Rafiki yangu mpendwa,

Kwenye maisha huwa hatupati kile tunachostahili, bali tunapata kile tunachopambania kwenye majadiliano. Watu wengi wamekuwa wanashindwa kufanikiwa kwa sababu hawajui njia bora za kushinda majadiliano mbalimbali wanayoshiriki.

Kila siku unahusika kwenye majadiliano mbalimbali ambayo yanagusa maslahi yako moja kwa moja. Kama unafanya biashara, wakati wa kuuza na kununua kunakuwa na majadiliano ya bei. Kama umeajiriwa, kuna majadiliano ya mshahara, majukumu ya kazi na vitu vingine.

xr:d:DAF_0orONc8:210,j:2930015493117856540,t:24040517

Wanaofanikiwa kwenye maisha ni wale ambao wanajua njia bora ya kushinda majadiliano wanayohusika. Na njia pekee ya kushinda majadiliano ni kujifunza mbinu za ushindi na kuwa na maandalizi sahihi kabla ya majadiliano husika.

Leo tunakwenda kujifunza njia muhimu ya kushinda majadiliano wakati wa bei. Njia hiyo ni kunyamaza baada ya kutaja bei.

Pale kunapokuwa na majadiliano yanayohusu bei, watu huwa wanabishana kwa muda mrefu, na upande unaoshinda ni ule ambao una mbinu nzuri za ushindi pamoja na maandalizi.

Mbinu ya kunyamaza baada ya kutaja bei huwa ina nguvu sana kwenye majadiliano. Baada ya bei kutajwa, upande wa kwanza kuongea ndiyo huwa unaishia kushindwa kwa kulazimika kukubaliana na upande wa pili.

Kama wewe ndiye unayeuza na umempa mteja bei, unapaswa kunyamaza baada ya kumpa bei. Kama itamchukua mteja muda kukujibu, mpe muda, usikimbilie kuanza kuielezea bei hiyo au kumwambia kuna punguzo. Kadiri inavyomchukua mteja muda mrefu kujibu pale unapompa bei, ndivyo anavyoshawishika kukubaliana nayo. Pale mteja anapokuwa anachukua muda mrefu kujibu na wewe ukaanza kuongea, unakuwa umemwondoa kwenye mtego ambao alikuwa ameshanasa.

Kama wewe unanunua na umepewa bei kisha kutaja bei unayoweza kulipa, kaa kimya. Usianze kutoa maelezo mengi kuhusu bei hiyo, acha upande wa pili ufikirie na kukujibu. Pale upande uliopewa bei unapokaa kwa muda mrefu na bei hiyo, ndivyo unavyoshawishika kukubali.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; How To Negotiate Better Deals (Mwongozo Wa Majadiliano Ya Kukuwezesha Kupata Mipango Bora).

Ili uweze kutumia njia hii kwenye majadiliano ni lazima uwe na subira, usiwe na haraka ya kutaka makubaliano yafikiwe kwa haraka. Kwa sababu yule mwenye haraka ndiye atakayeishia kukubaliana na upande mwingine.

Lakini pia ni lazima uweze kujizuia kwenye mazoea yako ya kujaza ombwe linaloachwa wazi na ukimya ambao unajitokeza baada ya kutaja bei. Watu wengi huwa hawawezi kuvumilia pale kunapokuwa na ukimya na hivyo kuongea ili maongezi yaendelee. Wewe jizuie kwenye hilo na vumia hali ya ukimya inayojitokeza, hapo ni mbinu inakuwa inafanya kazi, hivyo usiingilie.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimefafanua kwa kina jinsi ya kutumia njia hii ya majadiliano kuweza kuwa na ushawishi mkubwa kwa wengine wakubaliane na wewe na upate kile unachotaka. Karibu ujifunze kwenye kipindi hapo chini.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.