3378; Kokotoa kwa usahihi.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Kama umekuwa mfuatiliaji makini wa maarifa tunayoshirikishana, unajua wazi kwamba mafanikio hayaji tu kama bahati.
Bali ni matokeo ya uwekezaji sahihi wa rasilimali mbalimbali zinazohitajika.

Kuna rasilimali kuu nne ambazo kila mtu anapaswa kuziweka ili kuweza kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yake.

Moja ni muda, hakuna mafanikio yanayotokea kwa haraka, lazima muda uwekezwe.

Mbili ni nguvu, hizi ni lazima ziwekwe kwenye kile kinachofanyiwa kazi ili kufanikiwa.

Tatu ni fedha, ambapo ni lazima utumie fedha ili kupata fedha, hata kama unaanzia chini bila fedha, kuna ukuaji huwezi kuufikia bila kuweka fedha za kutosha.

Nne ni juhudi, hizi lazima ziwekwe kwa kiwango kikubwa ili kuleta matokeo ya tofauti ambayo ndiyo yanachangia mafanikio.

Rafiki, rasilimali hizo nne, wengi tayari wanaziweka.
Lakini bado hata wale wanaoziweka, siyo wote wanaopata mafanikio makubwa wanayokuwa wanayataka.

Hiyo inasababishwa na kutokukokotoa kwa usahihi kiasi cha uwekezaji wa rasilimali hizo muhimu zinazohitajika kwenye mafanikio.

Wengi wanawekeza rasilimali hizo, lakini kwa kiwango kidogo sana ambacho hakiwezi kuleta matokeo makubwa wanayotaka.

Kwenye muda ndiyo watu huwa wanashangaza sana, wanataka kupata mafanikio makubwa kwa haraka sana, kitu ambacho hakipo.
Mafanikio makubwa yanahitaji muda mrefu kujengwa, hivyo lazima rasilimali hiyo iwekezwe kwa kiasi sahihi, ambacho ni muda mwingi.

Kwenye nguvu, watu wamekuwa wanatawanya sana nguvu zao kwenye vitu vingi visivyokuwa na tija. Hivyo licha ya kuonekana wanafanya sana, bado hawapigi hatua kubwa.
Anza kwa kuachana na yote yasiyo na tija ili uweze kufokasi nguvu zako kwenye mambo machache.

Fedha inajieleza yenyewe, kila mafanikio yanataka uwekezaji wa fedha uweze kufanyika kwa wakati sahihi na kiwango sahihi. Kuna rasilimali nyingine nyingi utakazohitaji ili kujenga mafanikio unayotaka.

Juhudi kubwa sana zinahitajika kwenye kujenga mafanikio makubwa. Watu wamekuwa wanajidanganya kwamba hawahitaji kufanya kazi kwa nguvu (hard) bali wanafanya kwa akili (smart). Ukweli ni mafanikio makubwa yanatokana na kufanya kazi kwa juhudi kubwa na akili pia (hard and smart).

Ukikokotoa kwa usahihi rasilimali hizo na kuziwekeza bila ya kujizuia, utaweza kujenga mafanikio makubwa unayoyataka.

Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, tunajua dhahiri kwamba tunavuna kile tulichopanda.
Tunajua matokeo tunayopata leo yanatokana na uwekezaji tuliofanya huko nyuma.
Ili tupate matokeo ya tofauti kesho, lazima tufanye uwekezaji wa tofauti leo.
Kwa rasilimali nne za mafanikio, ambazo ni muda, nguvu, fedha na juhudi, tupo tayari kuziweka kwa ukubwa unaohitajika ili kupata mafanikio tunayoyataka.

Msimamo wetu ni kufanya kila kinachohitajika kufanyika ili kupata tunachotaka kupata.
Kwa maana hiyo hatujizuii kwa namna yoyote ile kwenye kuwekeza rasilimali hizo.
Kwa kila matokeo tunayopata tunajitathmini ni rasilimali kiasi gani tumewekeza na kisha kuongeza zaidi.
Tunajua kwa kuwekeza kiwango sahihi cha rasilimali hizo nne ndiyo kunatupa mafanikio yoyote tunayoyataka.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe