3380; Haupo vizuri kihivyo.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Jim Rohn alisema; unalipwa kulingana na thamani unayoitoa sokoni.

Hiyo ina maana kipato unachoingiza sasa, kinatokana na thamani unayotoa kwa watu wengine.

Kama huingizi kipato kikubwa kadiri ya unavyotaka, ni kwa sababu hutoi thamani kubwa.
Au kama kweli unatoa thamani kubwa lakini bado kipato ni kidogo, basi hutoi thamani hiyo kwa watu sahihi.

Kufupisha mambo, kama huingizi kipato kikubwa kama unavyotaka, sababu kuu ni haupo vizuri kama ambavyo unadhani.
Haupo vizuri kwenye hiyo thamani unayoitoa na ndiyo maana watu hawapo tayari kukulipa zaidi.
Na kama unasisitiza upo vizuri kwenye thamani, basi haupo vizuri kwenye kuwafikia watu sahihi ambao wanathamini na kuwa tayari kulipa zaidi.
Ambapo bado ni kitu kile kile, haupo vizuri kihivyo.

Kadiri unavyokubali haraka kwamba haupo vizuri na kuchukua hatua, ndivyo unavyoweza kuboresha yale maeneo ambayo haupo vizuri.
Kama haupo vizuri kwenye thamani basi unachukua hatua ya kutoa thamani kubwa zaidi.
Na kama haupo vizuri kwenye kuwafikia walio sahihi kwa thamani uliyonayo, unachukua hatua ya kuwafikia hao.

Wale wanaokukataa, wanaokataa thamani unayotoa au kukataa kulipia kiasi kikubwa unachotaka wana manufaa kwako kuliko hata wanaokubali.
Kwa sababu hao wanaokataa wanakuonyesha madhaifu yako yalipo na kama ukiyafanyia kazi basi utanufaika zaidi.

Wanaokukataa ndiyo wanakuambia wazi kwamba haupo vizuri kihivyo.
Na wajibu wako ni kuhakikisha unazidi kuwa vizuri kwenye thamani unayotoa na jinsi unavyoifikisha kwa wale unaowalenga ili thamani hiyo iweze kufidiwa kwa usahihi.

Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, tunatumia kila mrejesho kujiboresha zaidi.
Kila matokeo tunayoyapata tunajua ni mrejesho wa soko na hatubishani na mrejesho huo.
Badala yake tunakazana kutoa thamani kubwa zaidi na kuwalenga watu sahihi zaidi.
Kupitia mrejesho wa soko tunachukua hatua zilizo sahihi.

Ndani ya jamii hii tunajua kujifunza ni zoezi endelevu na hata kama tumefika juu kiasi gani, bado tuna nafasi ya kujifunza na kuwa bora zaidi.
Na tunajua mrejesho wa soko ndiyo umebeba ukweli kuliko maoni mengine mengi tunayoweza kupokea kwa watu wengi.

Utayari wa watu kulipia au kutokuwa tayari kulipia ni maoni yenye nguvu zaidi kwako kuliko maoni ya aina nyingine ile.
Wajibu wetu ni kuyapokea maoni kama yanavyokuja na kuyatumia kuwa bora zaidi ya tulivyo sasa.

Ukiwa mnyenyekevu katika kupokea kila mrejesho na kuutumia kuwa bora zaidi, utaendelea kutoa thamani kubwa na hatimaye kuwa vizuri sana kiasi cha wale unaowalenga kutoweza kukupuuza.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe