Rafiki yangu mpendwa,

Unaweza kuona unapitia magumu kwenye maisha yako kiasi cha kukata tamaa, lakini ukiyaangalia maisha ya wale walioweza kufanya makubwa, unajiona wazi kwamba bado hujafanya kiasi cha kutosha.

Hadithi ya maisha ya Soichiro Honda, aliyekuwa mwanzilishi wa kampuni ya Honda, ambayo inazalisha pikipiki, magari na vifaa vingine vya mashine inatuonyesha jinsi ambavyo mafanikio yanataka uvumilivu mkubwa.

Tangu akiwa mtoto, Honda alipenda sana kazi za mikono na alikuwa akimsaidia baba yake ambaye alikuwa fundi wa baiskeli. Mapenzi yake ya umakenika ulipelekea aachane na elimu ya kawaida na kwenda kujifunza ufundi makenika. Kwa kuwa alipenda sana alichokuwa anafanya, aliweza kuelewa kwa haraka na hivyo kupata kazi kama fundi na baadaye injinia kwenye kampuni ya magari.

Kujituma kwenye kazi kulimpa fursa ya kuwa kiongozi wa tawi la kampuni hiyo, kitu ambacho kilimfanya aingize kipato kikubwa. Pamoja na kipato kikubwa ambacho Honda alikuwa anaingiza, alikuwa na ndoto ya kutengeneza Piston Ring. Alipendekeza kwa kampuni yake kufanya hivyo, lakini haikuwa tayari kwa hilo.

Kwa kuamini kwenye ndoto yake, Honda aliamua kuacha kazi inayomlipa vizuri na kwenda kuanzisha kiwanda chake cha kuzalisha Piston Ring. Alilenga kuuza kwa makampuni makubwa ya magari kama Toyota. Alipopeleka Piston Ring zake sokoni, hazikupokelewa, kwa sababu hazikuwa na viwango. Hivyo ilimlazimu Honda kurudi tena darasani kujifunza namna sahihi ya kuzizalisha kwa viwango vinavyohitajika.

Aliweza kubobea kwenye uzalishaji mzuri wa Piston Ring na kuanza kufanya biashara na makampuni ya magari. Lakini vita ya pili ya dunia ndiyo ilikuwa inaendelea na hivyo kiwanda chake kulipuliwa mara mbili. Mara ya kwanza alijikusanya na kuendelea na uzalishaji. Lakini mara ya pili lilikuwa pigo baya na ambalo lilimwacha akiwa hana fedha kabisa.

SOMA; Jifunze Ung’ang’anizi Wa Rambo Ili Uweze Kupata Mafanikio Makubwa.

Maisha yalikuwa magumu kwake kiasi cha kukosa hata fedha ya kuweka mafuta kwenye gari. Hivyo alitengeneza injini ndogo na kuifunga kwenye baiskeli ili kurahisisha usafiri kwake. Watu wengine walipoona usafiri huo rahisi wa baiskeli nao wakata kuupata. Hivyo alizungumza na maduka ya baiskeli ambayo yalikuwa tayari kumpa baiskeli na yeye kutengeneza injini na kuzifunga kisha kuuza na kuwalipa fedha zao.

Na hivyo ndivyo kampuni ya Honda ilivyozaliwa kwa kuanza kuzalisha pikipiki na baadaye magari na vipuri vingine.

Kupitia maisha ya Honda tunajifunza uvumilivu unaohitajika kwenye safari ya mafanikio. Kwani hiyo ni safari ambayo ina vikwazo na changamoto za kila aina hivyo kama hutakuwa na uvumilivu, utaishia njiani.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA tumekuwa na mjadala kuhusu hadithi hii fupi ya maisha ya Honda kwa masomo ambayo washiriki wameondoka nayo. Ni mjadala wenye mambo mengi ya kujifunza na hatua za kuchukua ili kuweza kufikia mafanikio makubwa licha ya changamoto utakazokutana nazo kwenye safari hiyo.

Karibu usikilize kipindi hapo chini, ujifunze na kwenda kuweka kwenye vitendo ili kubadili maisha yako.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.