Taasisi ya Brain Research Magazine, walifanya utafiti kuhusu kitu gani kinanasa umakini wa mtu. Waligundua ni jina. Sisi binadamu tunapenda sana kusikia jina letu na sio la watu wengine. Utafiti huo ulionyesha, “upande wa ubongo huwa unasimama, pale unaposikia jina la mhusika likitajwa. Sio jina la mtu mwingine, bali jina lake”.

Kadhalika katika ulimwengu wa biashara ipo hivyo. Kuwa na jina la mteja na kulitumia katika mazungumzo ni kitu muhimu sana. Jina ndio upekee alionao mteja.

Wateja wanapenda kuonekana kama binadamu na sio vitu au wanyama. Maana, wanyama unaweza kuwaita kwa vyovyote vile utakavyo. Lakini binadamu anahitaji kuguswa hisia zake. Unapotumia jina lake unamfanya awe tayari kuendelea kukusikiliza.

Namna nzuri ya kupata jina la mteja msiyefahamiana ni kuanza kujitambulisha wewe kwanza. Naitwa Lackius Robert, wewe ni? Hapo inakuwa rahisi kutaja jina lake na anaona ni wajibu wake kukutajia.

Baada ya kujua jina hilo au kama unalijua ni wewe kutumia jina la mteja wakati wa mazungumzo. Kutumia jina ni muhimu kwa sababu zifuatazo;

Moja; Jina ndio upekee wa mtu.

Dale Carnegie aliwahi kusema; “Jina la mtu ni utu, ni tamu, ndiyo lugha anayopenda kusikia”. Kazi ni kwako kumuuzia sauti anayopenda kusikia.

Mbili; Jina linatengeneza mvuto mbele ya mteja, hali inayowafanya wateja kutaka kujua ofa au habari uliyonayo. Ndiyo maana ni muhimu kulitumia wakati wa mazungumzo. Mteja akifurahia mazungumzo na huduma kiwango cha uaminifu kinaongezeka pia.

Tatu; Kumrudisha mteja katika mazungumzo.
Wateja huweka umakini mkubwa wa kusikiliza kwa umakini pale linapotajwa jina lake. Hivyo, kama unahitaji umakini na mteja litumie mara nyingi zaidi.

Nne; Linaongeza uaminifu na kumchochea mteja kufanya maamuzi.
Hii ni kwa sababu wateja wanapenda kufanya kazi na watu wanaokumbuka majina yao. Wanapoyasikia wanapata furaha na kuona wanathaminiwa, hali inayofanya wachukue hatua za haraka kufanya maamuzi.

Tano; Utaalamu
Tunajua ulimwengu tuliomo, kelele ni nyingi na mambo ni mengi, watu wengi hawaweki umakini kukumbuka majina ya wateja. Wewe unapolitumia unaonekana ni mtaalamu na unawavutia wateja wengi katika biashara yako. Pia, inaonyesha upo makini na kazi unayofanya.

Sehemu za kutumia jina la mteja;

Moja; Mazungumzo ya ana ana au simu.
Mbili; Kwenye SMS au barua pepe.
Kwenye kutumia jina la mteja usiwe mvivu wa kutolitumia wakati wa mazungumzo. Kumbuka ni sauti anayopenda kusikia wakati wote.

Kumbuka; Matumizi sahihi ya jina la mteja ni kitu muhimu sana. Ikiwa hujui linavyotamkwa au kuandikwa, muulize mhusika. Pia, kwenye kulitamka jina la mteja, kuwa na kiasi. Usilitumie kupitiliza, uzito na umakini unapungua.

Kitu kimoja zaidi, hakikisha unapata jina la mteja mwanzoni mwa mazungumzo ili iwe rahisi kulitumia katikati ya mazungumzo. Epuka kuomba jina la mteja mwishoni mwa mazungumzo. Sio sawa, mteja ataona huna umakini.

Kiwango cha chini kutumia jina la mteja ni mara tatu.
Wakati ndiyo huu kumuuzia mteja sauti anayopenda kusikia.

Imeandaliwa na Lackius Robert Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo Na Mwandishi. Tuwasiliane 0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz.