Rafiki yangu mpendwa,
Kuna watu ambao tayari wana uhakika wa kushindwa kwenye maisha yao. Hao ni watu ambao hata iweje, hawawezi kufanikiwa kabisa. Yaani hata kama watakutana na bahati fulani inayowapa mafanikio, bado watatafuta njia ya kupoteza mafanikio hayo na kurudi kwenye maisha yao ya kushindwa.
Na hizi siyo habari ngeni, kwani unawajua watu wengi ambao walipata fursa ya kutoka kwenye maisha ya kushindwa na kwenda kwenye maisha ya mafanikio. Lakini haikuwachukua muda wakajikuta wamerudi kwenye maisha yao ya kushindwa. Tunaona hayo kwa watu wanaoshinda bahati nasibu, wanaopata urithi, wanaopata fidia au mafao.
Wengi ambao wanapata fedha nyingi kwa wakati mmoja, kitu kinachowapa fursa ya kufanikiwa, huwa wanaishia kupoteza fedha hizo na kurudi kwenye maisha ya umasikini. Hiyo ni kwa sababu kwa namna walivyo, wanakuwa wamejihakikishia kushindwa na kubaki kwenye kushindwa.

Kitu kinachowahakikishia watu kushindwa na kubaki kwenye kushindwa ni upumbavu. Upumbavu ni mzigo mkubwa sana ambao umewakwamisha wengi kwenye maisha. Kama unataka kutoka pale ulipo sasa na kufanikiwa, ni lazima uwe tayari kujitofautisha na wapumbavu.
Upumbavu ni kutokujua, lakini kujifanya unajua na hivyo kutokuwa tayari kujifunza. Kwa chochote ambacho huna au hujafikia, kikwazo cha kwanza ni kutokujua, kama hautakuwa tayari kujifunza kutoka kwa wale ambao tayari wameshapata unachotaka, hutaweza kufanikiwa. Usiwe mpumbavu kwa kukataa kujifunza kutoka kwa waliofanikiwa, kuwa mnyenyekevu, jifunze na fanyia kazi yale unayojifunza na utaweza kufanikiwa.
Upumbavu ni kufanya jambo lile lile na kwa namna ile ile halafu kutegemea kupata matokeo ya tofauti. Watu wote wanaoshindwa huwa wanafanya mambo kwa mazoea au kuiga wengine. Kwa kufanya hivyo, wanaishia kupata matokeo yale yale ambayo wamekuwa wanapata au wanayopata wengine. Halafu wanashangaa kwa nini hawafanikiwi. Huwezi kufanikiwa kama haupo tayari kujaribu vitu vipya. Na ili uweze kujaribu vitu vipya, lazima uwe tayari kuchukua hatua za hatari, lazima uwe tayari kupoteza, kitu ambacho wengi hawakiwezi na ndiyo maana wanabaki kwenye mazoea. Wewe usiwe hivyo, jaribu mambo mapya kila wakati, ukikosea ndiyo unajifunza.
SOMA; 1719; Utumwa Kama Zao La Upumbavu…
Upumbavu ni kujaribu kutatua tatizo kwa kutumia fikra zile zile ambazo zimetengeneza tatizo hilo. Upo hapo ulipo sasa kwa sababu ya fikra ambazo umekuwa nazo kwenye akili yako kwa muda mrefu. Kama utaendelea na fikra hizo, hata kama utaweka juhudi kubwa kiasi gani, hutaweza kuvuka hapo ulipo. Fikra zako ndiyo zinazoweka ukomo kwenye nini ambacho unaweza kupata au kufikia. Wapumbavu huwa wanabaki na fikra zile zile na kuishia kupata matokeo yale yale. Wewe kuza zaidi fikra zako, fikiria kwa ukubwa zaidi ya unavyofikiria sasa, ona picha kubwa zaidi ya unayoiona sasa. Usijali sana kama utaweza kufikia au la, wewe anza na kukuza fikra zako na utaweza kukuza matokeo yako.
Rafiki, wajibu wako mkubwa kwenye hii safari ya mafanikio ni kila wakati kujihoji unajitofautishaje na wapumbavu? Kwa hizi sifa za upumbavu ulizojifunza hapa, jikague mara kwa mara kuhakikisha haupo nazo. Ni kwa kuvuka upumbavu ndiyo unakuwa umetua mzigo mkubwa unaokuzuia kufanikiwa.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimeelezea hili kwa kina zaidi na kukupa mwongozo mzuri kwamba kama jambo linaweza kufanywa na mpumbavu, lifanye kuwa marufuku kwako kufanya. Wengi huona wanakwama kufanikiwa kwa sababu hawana watu waliofanikiwa wa kuwaiga. Lakini ukweli ni kwamba, unaweza kuwatumia wapumbavu kufanikiwa, kwa kujizuia kufanya yale ambayo wanayafanya. Karibu ujifunze ili uondokane kabisa na upumbavu na njia yako ya mafanikio iwe nyeupe kabisa.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.