Rafiki yangu mpendwa,
Kila kitu kinachozaliwa au kuanzishwa, huwa kina nguvu ya ukuaji ndani yake. Ndiyo maana mtoto mchanga anapozaliwa, watu hawakeshi wakiomba kwamba aweze kukaa, kusimama, kutembea, kuongea na kadhalika. Hayo ni mambo ambayo lazima yatatokea, kwa wakati wake sahihi.
Ila kama muda unakwenda na mtoto hafanyi yote hayo, ndipo sasa wasiwasi unaanza kwamba huyo mtoto ana shida gani. Kwa nini hakui kama anavyopaswa kukua. Ndiyo maana huwa kuna kliniki za watoto ambapo lengo ni kupima maendeleo yao ili waweze kuwa na ukuaji mzuri.

Hivyo ndivyo pia biashara zilivyo, zinapoanzishwa, zinapaswa zikue, maana ndani yake tayari zina nguvu ya ukuaji. Kama biashara imeweza kuuza kwa mteja mmoja, inaweza pia kuuza kwa wateja 10, wateja 100, wateja 1000 na kuendelea. Kwa sababu ni mchakato ule ule ambao umeleta mteja mmoja, ndiyo pia utaweza kuleta wateja wengi zaidi.
Lakini kwenye uhalisia mambo yamekuwa ni tofauti kabisa. Biashara ambazo zinaanzia chini kabisa huwa zinapata ukuaji mwanzoni, lakini baada ya muda ukuaji ule unasimama. Na biashara huwa inabaki hapo kwa muda mrefu na baadaye kuanza kushuka na kufa kabisa.
Cha kushangaza, watu huwa hawajiulizi kwa nini biashara zao zimekwama kukua. Watakazana kuongeza juhudi mbalimbali, lakini ukuaji unakuwa umeganda kabisa. Na hayo yote ni kutokana na watu kutokuzingatia kliniki za biashara. Kwani wangekuwa wameandikisha biashara zao kwenye kliniki ambazo zinapima maendeleo na kuona ukwamishwaji unatokea wapi, zingeweza kukua zaidi.
Rafiki, leo nakwenda kukupa kliniki ya bure kabisa ya kuiwezesha biashara yako kukua mara 10 zaidi ya hapo ilipo sasa. Na kliniki hiyo inahusisha kuondoa mdomo wa chupa (bottleneck) ambao ndiyo umekuwa unazuia biashara yako isikue zaidi.
Unajua kabisa kwamba ukiweka maji kwenye ndoo na ukaweka kwenye dumu, ukitaka kuyamwaga, ya ndoo yatatoka haraka kuliko kwenye dumu. Hiyo ni kwa sababu ndoo ina mdomo wa wazi wakati dumu lina mdomo mdogo. Mdomo mdogo wa dumu ndiyo unazuia maji yasitoke kwa kasi.
SOMA; Mambo 6 Yanayokukwamisha Na Kukurudisha Nyuma Sana Katika Maisha Yako.
Kwenye biashara yako, kuna mahali ambapo mambo yanakwama na hapo ndipo panazuia ukuaji usiende kwa kasi. Na mahali hapo ni WEWE MWENYEWE.
Ndiyo, wewe mwenyewe umekuwa ndiyo mdomo wa chupa ambao unakwamisha ukuaji wa kasi kubwa wa biashara yako. Na unakuwa mdomo wa chupa pale;
1. Umeajiri watu kwenye biashara yako, lakini hawawezi kufanya maamuzi yoyote bila wewe.
2. Kila kitu muhimu kwenye biashara yako unajua wewe tu hivyo lazima watu wakuulize kwanza.
3. Hujawapa watu maelekezo ya kufanya yale uliyowapangia kufanya, tena kwa maandishi ili waweze kuyafuata.
4. Unafurahia pale wateja wanapokuambia wasipokukuta wewe hawanunui.
5. Unawazuia watu wasikosee kwa kuwasaidia kwenye kila kitu.
Rafiki, kwa kusoma hayo unaweza kushangaa, kwamba kama biashara ni yako kwa nini usifanye yote hayo. Na hapo ndipo nataka kukuambia kwamba kufanya yote hayo ndiyo kumekuwa kunaikwamisha biashara yako kukua.
Ili biashara yako iweze kuwa na ukuaji mkubwa, inapaswa kuwa na mfumo unaoeleza jinsi majukumu yote yanavyofanyika, hatua kwa hatua na kisha kuwa na wafanyakazi waliojengewa uwezo wa kutekeleza majukumu hayo kama yalivyoelekezwa. Baada ya hayo wewe mwenye biashara unapaswa kujitoa kwenye mengi kadiri uwezavyo, kusiwepo na jambo lolote linalokwama kama wewe haupo.
Ni kwa kuweza kujenga biashara inayoweza kujiendesha bila hata ya uwepo wako ndiyo unaweza kupata ukuaji mkubwa wa kibiashara.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini tumekuwa na mjadala mzuri kuhusu dhana hii ya mdomo wa chupa unaokwamisha ukuaji wa biashara. Fungua kipindi ujifunze kwa kina ili uache kuikwamisha biashara yako kukua.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.