3376; Weka hesabu sawa.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Kuna vitu huwa tunajifunza shuleni, ambavyo wakati wa kujifunza unaweza usione umuhimu au matumizi yake, lakini baadaye kwenye maisha vikawa na matumizi makubwa.
Moja ya vitu hivyo ni kuweka hesabu sawa (balance equation) ambayo inafundishwa kwenye hisabati, kemia na hata uhasibu.
Katika masomo hayo, inafundishwa namna ya kuweka hesabu sawa kwa pande mbili zinazokuwa zinategemeana.
Huenda ulisoma hayo kwa ajili ya kujibu mtihani na kuona hutakuja kuyatumia kwenye maisha yako, kwa sababu shughuli zako hazihusiani na hayo mambo.
Lakini leo tunakwenda kuona jinsi ambavyo kuweka hesabu sawa ni hitaji muhimu sana kwenye maisha yako ya kila siku.
Hiyo ni kwa sababu maisha yetu yote yanaongozwa na hesabu moja kuu.
Hesabu hiyo ni;
TOA THAMANI = INGIZA KIPATO.
Kwa kuwa kwa maisha yako yote utakuwa unahangaika na kipato, basi hesabu hiyo utahangaika nayo kila siku ya maisha yako.
Wajibu wako mkubwa ni kuhakikisha pande zote mbili za hesabu zinakwenda sawa.
Kama upande mmoja wa hesabu uko chini kuliko unavyotaka au kutarajia, hasa upande wa kuingiza kipato, unajua unachopaswa kufanya ni kuongeza upande mwingine.
Yaani kama kipato kiko chini, unachohitaji kufanya ni kuongeza thamani unayotoa.
Kwa sababu unalipwa kulingana na thamani unayotoa sokoni.
Kama kipato unachoingiza ni kidogo, ni kwa sababu pia thamani unayotoa ni ndogo.
Au unaweza kuwa unatoa thamani kubwa kwa watu wachache au watu wasiokuwa sahihi.
Ni wewe kuangalia ni wapi hesabu haijakaa sawa na kuisawazisha ili mambo yako yaweze kwenda.
Ukiendelea kuiangalia hiyo hesabu kuu ya maisha utaendelea kuona kwamba hakuna aina fulani ya kazi au biashara iliyotajwa kama ndiyo inayoweza kukupa kipato kikubwa.
Bali kinachohitajika ni wewe kutoa thamani. Hivyo basi, chochote unachofanya, unachopaswa kufanya ni kutoa thamani kubwa kwa watu wengine.
Pesa inafuata thamani. Nukta.
Usihangaike sana na nini unafanya, bali hangaika na thamani gani unayotoa, kwa wingi kiasi gani na kuwalenga watu gani.
Pesa haina hisia wala upendeleo, mara zote inafuata mkondo wake ambao ni thamani.
Kama huzipati fedha za kutosha, ni kwa sababu hesabu yako haijakaa sawa.
Iweke hesabu sawa na mambo yatakwenda sawa.
Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga msimamo wetu ni kutoa thamani kubwa kwa wengine ili kuongeza kipato chetu.
Upande wa thamani ndiyo tuna udhibiti nao na tunaufanyia kazi kwa uhakika kuhakikisha tunatoa thamani kubwa sana, ambapo tumelenga watu sahihi na kwa ukubwa ambao pia ni sahihi.
Kwenye KISIMA CHA MAARIFA hatuhangaiki sana na ni shughuli ya aina gani tunafanya, bali tunahangaika zaidi na ni thamani kubwa kiasi gani tunayotoa na watu gani tunaowalenga kwenye thamani hiyo.
Tunapopewa habari za fursa mpya zinazoingiza sana pesa, huwa hatuangalii huo upande wa pesa pekee, bali pia tunaangalia upande wa thamani.
Kwamba ni thamani gani tunayopaswa kutoa ili kuingiza hizo pesa zinazoelezwa.
Kama upande wa thamani haueleweki, ila upande wa fedha ndiyo unasisitizwa zaidi, tunaelewa wazi kuna kitu hakipo sawa.
Kwa kusimamia vizuri hiyo hesabu kuu ya maisha, huwezi kudanganywa wala kutapeliwa kama inavyotokea kwa wengi.
Maana wengi wamelaghaiwa sana kuacha shughuli zao zilizokuwa sahihi ila haziwaingizii kipato kikubwa na kwenda kwenye mambo waliyoahidiwa yana kipato kikubwa wakati hayana thamani inayoambatana na kipato hicho.
Tunachojua na ambacho tuna uhakika nacho ni kama kipato tunachoingiza hakitutoshelezi, tunachopaswa ni kuweka sawa hesabu yetu kabla hata hatujakimbilia kubadili kile tunachofanya.
Kwa sababu mara nyingi sana tatizo halipo kwenye kile unachofanya, bali linakuwa kwenye hesabu kutokuwa sawa.
Kuweka sawa hesabu yako ya THAMANI = KIPATO ni kazi unayopaswa kuifanya kila siku bila kuchoka.
Na wala hupaswi kuifanya kwa mazoea, kwa sababu mara zote kuna vitu unavyoweza kuboresha zaidi kwenye upande wa thamani na kuathiri upande wa kipato.
Toa thamani kubwa na mwa watu wengi ili kuweza kuingiza kipato kikubwa pia.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe