao wanatamani sana kufanikiwa, lakini hawafanikiwi, wanakuwa wamevamia mtumbwi wa vibwengo. Wanakuwa wanayachukulia mafanikio poa sana, wanaona ni kitu rahisi ambacho wanaweza kukifikia bila ya shida yoyote.

Lakini kwenye uhalisia, safari ya mafanikio ni moja ya vitu vyenye mateso makubwa sana kwenye maisha. Ili uyapate hasa mafanikio, lazima utokwe na machozi, jasho na damu. Yaani utalia sana, utafanya sana kazi na utaumizwa sana. Hakuna mtu amewahi kufanikiwa bila ya kupitia hali hizo.
Sasa unapokutana na mtu anayesema anataka kufanikiwa, halafu anayaendesha maisha yake kwa mazoea, unajua kabisa huyu anaenda kuvamia mtumbwi wa vibwengo na hataweza kutoka salama. Atakwenda kusulubishwa vya kutosha na atajuta hata kuzaliwa.
Wewe rafiki yangu sitaki ukumbane na hiyo kadhia, nataka wewe uweke mkakati sahihi wa mafanikio ambao utaufanyia kazi kwa uhakika na kuweza kujenga mafanikio makubwa unayoyataka.
Ndiyo maana nakuambia kwenye safari yako ya mafanikio, unapaswa kujipanga vya kutosha, unatakiwa ujitoe hasa, kwa sababu mambo hayatakuwa rahisi. Yaani kama upo kwenye safari ya mafanikio halafu unayaona mambo ni rahisi, jua kabisa unavutwa kwenye mtumbwi wa vibwengo na utakwenda kusulubishwa vya kutosha.
Jiandae kwa kuwa na roho mbaya na ngozi ngumu.
Roho mbaya ni kwa ajili ya kuwakatalia wengine kwenye mambo mbalimbali wanayokuwa wanayataka kwako. Bila ya kusema hapana, hakuna makubwa utakayoweza kuyafanya.
Na ngozi ngumu ni kwa ajili ya kuvuka kusemwa vibaya na kukatishwa tamaa na wengine. Maana utakapoianza tu safari ya mafanikio, utakaribisha kila mwenye maoni mabaya juu yako kukukatisha tamaa.
Rafiki, ninachotaka kukuuliza ni je umedhamiria kabisa kwamba unataka kujenga mafanikio makubwa? Je upo tayari kupambana na kila utakachokabiliana nacho kwenye hiyo safari? Kama majibu ni ndiyo, basi karibu uangalie kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini ambapo utajifunza maandalizi sahihi ya kuwa nayo kwenye safari yako ya mafanikio.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.