Rafiki yangu mpendwa,
Mafanikio unayoyataka kwenye maisha yako, hutaweza kuyapata peke yako. Badala yake unawategemea sana wengine katika kuyapata mafanikio hayo. Ili uweze kwenda vizuri na wengine katika kuyapata mafanikio unayoyataka, kuna vitu viwili vikubwa unavyopaswa kuvifanyia kazi ambayo ni maelewano na ushirikiano.

Mwandishi Stephen Covey kwenye kitabu chake cha The 7 Habits of Highly Effective People ameshirikisha mambo hayo mawili kwenye tabia ya tano na ya sita kwenye tabia saba alizofundisha. Karibu tujifunze tabia hizo na jinsi ya kujijengea kwenye maisha yetu ili kupata mafanikio makubwa.
TABIA YA TANO; WAELEWE WENGINE KWANZA ILI KUELEWEKA.
Watu wengi wanaoshindwa kwenye maisha huwa wanalalamika kwamba watu wengine hawawaelewi. Lakini ambacho wanakuwa hawapo tayari kufanya ni wao kuanza kuwaelewa watu wengine. Hapo ndipo udhaifu wa wengi ulipo na unaowazuia kufanikiwa.
Kuwaelewa wengine kunaanza na kuwa msikilizaji. Na siyo tu kuwa msikilizaji, bali msikilizaji makini na anayejali.
Kwa bahati mbaya sana, tulipoenda shule tulifundishwa jinsi ya kusoma, kuandika na kuhesabu. Lakini hatukufundishwa jinsi ya kusikiliza, kitu ambacho ni muhimu sana kwenye kujenga mahusiano mazuri na watu wengine.
Wengine wameenda mbali mpaka kujifunza jinsi ya kuongea kwa ushawishi, lakini swala la kusikiliza kwa ushawishi limekuwa halifundishwi. Katika yote tunayofanya katika kuhusiana na wengine, kusikiliza kwa usahihi ni kitu chenye nguvu sana.
Watu wengi wanapokuwa wanazungumza na wengine, wamekuwa hawasikilizi kabisa. Badala yake wanasubiri zamu yao ya kuongea ifike ili waongee. Wakati wengine wanaongea wao hawasikilizi kuelewa, bali wanakuwa wanajiandaa nini watajibu. Kwa njia hiyo mawasiliano yanakuwa mabovu na mahusiano kuvunjika.
Kuna ngazi mbalimbali za usikilizaji ambazo watu huwa wanapitia.
Ngazi ya kwanza ni kupuuza, hapa mtu hasikilizi kabisa, wakati wengine wanaongea wao wanakuwa wanafanya mambo yao.
Ngazi ya pili ni kuigiza kusikiliza, hapa mtu anajifanya kama anasikiliza, kwa kuitikia kwa maneno na vitendo, lakini kiuhalisia anakuwa hasikilizi.
Ngazi ya tatu ni kuchagua ya kusikiliza, hapa mtu anachagua yale anayotaka kusikia kwenye maelezo ambayo anatoa mwingine.
Ngazi ya nne ni kusikiliza kwa makini, hapa mtu anaweka umakini wake kwenye kusikiliza kile ambacho mwingine anaeleza.
Ngazi ya sita ni kusikiliza kwa kujali, hapa siyo tu mtu anasikiliza kwa makini, bali pia anaelewa hisia ambazo zipo nyuma ya kile ambacho mtu anaeleza.
Ili kuwaelewa wengine na kuweza kueleweka, unapaswa kusikiliza kwa kujali.
Na njia ya kuweza kusikiliza kwa kujali ni kuelewa kile ambacho mtu anaeleza na hisia ambazo zipo nyuma ya kile anachoeleza.
Pale mtu anapoongea, ujumbe anaotoa umebebwa kwa asilimia 10 kwenye maneno, asilimia 30 kwenye sauti na asilimia 60 kwenye mwili.
Hivyo kama hutachukua muda wa kuelewa hisia za mtu, hutaweza kumwelewa, hutaweza kueleweka na mahusiano yenu hayatakuwa mazuri.
Sikiliza kwa kujali na utaweza kujenga maelewano mazuri na wengine.
SOMA; Mbinu Tisa (09) Za Kukuwezesha Kuwa Msikilizaji Bora Sehemu Yoyote Ile
TABIA YA SITA; USHIRIKIANO WA KIBUNIFU.
Ushirikiano ndiyo hali ya juu kabisa kwenye maisha. Ushirikiano wa kibunifu ni ule ambao umoja unakuwa na manufaa kuliko jumla ya utengano.
Kwenye hesabu 1 + 1 = 2, kwenye ushirikiano 1 + 1 = 11 au namba yoyote kubwa. Hiyo ni kwa sababu watu wawili wanaposhirikiana kibunifu, matokeo wanayozalisha yanakuwa ni makubwa kuliko kila mmoja angefanya peke yake.
Ili watu waweze kushirikiana vizuri, lazima kwanza waaminiane. Na watu wanapoaminiana na kushirikiana, nguvu kubwa inakuja kati yao na kuwawezesha kupata matokeo makubwa kuliko ambayo yangeweza kupatikana bila ushirikiano huo.
Ushirikiano haimaanishi kufanana au kukubaliana kwa kila kitu. Bali unamaanisha kufidiana, yaani udhaifu wa upande mmoja unafidiwa na uimara wa upande mwingine.
Ushirikiano wa kibunifu unaangalia jinsi kila upande unavyokuwa na mchango kwenye kuleta matokeo makubwa na mazuri.
Ili kupata mafanikio makubwa unayoyataka, jenga ushirikiano mzuri na wengine. Aminika na shirikiana na unaowaamini, jua uimara wako na udhaifu na shirikiana na wale ambao wana uimara yale maeneo ambayo wewe una udhaifu na wao wana udhaifu kwenye maeneo ambayo wewe una uimara.
Kwa kuelewana na kuthaminiana kwenye tofauti zenu, mtaweza kufanya makubwa na wote kunufaika.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA tumekuwa na mjadala mzuri kuhusu kujenga maelewano na ushirikiano na wengine ili kuweza kufanya makubwa. Karibu ujifunze kwa kufunga kipindi hapo chini.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.