Rafiki yangu mpendwa,
Juhudi kubwa tunazoweka ili kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yetu, lengo pia ni tuwe huru na maisha yetu. Na wengi tunasubiri sana siku tutakayokuwa huru na hatuhitaji kufanya kazi yoyote, tunadhani tutayafurahia sana maisha.
Lakini kama ilivyokuwa wakati tupo shuleni, tulisubiri kwa hamu siku ya kumaliza shule. Tulijiambia tutafurahia maisha kwa sababu hatulazimiki kuamka asubuhi ili kuwahi shule na wala hakuna kusoma kwa ajili ya mitihani.

Wote tunakumbuka jinsi furaha hiyo ilikuwa ya siku chache tu, baada ya muda mfupi tulianza kuchoshwa na ile hali ya kutokuwa na majukumu ya shule. Na kama hatukuwa na majumu mengine yaliyokuwa yanatubana, tunaishia kuwa na maisha ya uchoshi (kuboreka) kuliko maisha ya kufurahia.
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye uhuru wa maisha ambao tunausubiria kwa hamu, siku ambayo hatuhitaji tena kufanya kazi. Tutaifurahia hali hiyo kwa muda mfupi tu na baada ya hapo itaanza kutuchosha. Tutaanza kuona maisha yetu yamekosa maana kwa sababu hatuna mchango kwa wengine.
Kitu muhimu ambacho tunapaswa kukijua tangu mapema ni kwamba ili maisha yetu yawe bora, basi yanapaswa kuambatana na kazi. Maisha bora na kazi ni vitu ambavyo haviwezi kutenganishwa. Kwa sasa kazi unazofanya zinaweza kuwa zinakuchosha na unapambana kupata uhuru ili uachane nazo, lakini hilo halimaanishi usiwe kabisa na kazi yoyote ya kufanya.
Ni wakati ambao huna kazi ya kufanya ndiyo utakaribisha matatizo na changamoto nyingi za maisha yako. Utaanza kuwa na hofu na wasiwasi juu yako mwenyewe. Utaona maisha yako hayana maana. Na inaweza kukupelekea hata kwenye kifo cha mapema, kwa sababu unaona huna tena matumizi hapa duniani.
Kusudi la maisha yetu hapa duniani ni kuwa na manufaa kwa watu wengine na dunia kwa ujumla. Tupo hapa duniani kuifanya dunia kuwa sehemu bora zaidi ya tulivyoikuta. Na hilo linahusisha wewe ufanye kazi.
Maana ya maisha yetu ni kuishi maisha yenye maana. Na maisha yenye maana ni yale ambayo yanawagusa wengine kwa namna nzuri, yanayoleta mabadiliko chanya na yenye manufaa. Kuishi maisha yenye maana kunakutaka ufanye kazi.
Lengo la maisha yetu hapa duniani ni kutumia kila kilicho ndani yetu kabla hatujaondoka. Kuhakikisha kile kilicho ndani yetu tunakitoa katika kipindi cha uhai wetu. Utaweza kutoa kila kilicho ndani yako kupitia kazi.
Na furaha ya maisha yetu inatokana na kufanya vitu ambavyo tunapenda, vyenye maana kwetu na vinavyoturidhisha. Pia pale wengine wanapotushukuru kwa yale tuliyofanya, tunafurahi. Utaweza kufanya unayopenda na kupata shukrani za wengine kupitia kufanya kazi.
Kama ambavyo tumeona hapo juu, hakuna namna tunaweza kuikwepa kazi kwenye maisha yetu. Tunapoanzia chini, tutalazimika kufanya hata kazi tusizopenda ili kuingiza kipato na kujijengea uhuru. Lakini baada ya kuwa huru haimaanishi kwamba hatupaswi tena kutofanya kazi, badala yake tunakuwa huru kufanya kile tunachopenda, hata kama hakituingizii fedha.
Tuchukue mfano mzuri wa mtu wa zama zetu ambaye amefanya hili kwa uhalisia. Bill Gates alianzisha kampuni ya Microsoft na kuikuza sana kiasi cha kuwa tajiri namba moja duniani. Wakati wa kujenga kampuni yake alifanya kazi usiku na mchana kwa miaka mingi bila kupumzika. Baada ya kufikia utajiri wa juu kabisa, alistaafu kwenye kampuni yake. Hapo alikuwa na utajiri wa kuwezesha vizazi vyake vinne kuishi vizuri bila kuhitajika kufanya kazi kabisa. Angeweza kutokufanya chochote na bado akaweza kuendesha maisha yake. Lakini hilo silo alilofanya, kwani kwa miaka zaidi ya 20 amekuwa balozi namba moja wa kutokomeza magonjwa yanayoambukizwa kama polio, malaria, minyoo na mingine. Bill Gates amekuwa anatoa misaada na kusafiri nchi mbalimbali duniani kuhakikisha lengo lake linatimia. Hata nchini Tanzania amekuwa anakuja mara kwa mara kwa ajili ya kazi hiyo. Hivyo licha ya kustaafu kwenye kampuni yake, Bill Gates amekuwa na kazi kubwa zaidi, japo haimlipi, lakini inampa maana kubwa.
Hivyo ndivyo tunavyopaswa kwenda pia. Wakati tunautafuta uhuru, tupambane sana na zile njia ambazo zina uwezo wa kutufikisha tunakotaka kufika. Tukishaupata uhuru tusibweteke, badala yake turudi kufanya yale tunayoyapenda na kuyajali zaidi. Muhimu ni tusijidanganye tu kwamba tukishakuwa huru hatuhitaji tena kufanya kazi. Kazi ni sehemu ya kudumu ya maisha yetu, tuikubali na kwenda nayo vizuri.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA tumekuwa na mjadala mzuri kuhusu umuhimu wa kazi kwenye maisha yetu kama wanadamu. Fungua kipindi hapo chini uweze kujifunza kwa kina na utoke ukiwa na msukumo wa kwenda kuweka kazi kubwa kwa kipindi chote cha maisha yako.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.