Rafiki yangu mpendwa,
Safari ya mafanikio ni ngumu na iliyojaa changamoto za kila aina. Unaweza kupanga vizuri kabisa ni mafanikio gani unayotaka na hatua za kuchukua.
Na kwa msukumo mkubwa unaokuwa nao, unaanza kuchukua hatua kwenye malengo na mipango unayokuwa umejiwekea. Lakini sasa, matokeo unayokuwa unayapata yanakuwa ni tofauti kabisa na matarajio uliyokuwa nayo.

Kwa kuwa unayataka sana mafanikio, unajipa moyo na kuvuka magumu na changamoto unazokutana nazo. Lakini bado mambo yanazidi kuwa magumu. Watu wote uliokuwa unawategemea wanakuangusha. Unafika hatua ambayo inakuwa vigumu kabisa kwako kuendelea.
Ni katika hatua kama hiyo ndiyo unakata tamaa na kuona mafanikio uliyoyataka hayawezekani. Hapo unazika ndoto kubwa ulizokuwa nazo na kurudi kwenye kuwa mtu wa kawaida.
Hakuna makosa makubwa unayoweza kuyafanya kwenye maisha yako kama kukata tamaa kwenye safari ya mafanikio kwa sababu ya magumu na changamoto unazokutana nazo. Kwa sababu uwepo wa magumu na changamoto ni kiashiria kwamba hiyo ndiyo safari sahihi. Kwa sababu wengi hawataweza kuvuka magumu hayo, hivyo wewe ukiyavuka utakuwa na ushindani mchache.
Lakini pia kadiri unavyokutana na magumu na changamoto ndiyo unavyozidi kukomaa na kuweza kukabiliana na magumu ya kila aina. Unapoacha unakuwa umepoteza huo ukomavu ambao umeshaujenga, ambao ungefanya safari kuwa nyepesi zaidi mbeleni kuliko ilivyokuwa wakati unaanza.
Zaidi ni ile kauli ya Kiswahili inayosema giza linapokuwa kali, jua imekaribia kupambazuka. Mara nyingi pale unapokuwa umekata tamaa, unakuwa karibu kabisa na mafanikio kuliko kule ulikotoka. Hivyo unakuwa umepita magumu mengi na makubwa na kubakisha kipande kidogo, halafu unakata tamaa.
Rafiki, kama umewahi kufanya hilo la kukata tamaa kwenye safari yako ya mafanikio ulikosea sana. Kuanzia sasa usirudie tena. Chagua chochote unachotaka kufanikiwa na weka juhudi kubwa bila ya kukata tamaa licha ya kukutana na magumu na changamoto.
SOMA; Bila huu ung’ang’anizi huwezi kufanikiwa.
Amua kwamba utafanikiwa au utakufa ukiwa unapambana. Usikubali kitu kingine nje ya hayo mawili. Usikubali kukata tamaa na kuishi maisha yako yote kwa majuto ya kukosa kile ambacho ulikitaka hasa. Unawezaje kuwa hai huku ukiwa na majuto ya kukosa ulichotaka? Kwa kipindi chote cha uhai wako unapaswa kuwa unapambania ndoto zako kubwa.
Na kwa wale ambao hawaanzi kabisa, wale ambao wanasema haiwezekani kabla hata ya kuanza, hao ndiyo wanazika uwezo mkubwa ulio ndani yao. Kama umekuwa mtu wa aina hii, hebu acha mara moja. Kamwe usije kujiambia kitu hakiwezekani wakati hata hujajaribu. Na ukishajaribu, usikubali kuacha mpaka umepata matokeo unayoyataka.
Na kama kwa sasa unapitia magumu ambayo umekaribia kabisa kukata tamaa, pokea ujumbe huu maalumu ambao unauhitaji sana leo, endelea kujisukuma, usikate tamaa. Nenda siku moja tu, fika kesho, halafu kesho nenda tena siku moja. Ikabili safari yako siku moja baada ya nyingine. Ni mpaka uyapate mafanikio unayoyataka au ufe ukiwa unapambana.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimekushirikisha umuhimu wa kukaa kwenye mchakato wako wa mafanikio bila ya kukata tamaa. Karibu uangalie somo hilo ili utoke ukiwa na msukumo ambao hauwezi kuathiriwa na chochote.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.