Kwenye ufuatiliaji wa wateja, kuna taarifa muhimu unahitaji ili kurahishisha suala hilo. Katika hali hiyo, mteja anapaswa kukupa taarifa hizo. Sio wateja wote watakuwa tayari kufunguka. Je, unafanyaje ili kumfanya mteja aongee na kukupa kile unachotaka?

Ipo njia moja tu ya kufanya hivyo, ambayo ni kumuuliza maswali. Unapomuuliza maswali akayajibu, anajikuta akiongea sana kitu kinachomfanya akupe taarifa ambazo zinakupa urahisi na kumshawishi kununua.

Kwenye mazungumzo yoyote ya mauzo, anayeongea sana ndiye ambaye huwa anaishia kushindwa. Hiyo ina maana kwamba, kama mtu wa mauzo ndiye anayezungumza sana basi atashindwa kuuza. Na kama mteja ndiye anayezungumza sana, atashawishika kununua. Huo ndio ukweli unaopaswa kuujua na kuufanyia kazi.

Kwanini Tunauliza Maswali?

Moja; Kumfanya mteja aweke umakini kwenye mazungumzo mnayofanya.
Unapozungumza na mteja na wewe ukawa ndiyo mwongeaji mkuu, mteja anaweza asiweke umakini kwenye kile unachoongea. Unapopunguza kuongea wewe na ukamuuliza mteja maswali, katika kuyajibu inabidi aweke umakini kwenye kile anachoongea, kitu ambacho kinafanya awe rahisi kushawishika.

Pili; Ni Udhibiti.
Kwenye mazungumzo ya mauzo, anayeuliza maswali ndiye anayekuwa na udhibiti wa mazungumzo hayo, kitu kinachomfanya awe na ushawishi zaidi. Nimeelezea hapo juu kuwa; kama muuzaji anaongea sana, ni ngumu kuuza. Ni bora mteja aongee sana kuliko muuzaji. Na namna nzuri kumfanya aendelee kuongeza zaidi ni kupitia maswali unayomuuliza.

Tatu; Maelezo binafsi.
Kwenye mauzo wanachokipenda sana wateja ni kujielezea wenyewe. Watu wanapenda kuzungumzia mambo yanayowahusu kuliko kusikiliza wengine wakizungumzia mambo yao. Unapowauliza wateja maswali, wanajieleza zaidi wao wenyewe, kitu kinachowafanya wajifikirie zaidi na kuwa kwenye hali ya kushawishika kwa urahisi licha ya ukinzani.

Kwenye mauzo nidhamu kuu ipo kwenye uulizaji. Unapouliza kuna namna unamfanya mtu achukue hatua kidogo hasa kutoa majibu. Uzuri ni kwamba, binadamu tupo tayari kutoa majibu juu ya maswali tunayouliza.

Mambo muhimu kuzingatia wakati wa uulizaji maswali;

Moja; Maandalizi
Kabla ya kumfuatilia mteja, jiandae vema jua mawili matatu kuhusu mteja huyo Ili ujue mahali pa kuanzia.

Pili; Heshima
Usiulize maswali yasiyo ya muhimu mbele ya mteja. Fokasi kwenye mahitaji yake, ili swali likusogeze karibu na mauzo.

Tatu; Udadisi
Uliza maswali kuendana na hali ya mteja, maswali mengi yawe ya kujielezea.

Nne; Msimamo.
Usiogope kuuliza maswali ili kupata taarifa zaidi.

Uulizaji wa maswali kwenye mauzo unakusaidia kupata kile tunachotaka. Kama muuzaji unapaswa kuuuliza maswali mengi kadiri unavyoweza. Kitu cha kuzingatia ni usahihi wa maswali unayomuuliza mteja.

Maswali unayouliza hakikisha yapo kwenye aina hizi;

Moja; Maswali ya wazi.
Haya ni yale maswali ambayo yanamfanya mtu atoe maelezo yake juu ya kitu fulani. Maswali haya hayana majibu ya ndiyo au hapana, badala yake mtu anatakiwa kutoa maelezo. Haya ni maswali mazuri kupata taarifa nyingi kutoka kwa mtu. Kutegemea na uulizaji wa maswali hayo, unaweza kupata taarifa nyingi na za tofauti kutoka kwa mtu huyo.

Mbili; Maswali yaliyofungwa.
Haya ni maswali ambayo majibu yake ni ndiyo au hapana. Haya ni maswali ambayo yanaulizwa kukamilisha kitu, hayana maelezo ya ziada. Maswali ya aina hii hayawezi kukupa taarifa nyingi kuhusu mtu, hivyo ni mazuri kwenye ufanyaji wa maamuzi, lakisi siyo mazuri kwenye kukusanya taarifa na kumjua mtu kwa kina.

Faida za kuuliza maswali;

Moja; Unajua maumivu ya mteja.
Hii ni kupitia maelezo anayotoa mteja.
Mbili; Kufanya mauzo ya ziada.

Tatu; Kuthibiti mapingamizi.

Nne;  Kuboresha mahusiano.

Muhimu; Kiwango cha chini kuuliza maswali kwa mteja ni kuanzia matatu. Yasiwe mengi sana, wala machache, lakini yakusogeze karibu na mauzo. Je, unauliza maswali kwa wateja wako? Wakati ndio huu kuongeza ushawishi kupitia uulizaji wa maswali sahihi.

Imeandaliwa na Lackius Robert Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo Na Mwandishi. Tuwasiliane 0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz.