Habari wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,
Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya CHUO CHA MAUZO ambayo yana lengo la kutufanya kuwa wauzaji bora na kufanya mauzo makubwa.
Moja ya masomo tunayopata kwenye mauzo ni ya MAENDELEO BINAFSI ambayo yanatujenga sisi kuwa bora na kutumia uwezo mkubwa ulio ndani yetu kufanya mauzo makubwa.
Huwezi kufanya mauzo makubwa kama wewe siyo muuzaji bora. Na huwezi kuwa muuzaji bora kama wewe siyo mtu bora. Ndiyo maana kauli mbiu yetu ni KUWA MUUZAJI BORA, LAZIMA KWANZA UWE MTU BORA.
Kwenye somo hili unakwenda kujifunza kuhusu kuwa MTULIVU ili uweze kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa. Utulivu ni hitaji muhimu sana kwa mafanikio kwenye kila eneo la maisha yetu. Ukosefu wa utulivu, ambao unasababishwa na kuharakisha na kukosa maandalizi sahihi umekuwa unawavuruga watu na kupelekea wapoteze fursa nzuri za kupata kile wanachotaka.

UNAWAZUIA WATEJA KUNUNUA.
Kama una bidhaa au huduma ambayo wateja wanaihitaji na wanaweza kumudu kuinunua, kama hawanunui ni kwa sababu wewe ndiye unayewazuia kununua.
Unafanya hivyo kutokana na kukosa utulivu kwenye mchakato wako wa mauzo. Unaonekana kuwa mtu ambaye huna maandalizi ya kutosha na kutokujua kwa hakika kile unachouza.
Mambo hayo yanamfanya mteja akose imani na wewe na kusita kufanya maamuzi ya kununua. Mteja anahitaji kukuamini ndiyo awe tayari kutoa fedha kununua unachouza. Kukosa utulivu kunawafanya wateja wakose uaminifu na hivyo kutokuwa tayari kununua.
KUWA NA MAANDALIZI SAHIHI.
Eneo muhimu la kufanyia kazi ili kuwa na utulivu ni kuwa na maandalizi sahihi kwenye mchakato wako mzima wa mauzo. Kabla hujakutana na mteja, hakikisha unajua kuhusu biashara yako na unajua kuhusu mteja. Kwenye biashara yako jua manufaa ya kile unachouza na majibu ya mapingamizi ambayo wateja wanakuwa nayo. Kwa wateja jua maumivu wanayokuwa nayo na jinsi unachouza kinayatatua, pia kuwa na taarifa nyingi zinazowahusu wao binafsi.
Kama kwenye mazungumzo ya mauzo na mteja unajikuta kwenye hali ya kushangaa kutokana na kitu ambacho mteja amekuambia, maana yake hukuwa na maandalizi ya kutosha. Unapaswa kutegemea mambo yote ambayo mteja anaweza kufanya na kuwa na maandalizi sahihi ya kuyakabili.
Kwa mfano mteja akikupa pingamizi, halafu likakushangaza, maana yake hukuwa na maandalizi na pingamizi hilo, hivyo hutaweza kulijibu vizuri na kushindwa kujibu mapingamizi ya wateja ni njia ya uhakika ya kukosa mauzo.
Jiandae kwa kila kitu kinachoweza kutokea ili uweze kukabiliana nacho kwa usahihi pale kinapotokea na kukamilisha mauzo.
PANGILIA MAMBO YAKO YOTE.
Unazijua siku ambazo umechelewa kuamka na kuwa hujapangilia siku yako jinsi ambavyo huwa zinaenda. Kila kitu unafanya kwa kuharakisha, muda unakwenda kasi, mambo hayakamiliki na hata yale unayokamilisha yanakuwa na makosa mengi.
Kuepuka kuwa kwenye hali ya aina hiyo ambayo inavuruga utulivu wako, unapaswa kupangilia mambo yako yote. Anza kwa kupangilia wiki yako nzima ya mauzo, kwa kuweka mambo unayokwenda kukamilisha kwenye wiki hiyo. Ipangilie kila siku yako kabla hujaianza, weka orodha ya yale unayokwenda kutekeleza na muda wa utekelezaji. Kisha fuata mpango uliouweka kama ulivyoweka.
Kukosa mpango kunakufanya uhangaike na kila linalokuja mbele yako, kitu ambacho kinakukosesha utulivu na kupunguza sana mauzo yako. Kadiri unavyojipanga vizuri na kutekeleza mipango yako, ndivyo unavyokuwa na utulivu mkubwa unaokuwezesha kukamilisha mauzo makubwa.
Kila unapojikuta kwenye hali ya kukosa utulivu, jiulize ni mipango gani ambayo umekosa. Rudi kwenye kuweka mipango na kuifuata na utaweza kuwa na utulivu mkubwa.
SOMA; Tabia Tano (5) unazohitaji ili kuwa muuzaji bora.
JITATHMINI BAADA YA KILA HATUA.
Kwa kila mteja unayekuwa naye kwenye mchakato wa mauzo, unapomaliza, bila ya kujali ni matokeo gani umeyapata, jipe muda wa kujitathmini. Na kwenye tathmini hiyo jiulize maswali mawili; Nini ambacho umefanya vizuri na nini cha kuboresha kwenye mazungumzo mengine. Kwa kujifanyia tathmini ya aina hiyo kunakupa nafasi ya kujifunza na kufanya kwa ubora zaidi wakati mwingine.
Wauzaji ambao huwa hawajifanyii tathmini huwa wanakosa utulivu. Wakimaliza mazungumzo na mteja, na kama hawajapata matokeo mazuri wanakuwa kwenye hali ya taharuki. Wanaenda na hali hiyo ya taharuki kwa mteja mwingine na kuzidi kukosa mauzo.
Kama utachukua muda wa kujitathmini kabla ya kwenda kwa mteja mwingine, unapata utulivu mzuri ambao unakujengea ushawishi mkubwa kwenye mazungumzo yanayofuata. Haijalishi umepata matokeo mabaya kiasi gani, usijiruhusu kupeleka mtazamo huo kwenye mazungumzo mengine. Jitathmini na upate utulivu ndiyo uende kwenye mazungumzo mengine.
KAA KWENYE MCHAKATO MARA ZOTE.
Kutokujua nini cha kufanya na kwa wakati gani huwa kunakuweka mtu kwenye hali ya kubahatisha. Unajikuta ukijaribu mambo mengi na ambayo hayakupi matokeo unayotaka. Hilo linakuweka kwenye hali ya kutaharuki na kukosa utulivu. Kutaharuki huko kunapelekea ufanye makosa zaidi na kuzidi kuharibu.
Kuepukana na hali hizo unapaswa kuwa na mchakato sahihi na unaoufuata mara zote. Mchakato sahihi huwa una matokeo ya uhakika na hivyo wajibu wako unakuwa ni kufuata tu mchakato. Hata kama matokeo yanachelewa, huhitaji kuwa na taharuki kama umeufuata mchakato kwa usahihi. Linakuwa ni swala la muda tu kupata matokeo mazuri unayoyataka.
Kuwa na mchakato sahihi na unaoufuata kunakupa utulivu mkubwa unaokuwezesha kufanya mauzo makubwa.
KUWA NA NJIA ZA KUKUPA UTULIVU UNAPOKUWA NA TAHARUKI.
Maisha huwa yana njia nyingi za kutuvuruga. Unaweza kufanya kila kitu kwa usahihi, lakini mambo ambayo yako nje ya uwezo wako yakakwamisha wewe kupata matokeo mazuri uliyokuwa unayatarajia. Hali hiyo inakufanya mtu uvurugwe na hivyo kuondoa utulivu wako.
Ni muhimu kutambua wakati ambao umekosa utulivu na kuwa na njia zinazorudisha utulivu wako. Kuna njia mbalimbali za kurudisha utulivu ambao umeotea ambazo zikitumiwa zinaleta matokeo mazuri.
Kujipa muda wa kupumzika ni moja ya njia hizo. Mara nyingi mtu unavurugwa kirahisi pale unapokuwa na uchovu. Ukijipa mapumziko unapata utulivu.
Kufanya zoezi la tafakari au tahajudi, ambapo unatulia na fikra zako kwa muda fulani ni njia nyingine ya kupata utulivu baada ya kuvurugwa. Zoezi hili linatuliza mawazo yako kwa kuyaweka kwenye kitu kimoja kitu ambacho kinakusaidia sana.
Kwa vyovyote vile, jizuie sana kuchuka hatua ukiwa kwenye hali ya kuvurugwa, kwani unaishia kuharibu zaidi. Hakikisha unapata utulivu kwanza kabla ya kuendelea na mambo yako mengine.
Utulivu ni hitaji muhimu sana kwako ili kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa. Mara zote jijengee utulivu kwenye kila eneo la maisha yako ili uweze kunufaika nao.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.