Rafiki yangu mpendwa,
Maisha tayari ni magumu, lakini huwa tunatafuta njia za kuyafanya kuwa magumu zaidi ya yalivyo sasa.
Chukua mfano umetoka asubuhi kwenda kwenye shughuli zako, umepanda usafiri wa umma ambapo watu mmebanana. Mtu anakukanyaga na kuchafua viatu vyako ulivyosafisha vizuri. Unamwambia kwa upole kwamba amekukanyaga. Lakini yeye anakujibu kwa ukali; “Wewe mpumbavu nini? Huoni kwamba tumebanana? Kama ungetaka starehe ungepanda gari yako mwenyewe au kukodi teksi.”
Kauli kama hiyo utaichukuliaje kwa siku nzima? Huenda kwa siku nzima utakuwa unafikiria maneno makali ambayo mtu huyo amekuambia. Maneno hayo yatakuvuruga sana na hata kuivuruga siku yako nzima ya kazi. Lakini unadhani aliyekutolea maneno hayo anakuwa anaendaje na siku yake? Huenda atakuwa hakufikirii hata kidogo, badala yake atakuwa amevurugwa na mambo yake mengine.

Hivyo ndivyo tumekuwa tunaruhusu siku zetu kuvurugwa na watu wengine na kuishia kujikwamisha kuishi kwa ubora na kuweza kupata yale tunayoyataka. Katika hali ya kawaida huwa ni rahisi sana kwetu kuvurugwa pale uhalisia wa mambo yanayotokea unakuwa tofauti na matarajio ambayo tunakuwa nayo.
Na kwa sababu mambo mengi yanayotokea yapo nje ya uwezo wetu wa kuyadhibiti, nafasi za kuvurugwa ni nyingi sana. Na hapo bado kuna watu ambao wanakuvuruga kwa makusudi ili ufanye makosa ambayo yatawanufaisha zaidi wao.
Rafiki, vipi kama nitakuambia kuna dawa ya kukuzuia usiweze kuvurugwa na mtu yeyote yule? Vipi kama kuna njia ya kukufanya uendelee kubaki imara licha ya vikwazo mbalimbali ambavyo watu wengine watavileta kwako?
Habari njema ni kwamba njia hizo zipo na wewe unaweza kuzitumia na ukawa na maisha tulivu yanayokuwezesha kufanya makubwa kwenye maisha yako.
Falsafa ya Ustoa, moja ya falsafa bora kabisa za vitendo, inatupa njia za uhakika za kukabiliana na hali ya kuvurugwa na wengine ili tuweze kubaki kwenye utulivu mkubwa.
Njia ya kwanza ya kutumia falsafa ya Ustoa kukabiliana na kuvurugwa na wengine ni kutegemea hali ya kuvurugwa kukutokea. Mara nyingi tunavurugwa kwa kuwa na mategemeo mazuri halafu uhalisia kuja tofauti. Kwa kuanza na matarajio mabaya, hata yanapokuja kwenye uhalisia hayakuumizi na hivyo huvurugwi. Marcus Aurelius anatuambia tunapoianza siku tujiambie kwamba tutaenda kukutana na watu waliovurugwa na wasiojali. Hebu fikiria kama utaianza siku yako kwa matarajio hayo, halafu ukakutana na anayekujibu kama hapo juu, nini kitakuvuruga? Utajiambia tu kwamba nilitegemea hili na kisha kupuuza.
Njia ya pili ya kutumia falsafa ya Ustoa kukabiliana na kuvurugwa na wengine ni kujiuliza nini kimewafanya watu wafanye walichofanya. Marcus tena anatupa mbinu hii, anatuambia pale mtu anapofanya kitu ambacho kinakukwaza, jiulize nini kimepelekea afanye hivyo. Je mtu huyo anajua kuhusu wema na ubaya? Kama hajui, basi unapaswa kumwonea huruma, maana hajui. Na kama anajua, jiulize je ni tofauti na unavyochukulia wewe kuhusu wema na ubaya? Kama jibu ni siyo pia mwonee huruma, maana yupo upande wa kukosea. Na kama jibu ni ndiyo, kwamba mnafikiria sawa, basi hupaswi kumlaumu, kwa sababu hata ingekuwa wewe, ungefanya kama yeye. Kwa kifupi ni ukijiuliza kinachowasukuma watu kufanya wanayofanya, hutaona sababu ya kuvurugwa na wanayofanya, maana wengi hawajui au hawajali.
Njia ya tatu na ya mwisho kwenye somo hili ya kutumia falsafa ya Ustoa kukabiliana na kuvurugwa na wengine ni kujua kwamba muda wetu hapa duniani ni mfupi sana. Ukiangalia muda ambao dunia imekuwepo, ukiangalia wingi wa watu waliopita hapa duniani, tena waliokuwa na madaraka makubwa, lakini leo hii hawapo kabisa na wengi wamesahaulika, unagundua kwamba kujisumbua na mambo madogo madogo ni matumizi mabaya ya maisha yako. Kwa njia hii tunajikumbusha jinsi ambavyo muda wetu ni mfupi na hivyo hatupaswi kuupoteza kwenye kuvurugwa na yale ambayo wengine wamefanya au kutokufanya.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeeleza njia nyingine nzuri za kutumia falsafa ya Ustoa kuepuka kuvurugwa na watu wengine. Karibu ujifunze njia hizo na kuzitumia ili uweze kujenga maisha tulivu na yanayokuwezesha kufanya makubwa.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.