Rafiki yangu mpendwa,

Umewahi kusikia kauli ya nenda kashangae bandarini, shilingi inazama wakati meli inaelea? Hivyo pia ndivyo unapaswa kushangaa kwa nini watu wawili, waliozaliwa kwenye mazingira yanayofanana na kupitia hali sawa, lakini mmoja anaweza kupata mafanikio makubwa huku mwingine akishindwa kabisa.

Rafiki, unajua pia kwamba meli huwa inaelea kwenye maji, lakini maji hayo hayo yakiingia ndani ya meli, huwa yanaizamisha. Je unajua ni nini kinapelekea maji ambayo yakiwa nje yanaifanya meli ielee, lakini yakipata nafasi ya kuingia ndani yanaizamisha kabisa meli?

Rafiki, hicho tunachokiona kwenye meli na maji, ndiyo pia kipo kwa sisi binadamu na mazingira. Unaweza kuwa unazungukwa na mazingira ambayo ni kikwazo kabisa kwako kupata mafanikio makubwa. Lakini ukiwa vizuri, unaweza kutumia vikwazo hivyo hivyo kujenga mafanikio makubwa.

Unapotumia vikwazo vya mazingira kupata mafanikio makubwa unakuwa kama meli inayotumia maji kuelea.

Kwa upande wa pili ni pale unaporuhusu vikwazo vya mazingira kuingia ndani yako, hapo ndipo unavipa nguvu ya kukuzuia usifanikiwe. Kadiri unavyoruhusu mambo ya nje kuingia ndani yako, ndivyo unayapa nguvu ya kukuzuia. Na hivyo ndivyo unavyokuwa umekwama kufanikiwa.

Unaporuhusu mambo ya nje kuingia ndani yako na ukashindwa unakuwa kama meli inayozama kwa kuruhusu maji kuingia ndani.

Hivi ndivyo tunavyopata tofauti ya mafanikio kati ya watu ambao wapo kwenye mazingira yanayofanana na kuanzia kwenye hali zinazofanana. Matokeo wanayopata yanategemea nini ambacho wamekiruhusu kuingia ndani yao.

SOMA; Waepuke watu wenye tabia hizi 15, ni sumu kwa mafanikio yako.

Rafiki, wajibu wako mkubwa ni kuzuia mambo yote ya nje ambayo ni kikwazo kwa mafanikio, yasiingie ndani yako na kukuzuia kufanikiwa.

Mambo ya nje ambayo ni kikwazo kwako kufanikiwa na hupaswi kuyaruhusu kabisa yaingie ndani yako ni kama ifuatavyo;

1. Mambo ambayo wengine wanafikiria na kusema kuhusu wewe.

2. Kukosolewa na kukatishwa tamaa na watu wengine.

3. Ushindani ambao wengine wanaleta kwako.

4. Hali ya uchumi inayokuwa inaendelea.

5. Kushindwa kupata matokeo ambayo ulikuwa unayataka.

Rafiki, kwa hayo na mengine ambayo yanaendana nayo, haijalishi yanakuzunguka kwa wingi kiasi gani, usiyaruhusu kuingia ndani yako kabisa. Badala yake yatumie hayo kama msukumo kwako kujenga mafanikio makubwa zaidi ili yasipate nguvu ya kukusumbua kabisa.

Kitu kikubwa sana ambacho unapaswa kuwa na tahadhari nacho kwenye safari ya mafanikio ni hofu na wasiwasi. Hivi ni vitu ambavyo huwa vinaanza vikiwa dhaifu, lakini wewe mwenyewe ndiye unayevipa nguvu. Unavipa nguvu pale unapovifikiria kwa muda mrefu. Ili kuyanyima nguvu na yasikusumbue, usiyape muda kabisa, unapopanga kufanya kitu chochote kile, anza kukifanya mara moja. Kadiri unavyoendelea kusubiri ndivyo unavyozidi kuhofia na kushindwa kabisa kuanza.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimekushirikisha jinsi unavyopaswa kuyazuia mambo yote ya nje yasiwe kikwazo na kukuzamisha kwenye safari ya mafanikio. Karibu ufungue kipindi na kujifunza ili uweze kufanikiwa kwa uhakika.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.