Rafiki yangu mpendwa,
Huwa kuna utani unasema kwamba mtu mmoja akisema wewe una matatizo, anakuwa na chuki na wewe. Watu watatu wakisema wewe una matatizo wamekula njama. Lakini watu kumi wakisema wewe una matatizo, basi ni kweli una matatizo.
Rafiki, imekuwa ni kawaida kwa walio wengi kulalamika na kulaumu pale wanaposhindwa kupata mafanikio makubwa wanayokuwa wanayataka. Kila wanaposhindwa wanaangalia nani kachangia kwenye kushindwa kwao.

Kwa sababu atafutaye hakosi, wale wanaotafuta wa kuwalalamikia na kuwalaumu kwa kutokufanikiwa kwao, huwa hawakosi wa kuwapelekea lawama hizo. Lakini mwisho wa siku wanachopata ni nini? Hakuna zaidi ya kubaki pale wanapokuwa, ambapo ni kushindwa.
Rafiki, kitu kimoja ninachotaka kukuambia ni kwamba kama mpaka sasa hujapata mafanikio makubwa unayoyataka ni kwa sababu unajikwamisha wewe mwenyewe. Na kikubwa unachojikwamisha nacho ni tabia yako ya kutafuta watu wa kuwalaumu na kuwalalamikia kwenye yale ambayo umeshindwa.
Huwa kuna nukuu ya Bill Gates inayosema kuzaliwa masikini siyo tatizo lako, maana huchagui uzaliwe na wazazi gani. Lakini kufa masikini, hilo ni tatizo lako kabisa. Na siyo tu tatizo, bali uzembe wa hali ya juu sana. Najua kama bado hujafikia mafanikio makubwa unaweza usipendezwe na hilo, lakini ndiyo ukweli.
SOMA; Kama unataka kuondoka kwenye umasikini, waepuke masikini kama ukoma.
Ukitaka kuona kwa nini ni uzembe kufa masikini hata kama ulizaliwa masikini, umri wa utoto ambapo ndiyo ulikuwa chini ya wazazi wako ni miaka 18 tu. Au tunaweza kuweka mpaka hata 21 ili kuhakikisha umekomaa vizuri. Sasa hebu chukua umri wako wa sasa na utoe miaka hiyo, halafu uone kama kwa miaka yote hiyo umeshindwa kujenga mafanikio makubwa unayotaka, nini hasa kimekukwamisha?
Imekuwa ni kawaida kuwakuta watu wenye umri wa zaidi ya miaka 30 wakiwa wanawalaumu wazazi wao kama sababu ya wao kutokufanikiwa. Watu hao unakuta wana miaka zaidi ya 10 ambayo hawapo tena chini ya wazazi wao, kwa nini wameshindwa kufanya kitu kwenye huo muda? Jibu lipo wazi, ni kwa sababu wamekuwa wanajikwamisha wao wenyewe kupata mafanikio makubwa wanayoweza kuyapata.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimekushirikisha swali moja muhimu sana la kujiuliza na kujipa majibu ili uweze kuona wapi unajikwamisha wewe mwenyewe na jinsi ya kujikwamua kutoka hapo. Swali hili linarudisha uwajibikaji kwako mwenyewe na kukuondoa kwenye tabia ya kulalamika na kulaumu wengine.
Karibu ujifunze kwa kina kwenye kipindi hicho cha ONGEA NA KOCHA hapo chini. Usikubali tena kuendelea na hayo maisha ambayo hayana mafanikio makubwa unayoyataka wakati ipo ndani ya uwezo wako kufanya makubwa. Jifunze sasa na uchukue hatua ili kuleta mapinduzi makubwa kwenye maisha yako.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.