Rafiki yangu mpendwa,
Jana ulisema kesho utafanya, ambayo kesho yenyewe ni leo. Lakini leo tena unasema utafanya kesho. Hivi unafikiri kilichokuzuia kufanya jana na ambacho kinakuzuia tena kufanya leo, kwa nini kitakuruhusu ufanye kesho?
Rafiki, hakuna uongo mkubwa ambao umekuwa unajiambia kwenye maisha yako kama ‘nitafanya kesho.’ Ni uongo kwa sababu unajua wazi kabisa kwamba kama umeshindwa kufanya leo, nafasi ya kufanya kesho ni ndogo sana, ni kama haipo kabisa.
Lakini umekuwa unaendelea kujiambia hivyo na matokeo yake imekuwa ni kujikwamisha kufanya makubwa ambayo yapo ndani ya uwezo wako kuyafanya.
Rafiki, fanya zoezi hili rahisi sana ambalo litafungua ukweli muhimu wa maisha yako. Iwapo utaambiwa una masaa 24 tu ya kuishi na baada ya hapo utafariki, ni mambo gani utayafanya ndani ya hayo masaa 24? Jipe muda wa kutafakari hilo kabla ya kuendelea, orodhesha kabisa yale yote ambayo utayafanya.

Kama umefanya zoezi hilo, unajua kabisa kwamba kuna mambo ya muhimu ambayo umechagua kuyafanya kwenye masaa yako 24 ya mwisho hapa duniani. Na pia kuna mengi sana ambayo umechagua hutayafanya kwenye muda huo wa kipekee uliobakiwa nao.
Kama umefanya zoezi hilo kwa umakini, huo ndiyo ukweli ambao umekuwa hutaki kujiambia na kuishia kujificha kwenye ‘nitafanya kesho’.
Ukweli ni kwamba, yale uliyopanga kufanya kama ungekuwa na masaa 24 ndiyo mambo muhimu zaidi kwako kufanya. Na yale ambayo hayajaingia kwenye orodha yako ya mambo ya kufanya kwa muda wa mwisho kwako ni ambayo siyo muhimu kabisa.
Sasa basi, hayo ambayo siyo muhimu kwako kufanya ndiyo ambayo umekuwa unajiambia utayafanya kesho. Katika hali ya kawaida, hutaki kujiambia ukweli kwamba mambo siyo muhimu kwako, badala yake unajiambia utafanya kesho.
Tunajua kabisa kwamba kesho huwa haifiki, lakini bado tunaendelea kujiambia tutafanya kesho. Ukweli unaopaswa kujiambia ni kama huwezi kufanya kitu leo, basi hicho siyo kitu muhimu. Ni bora tu ukajiambia ukweli kwamba hutaki kufanya au siyo muhimu kwako kufanya kuliko kujifariji na kesho.
Ninachotaka utoke nacho hapa rafiki yangu ni hiki, pale unapojiambia utafanya kesho, jikamate na kujiambia ‘sitaki kufanya’ au ‘sina mpango wa kufanya.’ Angalau hapo utakuwa umejiambia ukweli na kuacha kujipa matumaini hewa.
SOMA; 1662; Leo Kama Jana Kama Kesho…
Kama kitu ni muhimu, unakifanya leo, unakianza sasa. Kama kitu siyo muhimu, utajiambia utakifanya kesho. Sasa kama kitu hakina umuhimu wa kukifanya leo, kwa nini unakipangia kesho? Kama kitu siyo muhimu hupaswi kukifanya kabisa. Kama kitu hakitaingia kwenye orodha ya vitu vya kufanya ukiwa na siku moja tu ya kuishi usijidanganye nacho.
Kwenye maisha, kujiambia ukweli ndiyo hatua ya kwanza ya kujenga mafanikio makubwa. Kujiambia ukweli kunakufanya uuone uhalisia jinsi ulivyo na kuweza kuukabili ili kupata kile unachotaka. Kujidanganya ni kujifariji kwa muda mfupi, lakini madhara yake ni kushindwa kupata mafanikio makubwa ambayo yako ndani ya uwezo wako kuyapata.
Ni utafanya leo au hutafanya kabisa. Ukianza kujiambia ukweli kiasi hicho, utaweza kufanya makubwa sana kwenye maisha yako.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimekueleza kwa nini unapaswa kuacha kujiambia utafanya kesho, kwa sababu kesho itakuwa ngumu zaidi. Kama umeshindwa kufanya leo ambayo tayari una udhibiti nayo, nini kinakufanya uamini utaweza kufanya kesho ambayo huna udhibiti nayo kabisa? Karibu ufungue kipindi na kujifunza ili uwe mtu wa kufanya kwa wakati na siyo kujidanganya na kesho.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.