Habari wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,
Karibuni kwenye mwendelezo wa masomo yetu ya CHUO CHA MAUZO, masomo yanayotujenga kuwa wauzaji bora kwa kutupa maarifa na hatua za kuchukua ili kukuza zaidi mauzo.
Maeneo makubwa mawili tunayoyafanyia kazi kwa uhakika ili kukuza mauzo ni USAKAJI ambao ni kutengeneza wateja wapya tarajiwa mara zote na UFUATILIAJI ambapo ni kuwafuatilia wateja kwa karibu bila kukoma.
Kwenye usakaji, kauli mbiu yetu kuu ni USAKAJI NDIYO PUMZI YA BIASHARA, UNAPASWA KUFANYIKA MARA ZOTE. Kila wakati kwenye biashara ni wa kusaka wateja wapya na hivyo kila muuzaji anapaswa kutumia njia mbalimbali kukamilisha hilo.
Kwenye somo hili tunakwenda kujifunza jinsi ya kuwafikia wateja wengi kwa kutumia matangazo ya mitandao ya kijamii.
Kwenye somo la nyuma la kufikia wateja wengi kwa maudhui ya mitandao ya kijamii tulijifunza jinsi ambavyo mitandao ya kijamii inatumika na watu wengi kwa sasa na hivyo kuwa na ushawishi mkubwa.
Kwenye somo hili tunakwenda kujifunza jinsi ambavyo kwa kutumia gharama kidogo, unaweza kuwafikia wengi zaidi, tena ambao unawachagua wewe mwenyewe.

Tofauti Ya Maudhui Na Matangazo.
Maudhui ni njia nzuri ya kuwafikia watu kupitia mitandao ya kijamii. Pale maudhui yanapokuwa mazuri, watu wanaweza kusambaziana na yakawafikia watu wengi zaidi. Lakini hicho ni kitu ambacho huwezi kukidhibiti, unaweza kutoa maudhui, lakini hujui yatasambaa kiasi gani.
Ili kudhibiti nani wa kufikiwa na maudhui unayotoa, unapaswa kulipia. Kwa kulipia maudhui hayo, unachagua yafikishwe kwa watu wa aina gani na mtandao husika unapeleka maudhui hayo kwa watu hao.
Matangazo ya kulipia ni njia ya kuhakikisha maudhui yanawafikia watu wengi zaidi kwa uhakika kuliko tu kutegemea maudhui yasambae yenyewe. Na kadiri unavyochagua vizuri watu unaowalenga na kuweka kiasi kikubwa cha fedha, ndivyo maudhui hayo yanavyofikishwa kwa watu wengi zaidi.
Hivyo pamoja na kutoa maudhui mazuri kupitia mitandao ya kijamii, bado unalazimika kulipia matangazo ili uweze kuwafikia watu wengi zaidi waliopo kwenye mitandao hiyo. Kwa kulipia unakuwa na uhakika zaidi wa watu wangapi umewafikia.
Mitandao Ya Kulipia Matangazo.
Kuna mitandao mingi ya kijamii ambayo watu wanaitumia. Na karibu mitandao yote ina njia ya kulipia matangazo ili kuwafikia watumiaji wengi wa mitandao hiyo.
Kuchagua mitandao ambayo utaweka matangazo ya kulipia kunapaswa kuanza na wateja unaowalenga wanapatikana zaidi kwenye mitandao ipi. Na njia nzuri ya kujua ni kuanza kwa kuweka maudhui ya bure kwenye mitandao mbalimbali, kisha kuangalia mitandao inayofanya vizuri kwa aina ya biashara unayofanya na wateja unaowalenga. Hiyo ndiyo mitandao utakayoichagua kuweka matangazo ya kulipia.
Kwa biashara nyingi kwa mazingira ya Tanzania, mitandao ifuatayo ni mizuri kwa kuweka matangazo.
Moja ni mtandao wa Facebook, huu una watumiaji wengi na ambao umri wao ni mkubwa hivyo kuwa wateja wazuri zaidi kuliko mitandao mingine. Pia mtandao huo una machaguo mengi ya aina ya matangazo na kuwafikia watu.
Mbili ni mtandao wa Google, huu ndiyo sehemu ya kwanza watu kwenda kutafuta kitu wanapotaka kupata taarifa zaidi. Kwa kuweka matangazo yako kwenye mtandao wa Google yanaonyeshwa kwa wale wanaotafuta vitu vinavyoendana na kile unachouza wewe.
Tatu ni mtandao wa Instagram, huu ni mzuri kwa bidhaa au huduma zinazohusu mwonekano wa watu. Watumiaji wengi wa mtandao huo wanajali sana mionekano yao na hivyo kushawishika zaidi na matangazo ya aina hiyo.
Mitandao mingine kama X (twitter), TikTok, LinkedIn n.k. ina fursa za kulipia matangazo na kuwafikia watumiaji waliopo, japo wanaweza wasiwe wengi kulingana na aina ya biashara ambayo mtu anafanya. Kwa biashara za kitaalamu (professional) LinkedIn ni mtandao mzuri kuwafikia watu sahihi kwa sababu wanautumia zaidi huo.
Tofauti Ya Matangazo Ya Mitandao Ya Kijamii Na Ya Kawaida.
Matangazo ya kawaida, ambayo kwa sehemu kubwa yanafanywa kwenye vyombo vya habari yamekuwepo kwa miaka mingi. Matangazo ya mitandao ya kijamii hayana muda mrefu, lakini yamekuwa na nguvu kuliko ya vyombo vya habari.
Matangazo ya mitandao ya kijamii yanatofautiana na matangazo ya kawaida kwa njia zifuatazo;
Moja ni matangazo ya kawaida yanaenda kwa watu wote hata wasiohusika, ni vigumu kuchagua watu gani wafikiwe na tangazo la redio au TV. Matangazo ya mitandao ya kijamii unachagua kabisa watu gani unataka wafikiwe, kuanzia walipo, umri, jinsia na mambo wanayopendelea. Kwa njia hiyo matangazo yanakuwa na ushawishi zaidi.
Mbili ni gharama za matangazo. Matangazo ya kawaida huwa yana gharama kubwa kulingana na chombo kilichotumika. Matangazo ya mitandao ya kijamii huwa yana gharama ndogo sana. Matangazo kama ya Facebook yanaanza na kiasi cha chini cha dola moja kwa siku. Hivyo kila aina ya biashara inaweza kutumia matangazo ya mitandao ya kijamii kuwafikia wateja wengi.
Tatu ni kupata ripoti ya ufanisi wa matangazo na kuweza kuboresha. Matangazo ya vyombo vya habari hayana ripoti ya ufanisi ambayo unaweza kuitumia kuboresha zaidi matangazo yako. Matangazo ya mitandao ya kijamii yanakuwa na ripoti ya ufanisi wa kila tangazo, kuanzia gharama zilizotumika, watu waliofikiwa, waliochukua hatua n.k. Unaweza kukusanya taarifa nyingi sana kwa matangazo ya mitandao ya kijamii na ambazo ukizitumia utafanya kwa ubora zaidi.
Mpango Wa Matangazo Kwenye Mitandao Ya Kijamii.
Ili kufikia wateja wengi na kuwashawishi kununua kile unachouza, unapaswa kuwa na mpango mzuri wa matangazo kwenye mitandao ya kijamii.
Hatua ya kwanza kwenye mpango ni kujua matokeo unayotaka kupata. Matangazo yanatofautiana kulingana na matokeo unayotaka. Matokeo yanaweza kuwa ni kujulikana (awareness), kutengeneza wateja tarajiwa (leads generation) au kuuza moja kwa moja (direct sales).
Hatua ya pili ni kuandaa tangazo ambalo litaleta matokeo mazuri kulingana na lengo. Tangazo linaweza kuwa la maandishi, picha na video kulingana na aina ya biashara na kile kinachouzwa. Tangazo zuri linapaswa kujumuisha vyote, maelezo mafupi, picha na video. Uzuri ni matangazo ya mitandao ya kijamii yanaruhusu kuweka picha na video zaidi ya moja kwenye tangazo moja.
Hatua ya tatu ni kuchagua hatua ambazo anayefikiwa na tangazo anapaswa kuchukua. Kwa tangazo la kujulikana, inaweza kuwa ni kutembelea tovuti au kujiunga na ukurasa au kundi la biashara. Kwa matangazo ya kutengeneza wateja tarajiwa, hatua ya kuchukua inakuwa ni kutuma taarifa zao au kuwasiliana moja kwa moja na biashara kwa njia ya ujumbe au simu. Kwa matangazo ya kuuza, mtu anaweka oda moja kwa moja.
Hatua ya nne ni kuweka tangazo kwa kuchagua sifa za unaowalenga na kulipia kulingana na muda ambao unataka tangazo hilo liweze kuruka. Kadiri unavyochagua walengwa kwa usahihi, ukalipa kiasi kikubwa na kuweka tangazo kwa muda mrefu ndivyo matokeo yanavyokuwa mazuri.
Hatua ya tano ni kufuatilia mwenendo wa tangazo kwa ripoti zinazotolewa kila siku. Kila siku mtandao husika huwa unatoa ripoti za mwenendo wa tangazo, unapaswa kufuatilia ripoti hizo ili uone kama unapata matokeo uliyotarajia. Kama matokeo ni tofauti na matarajio, unaweza kuchukua hatua za kuboresha tangazo hilo na likaendelea au kulisimamisha kabisa na kuweka tangazo jingine.
Kujifunza hatua zote hizo tano kwa maelezo, picha na video, ingia kwenye KUNDI MAALUMU LA MATANGAZO YA META. Bonyeza MAANDISHI HAYA kuomba kuingia kwenye kundi na utapewa nafasi kama tayari upo kwenye CHUO CHA MAUZO. Kama haupo kwenye CHUO CHA MAUZO wasiliana na namba 0678 977 007 upewe maelekezo ya kujiunga.
Mambo Ya Kuzingatia Ili Kupata Matokeo Mazuri Kwenye Matangazo.
Licha ya matangazo ya mitandao ya kijamii kuwa njia nzuri ya kuwafikia wateja wengi kwa gharama kidogo, siyo rahisi kufikia hilo. Kuna changamoto mbalimbali ambazo usipoweza kuzivuka zoezi zima litaonekana kuwa ni upotevu wa muda.
Changamoto kubwa ya matangazo ya mitandao ya kijamii ni kupata watu wengi ambao siyo wateja na wala hawana umakini. Kwa sababu watu wengi wanatumia mitandao ya kijamii kama sehemu ya kupoteza muda na kuburudika, utawapata wengi ambao watafungua tangazo lako lakini hawafai kabisa kuwa wateja wako. Hivyo unapaswa kuwa na mchakato wa kuwachuja wale wote wanaotoka kwenye mtangazo ya mitandao ya kijamii na kujua wapi ni wateja halisi na wapi siyo.
Jua kabisa katika wengi ambao wanakuja kwa matangazo ya mitandao ya kijamii, wachache sana ndiyo wenye sifa ya kuwa wateja wa biashara yako. hivyo usikate tamaa pale unapokutana na wengi ambao hawafai, wewe endelea kufikia wengi kwa matangazo hayo na kuwachuja, utaweza kuwapata wachache ambao watakuwa wateja wazuri sana kwa biashara yako.
Kitu kingine muhimu cha kuzingatia ili kupata matokeo mazuri kwa matangazo ya mitandao ya kijamii ni kufanya kwa muda mrefu na kuwa na ufuatiliaji wa karibu. Usifanye matangazo machache, kwa kiasi kidogo na kwa muda mfupi kisha ukakata tamaa na kuona hayafanyi kazi. Huwa kuna ushauri kwamba kama hujatumia zaidi ya dola elfu 1 kwenye matangazo ya mitandao ya kijamii, bado hujajua jinsi ya kuyafanya kwa usahihi. Hivyo endelea kuweka matangazo, kujifunza na kuboresha ili kupata matokeo mazuri. Usikate tamaa haraka kwa kukosa matokeo mazuri mwanzoni.
Kwa wateja unaowapata kutoka kwenye matangazo ya mitandao ya kijamii, imani yao huwa ni ndogo, hasa pale wanapokuwa mbali na biashara. Njia pekee ya kuwajengea imani ni kuwa na ufuatiliaji wa karibu na usiokoma. Wengi mwanzoni wanaweza kuonekana hawana sifa au uhitaji, lakini kadiri utakavyokuwa unawafuatilia, ndivyo wanazidi kukuelewa na kuonyesha uhitaji wao. Hivyo usiwaache moja kwa moja wateja wanaotokana na matangazo ya mitandao ya kijamii, waweke kwenye mfumo wako wa ufuatiliaji kama kuwatumia ujumbe mfupi kwa wengi (bulk sms) pamoja na kuwaweka kwenye broadcast ili mara kwa mara wawe wanasikia kutoka kwako.
Matangazo ya mitandao ya kijamii yana nguvu kubwa ya kuwafikia watu wengi na kuwashawishi kununua, lakini siyo kwa urahisi kama wengi wanavyochukulia. Yanahitaji kuwekewa kazi ya uhakika ili yaweze kuleta matokeo mazuri. Fanyia kazi haya uliyojifunza hapa ili uweze kutumia nafasi ya mitandao ya kijamii kufikia watu wengi, kutengeneza wateja tarajiwa wengi, kuwafuatilia kwa uhakika na kufanya mauzo makubwa.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.