Rafiki yangu mpendwa,
Kujenga maisha ya mafanikio imekuwa ni kitu kigumu kwa walio wengi.
Kwa wengi ambao wanataka kupata mafanikio makubwa wamekuwa hawayapati. Kwani licha ya kujua nini wanataka na nini wafanye ili kupata wanachotaka, bado wamekuwa wanashindwa kuchukua hatua sahihi na kupata mafanikio.
Kwa upande wa pili, wapo ambao wanajua wanachotaka na wanachukua hatua sahihi na kuyapata mafanikio ambayo walikuwa wanayataka. Lakini baada ya kupata mafanikio hayo wanagundua siyo kitu hasa walichokuwa wanataka. Kwa maneno mengine wanakuwa wamefanikiwa, lakini hawayafurahii mafanikio yao.
Hizo ndizo hali mbili ambazo zimekuwa zinawakuta watu wengi na ndiyo maana mafanikio ya kweli yamekuwa magumu sana.
Hali hizo mbili zimekuwa zinasababishwa na kitu kimoja; kukosekana kwa misingi sahihi ambayo watu wanaizingatia. Misingi sahihi ni kitu muhimu kabisa cha kuanza nacho, kwa sababu hicho ndiyo kinatoa mwongozo sahihi wa nini mtu afanye.
Ukichukua mfano wa kupanda ukuta kwa kutumia ngazi ya kuegesha, haijalishi umepanda urefu kiasi gani, kama ngazi haijawekwa kwenye ukuta sahihi, unaishia kupoteza. Hivyo misingi ya mafanikio ni kuhakikisha ngazi ipo kwenye ukuta sahihi kabla ya kuendelea kupanda.

Mwandishi Stephen Covey kwenye kitabu chake kinachoitwa The 7 Habits Of Highly Effective People amefundisha kwa kina tabia saba ambazo ndiyo misingi sahihi ya kujenga maisha yenye mafanikio. Tabia hizo saba zinaleta ushindi kamili wa maisha ambao ni mafanikio ambayo mtu anayataka.
Ujengaji Wa Tabia.
Kwenye kitabu hicho, mwandishi ameshirikisha kwamba ili kujenga tabia yoyote ile, vitu vitatu vinahitajika;
Moja ni maarifa ambayo ni kujua NINI ambacho mtu anataka kufanya au kuwa. Hii ndiyo tabia yenyewe.
Mbili ni ujuzi ambapo ni VIPI mtu anapaswa kufanya ili kupata au kuwa vile anavyotaka. Hapa ndiyo hatua za kuchukua.
Tatu ni matamanio ambayo ni KWA NINI inayomsukuma mtu kupata au kuwa vile anavyotaka. Hapa ndipo panakuwa na kichocheo cha kufanya.
Hayo matatu yanapaswa kuwepo kwa pamoja ndiyo tabia iweze kujengeka. Watu wengi wamekuwa wanashindwa kujenga tabia muhimu wanazohitaji kwa sababu wanakuwa wanakosa baadhi ya vitu hivyo vitatu muhimu.
Kwenye kujijengea tabia, hakikisha unaleta pamoja vitu hivyo vitatu.
Hali Ya Utegemezi.
Kwenye kitabu mwandishi anaeleza kwamba maisha ni mwendelezo wa hali ya utegemezi.
Huwa tunaanza maisha tukiwa tegemezi kabisa, tukiwa hatuwezi kufanya kitu chochote kile na hivyo kutegemea kufanyiwa kila kitu. Mtoto mchanga anahitaji kufanyiwa kila kitu.
Tunapokua tunafikia hali ya kuweza kujitegemea sisi wenyewe na kufanya mambo tunayoyataka. Kwa wengi hapa huona ndiyo uhuru wa maisha.
Lakini kadiri tunavyozidi kwenda, tunakutana na uhitaji wa kutegemeana na wengine, kwa sababu peke yetu hatuwezi kila kitu.
Hivyo mwendelezo ni UTEGEMEZI, KUJITEGEMEA na KUTEGEMEANA.
Ili mtu aweze kufika ngazi ya kutegemea, lazima kwanza aweze kujitegemea. Hiyo ni kwa sababu ambaye yupo kwenye hali ya utegemezi, hana anachoweza kutoa kwa wengine na hivyo hawezi kutegemeana na wengine.
Hali hizo za utegemezi, kujitegemea na kutegemeana hazitokani na umri, bali zinatokana na ukomavu. Mtu anaweza kuwa na umri mkubwa, lakini kihisia akawa tegemezi kwa wengine. Watu wengi ambao hawafanikiwi ni wale ambao wapo kwenye hali ya utegemezi au kujitegemea.
Mafanikio makubwa yanataka mtu kuwa kwenye hali ya kutegemeana, ambayo ndiyo hali ya juu kwenye mwendelezo wa utegemezi.
Zipo kauli ambazo zinaashiria mtu yupo kwenye ngazi ipi.
Mtu anayetumia zaidi kauli zenye WEWE anakuwa kwenye utegemezi na hivyo kuona wengine ndiyo wanawajibika na maisha yake.
Mtu anayetumia zaidi kauli ya MIMI yupo kwenye hali ya kujitegemea na hivyo kuona yeye mwenyewe ndiye anawajibika na maisha yake.
Mtu anayetumia zaidi kauli ya SISI yupo kwenye hali ya kutegemeana na hivyo anaona akishirikiana na wengine kwenye yale anayofanya.
Jipime kauli zako kwenye maeneo mbalimbali ya maisha yako ili uweze kuona upo kwenye ngazi ipi ya utegemezi.
Ushindi Ndani Na Wa Nje.
Dhana nyingine muhimu sana ambayo tunatoka nayo kwenye kitabu hiki ni ushindi wa ndani na ushindi wa nje.
Mwandishi anaelezea ushindi wa ndani ni ule wa kuweza kujitawala na kujidhibiti wewe mwenyewe. Kwenye ushindi huo unajitambua wewe mwenyewe na kuiishi misingi sahihi inayokufanya wewe kuwa imara.
Ushindi wa nje ni ule wa kuweza kushirikiana vizuri na watu wengine. Unakuwa umepata ushindi huu pale unapokuwa umejenga ushawishi mkubwa kwa watu wengine. Kwenye ushindi huu pia kuna misingi yake ya kuzingatia.
Watu wengi wamekuwa hawafanikiwi kwa sababu wanaanza kuhangaika na ushindi wa nje kabla ya ushindi wa ndani. Hivyo hata wakipata ushindi huo wa nje umekuwa haudumu kwa sababu ndani wanakuwa watupu.
Wajibu wetu ni kuanza kwa kupata ushindi wa ndani kisha kwenda kwenye ushindi wa nje.
Kitabu hiki cha The 7 Habits Of Highly Effective People kimepangiliwa kwa njia hiyo, tabia tatu za kwanza ni za kujijengea ushindi wa ndani na tabia tatu zinazofuata ni za kujenga ushindi wa nje. Tabia moja ya mwisho ni ya kuleta pamoja ushindi mkuu wa maisha.
Uaminifu Ni Msingi Mkuu.
Katika misingi yote muhimu ya kujenga mafanikio, uaminifu ni msingi mkuu ambao mwandishi ameusisitiza sana. Anaeleza kama msingi huo usipokuwepo, hakuna msingi mwingine unaoweza kufanya kazi. Kuanzia kwenye ushindi wa ndani na ushindi wa nje, uaminifu unahitajika sana.
Mwandishi anatoa mfano wa benki ya akaunti ya hisia, ambapo kila unapofanya jambo la kujenga uaminifu unakuwa umeweka fedha kwenye benki hiyo. Na unapofanya jambo la kubomoa uaminifu, unakuwa umetoa fedha kwenye akaunti hiyo. Mafanikio yako kwenye maisha yanategemea sana salio lako kwenye hiyo akaunti. Kama una salio jingi, yaani unaaminika kwa mambo ambayo umekuwa unafanya, unakuwa na fursa ya kupata mengi unayotaka. Lakini kama huna salio, maana yake huaminiki na inakuwa vigumu kwako kupata unachotaka. Wengi kwenye maisha wanakuwa wanatoa fedha kwenye hiyo akaunti kiasi kwamba wanakuwa hawana akiba yoyote ya kuwapatia chochote wanachokuwa wanataka.
Kwa kila unachofanya, kumbuka dhana hii ya akaunti ya benki ya hisia, kama linafanya uaminike zaidi au linavunja imani yako na kupelekea ugumu kwako kupata yale unayotaka.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA tumejadiliana kwa kina misingi hii muhimu tunayopaswa kujijengea ili kupata mafanikio makubwa tunayoyataka kwenye maisha yetu. Karibu usikilize kipindi hicho hapo chini ili uendelee kujifunza na kuchukua hatua sahihi ili kupata mafanikio unayoyataka kwenye maisha.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.