Habari Matajiri Wawekezaji,

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya programu ya NGUVU YA BUKU, programu maalumu ya kujenga utajiri kupitia uwekezaji wa hatua ndogo ndogo kwa muda mrefu bila kuacha.

Kanuni kuu ya uwekezaji tunayoifanyia kazi kwenye programu yetu ni WEKEZA NA SAHAU. Kanuni hiyo inatutaka tuwekeze kisha tuendelee na mambo yetu mengine, ili tuuache uwekezaji ukikua na kutuzalishia faida.

Lengo letu ni kuwekeza kwa muda mrefu, kuanzia miaka kumi na kuendelea kwa sababu ndiyo kipindi kizuri cha kuweza kuiona faida ya uwekezaji, yaani ule ukuaji halisi wa uwekezaji ambao umefanyika.

Kuelewa vizuri hilo, tuangalie dhana ya msitu na miti. Ukiwa unauangalia msitu kwa mbali, unaona majani ya miti yamefunga kila kitu, huoni kabisa mti mmoja mmoja wala ardhi. Kwa kuangalia msitu kwa mbali, unaweza kudhani hakuna hata mahali pa kukanyaga.

Lakini unaposogea na kuingia kwenye msitu huo, mambo yanabadilika, kwani unaacha kuona msitu na kuanza kuona mti mmoja mmoja. Unaanza kuiona ardhi iliyo wazi na maeneo ambayo yako wazi kabisa. Ukiwa ndani ya msitu huwezi kuuona msitu, unaona mti mmoja mmoja.

DHANA HII INAHUSIKAJE KWENYE UWEKEZAJI?

Unapofanya uwekezaji, ukiwa unaangalia siku kwa siku, wiki kwa wiki na mwezi kwa mwezi, utaona uwekezaji unapanda na kushuka. Kuna wakati utaona thamani ya uwekezaji wako imeshuka. Na kuna wakati utaona thamani imepanda. Hapo upo ndani ya msitu na unachoona ni mti mmoja mmoja.

Unapoangalia uwekezaji wowote kwa kipindi kirefu cha nyuma, kuanzia miaka 10 na kuendelea, unachoona ni ukuaji. Utaona thamani ilianzia chini na kuishia juu, hapo unauona msitu. Ndani ya huo ukuaji wa jumla, ndani yake kuna panda shuka nyingi sana.

Ukiangalia grafu hii ya uwekezaji, utaona kuna kupanda na kushuka kwingi. Lakini ukiangalia kwa ujumla, thamani imepanda kutoka 100 moaka 33,793. Ukiangalia kwa muda mfupi unaona kupanda na kushuka, ila ukiangalia kwa muda mrefu unaona ongezeko kubwa la thamani.

KUTUMIA DHANA YA MSITU NA MITI KUHIMILI UWEKEZAJI.

Kitu kimoja ambacho tutaendelea kukutana nacho kwenye hii safari ya uwekezaji ni kupanda na kushuka kwa thamani ya uwekezaji. Kama tusipokuwa na uelewa na mtazamo wa muda mrefu, tunaweza kuingia taharuki na kuchukua hatua ambazo zinatukwamisha tusinufaike na uwekezaji tunaofanya.

Wajibu wetu ni kuangalia kwa kipindi kirefu, kwa kujipa uhakika kwamba yale tunayoyaona siku kwa siku, ndani ya muda mrefu hayataonekana kabisa, kwani yatakuwa yamefutika kwa ule ukuaji wa jumla unaokuwa umetokea.

Kwa kutumia dhana yetu ya uwekezaji wa kukaa kitako na wekeza na sahau, tunaendelea na mpango wetu wa kuwekeza bila ya kujali mabadiliko ya ndani ya muda mfupi. Tunachojua ni kwamba kwa muda mrefu, thamani ya uwekezaji inakua.

Kwenye programu yetu ya NGUVU YA BUKU tumechagua kuwekeza kwa angalau miaka 10 bila kuacha wala kutoa. Tutakwenda na mpango huo bila kuyumbishwa na mabadiliko madogo madogo, kwa sababu tunajua hayo ni ya muda tu. Thamani kubwa zaidi ipo kwenye muda mrefu ambapo tutafanya uwekezaji huo.

MJADALA WA SOMO.

Karibu kwenye mjadala wa somo hili kushirikisha yale uliyojifunza kwa kujibu maswali yafuatayo;

1. Elezea jinsi ulivyoielewa dhana ya msitu na miti kwenye uwekezaji.

2. Pale uwekezaji unapokuwa unapitia kupanda na kushuka, unapaswa kuangalia nini ili usipate taharuki?

3. Kwa nini kwenye programu ya NGUVU YA BUKU tumechagua kuwekeza angalau miaka 10 bila kuacha wala kutoa?

4. Karibu uulize swali lolote kuhusu somo hili au programu ya NGUVU YA BUKU kwa ujumla.

Shirikisha majibu ya maswali hayo kama ushahidi wa kusoma na kulielewa somo hili ili kwenda kulifanyia kazi na kuwa mwekezaji bora huku ukidumu kwenye programu yetu ya NGUVU YA BUKU.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.