Habari Matajiri Wawekezaji,

Kujenga utajiri hakuwezekani bila ya kuwa na kipato. Hivyo ongezeko la kipato ni eneo ambalo kila anayetaka kujenga utajiri mkubwa lazima alifanyie kazi. Uwekezaji wa kipato ndiyo unampa mtu nyenzo ya kuweza kukuza utajiri wake bila kuhitajika kufanya kazi moja kwa moja.

Pamoja na kipato kuwa ndiyo sehemu muhimu ya kujenga utajiri, bado watu wengi wamekuwa wanashindwa kutumia vipato vyao kujenga utajiri. Na wengi huwa wanaanza na sababu ambayo mwanzoni inaweza kuonekana ni ya kweli, kwamba kipato hakitoshelezi.

Labda kweli kipato ambacho mtu anakuwa anaanza nacho, iwe ni kwenye kazi au biashara, kinakuwa ni kidogo. Lakini kadiri muda unavyokwenda, kipato hicho kimekuwa kinaongezeka. Pamoja na kipato kuongezeka, bado watu wanashindwa kujenga utajiri.

Kila mtu anayefanya shughuli yoyote ya kuingiza kipato, kadiri muda unavyokwenda, kipato chake kinaongezeka. Lakini kwa nini wengi wao utajiri wao hauongezeki? Tena kwa walio wengi, kadiri kipato kinavyoongezeka ndiyo madeni yanakuwa makubwa zaidi?

Kuna sababu kubwa sana kwa nini ongezeko la kipato limekuwa halileti utajiri kwa walio wengi, ambayo ni wengi kuruhusu ongezeko la kipato kuja na ongezeko la matumizi.

Wengi wanapoanza na kipato cha chini, huwa wanakuwa na matumizi madogo pia. Wanahakikisha wanakuwa na matumizi yanayoendana na kipato chao. Pale kipato kinapoongezeka, moja kwa moja na matumizi yao pia yanaongezeka.

Hilo ndiyo limekuwa linapelekea kipato kutokutosheleza kwa watu wote, licha ya kuwa na vipato tofauti. Kwa mfano kwenye eneo la ajira, wafanyakazi kwenye eneo moja wanakuwa na vipato vinavyotofautiana kwa ukubwa sana, lakini bado wote wanakuwa kipato hakiwatoshelezi.

Kwenye maisha, fedha huwa haikosi matumizi, pale fedha inapokuwepo, matumizi hutokea mpaka iishe. Kuna matumizi mengi ambayo tukiwa hatuna fedha wala hayatusumbui, lakini tukiwa na fedha yanaonekana ni muhimu.

SOMA; Anza Na Huu Uwekezaji Kama Hujui Chochote Kuhusu Uwekezaji.

Kwenye programu yetu ya NGUVU YA BUKU tunakwenda kuvunja huu mtego wa kushindwa kujenga utajiri licha ya kupata ongezeko la kipato. Hii ni hatua muhimu kwa sababu tunakwenda kuweka juhudi kubwa kwenye kuongeza kipato chetu, hivyo kama hatutaondoa huo mtego wa ongezeko la kipato kumezwa na matumizi, tutaendelea kubaki pale tulipo.

Ili kuhakikisha ongezeko la kipato tunalopata linachangia kwenye kujenga utajiri, tunapaswa kufanyia kazi mambo yafuatayo;

1. Kuwa na bajeti ya matumizi ya msingi tu.

Ukisubiri mpaka uwe na fedha ndiyo upange matumizi, fedha yote itaisha na matumizi hayataisha. Kuondokana na hilo unapaswa kupanga bajeti ya matumizi yako mapema na yawe yale ya msingi tu. Ukishaweka bajeti hiyo, fanya matumizi hayo tu na siyo nje ya hapo.

2. Ongezeko lote la kipato liende kwenye akiba na uwekezaji.

Ongezeko la kipato unaloingiza unapaswa kulipeleka kwenye akiba na uwekezaji moja kwa moja. Usijishawishi kwa namna yoyote ile kutumia ongezeko la kipato kwenye matumizi, badala yake peleka kwenye akiba na kuwekeza kama ulivyo mpango wako.

3. Kama kuna matumizi ya ziada ya lazima kufanya, wekeza kiasi hicho pia.

Unaweza kuona huu mpango unakubana usiwe na maisha huru kwako. Kwamba kama kuna matumizi ya ziada ambayo ni ya lazima kwako kufanya, kwa nini ujizuie kufanyafanya? Lengo letu ni kuhakikisha hatujidanganyi wenyewe na kupeleka ongezeko lote la kipato kwenye matumizi. Hivyo kama una matumizi ya ziada ambayo ni lazima uyafanye, hakikisha unawekeza kwanza kiasi kama hicho. Kwa mfano umeona unahitaji kupata toleo jipya la simu unayopenda, ambayo bei yake ni laki 5, basi tafuta milioni moja ya ziada, laki 5 unaiwekeza kwanza halafu laki 5 unaitumia kwenye hayo matumizi. Ukitumia matumizi kukusukuma kuwekeza zaidi, utaweza kujenga utajiri kwa ongezeko la kipato unalopata.

4. Fedha yoyote ambayo hukuwa na mpango nayo, usiitumie.

Watu huwa tunashangaza sana, unaweza kupata fedha ambayo hukuwa na matarajio nayo kabisa, labda mtu kakupa zawadi au vyanzo vingine. Ghafla unajikuta tayari una matumizi ambayo umeshajishawishi ni ya lazima kabisa. Wakati hukuwa hata unajua kama utapata fedha hiyo. Jizuie kuja na matumizi kwenye fedha ambazo hukuwa unazitegemea. Badala yake unapopata fedha za aina hiyo, moja kwa moja wekeza. Ikiwa umepewa zawadi, umeokota au kutoka vyanzo vingine, wekeza fedha hizo na endelea na maisha yako kama vile hakuna kilichotokea. Hivyo pia kwa wale wanaopata fedha nyingi kwa wakati mmoja, iwe ni mafao, mirathi, fidia au kushinda bahati nasibu, watanufaika iwapo watawekeza hizo fedha na kutulia kwa muda kuliko kukimbilia kufanya matumizi.

5. Kuwa makini na vipato vya msimu.

Kwa watu ambao wanafanya shughuli ambazo zina vipato vya misimu huwa wana aina ya maisha yanayoshangaza sana. Wakati msimu ni mzuri na kipato ni cha uhakika, wanakuwa na matumizi makubwa sana. Wakati msimu ni mbaya na kipato hakuna, wanaishia kuuza vitu walivyonunua kwa bei ya kutupa ili waweze kukidhi mahitaji yao. Hii ipo hata kwa wafanyakazi wanaolipwa mwisho wa mwezi, siku za malipo mambo yanakuwa mazuri na matumizi makubwa, lakini katikati ya mwezi mambo yanakuwa magumu. Usibadili matumizi yako kutokana na mabadiliko ya msimu, badala yake kuwa na matumizi ya msingi ambayo unayafanya nyakati zote. Pale msimu unapokuwa mzuri, kipato cha ziada chote wekeza. Kuwa na fedha ni kuzuri kuliko kufanya matumizi ambayo baadaye yanakuwa mzigo au unalazimika kuuza kwa hasara.

Kama hutaweza kujidhibiti kwenye matumizi, hasa pale kipato kinapokuwa kinaongezeka, utabaki kuimba wimbo wa kipato hakitoshelezi miaka yako yote na kubaki kwenye umasikini. Kipato hakijawahi kutosheleza matumizi yote, ni wewe upange yapi matumizi ya msingi kwako utakayohangaika nayo na mengine kuyapuuza.

MJADALA WA SOMO.

Karibu kwenye mjadala wa somo ushirikishe yale uliyojifunza kwa kujibu maswali yafuatayo;

1. Kwa nini ongezeko la kipato limekuwa haliwapi watu utajiri?

2. Unawezaje kutumia matumizi ya ziada unayotaka kuyafanya kukusukuma kuwekeza zaidi?

3. Kwa kipato cha msimu au unachoingiza kwa wingi mara moja, mambo gani ya kuzingatia ili kisimezwe na matumizi?

4. Karibu uulize swali lolote kuhusu somo hili au programu nzima ya NGUVU YA BUKU.

Tuma majibu ya maswali hayo kama kiashiria cha kusoma na kuelewa somo hili na kwenda kuchukua hatua ili kujenga utajiri kwa uhakika.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.