3385; Upande wa pili.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Kauli ya Kiswahili ya ukipenda boga penda na ua lake ina maana kubwa sana.
Kila kitu kina pande mbili, wa kwanza ambao ndiyo tunautaka na wa pili ambao mara nyingi hatuutaki.
Ili kupata upande ambao tunautaka, lazima tukubali na ule upande ambao hatuutaki.
Wengi sana wameshindwa kwenye maisha kwa sababu wanayataka mafanikio makubwa bila ya kulipa gharama yake.
Wanapoona mafanikio ya wengine kwa nje, wanatamani na wao kufikia kama hayo.
Ambacho hawatamani ni gharama ambazo mtu ameingia mpaka kufika hapo.
Hawapo tayari kuumia na kutoa kafara ambazo wengine walitoa.
Kuna ambao wanakuwa hawajui kuna gharama wanapaswa kulipa. Hivyo wao kujiendea tu na wanapohitajika kulipa gharama wanakuwa hawajajiandaa.
Na kuna ambao wanajua kuna gharama, ila wanajiona wao ni wajanja sana kwa hiyo wanaweza kupata mafanikio bila kulipa gharama hizo.
Gharama za kulipa ili kufanikiwa ni nyingi, lakini kubwa zaidi ni kazi, kafara, kukataliwa, kudhulumiwa, kujifunza, fedha.
Ukubwa wa gharama za kulipa huwa unategemea ukubwa wa mafanikio ambayo mtu unataka kuyajenga.
Mara zote ukweli umekuwa unabaki kwamba hakuna mafanikio kama hakuna gharama ambazo zimelipwa.
Kadiri mtu anavyoelewa hilo mapema na kulifanyia kazi, ndivyo anavyojenga mafanikio yake kwa uhakika.
Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, kulipa gharama ili kupata mafanikio ni kitu tunachokielewa na kukifanyia kazi mara zote.
Tunaanza kwa kujua gharama tunazopaswa kulipa ili kuyapata mafanikio tunayoyataka na kisha kulipa gharama hizo bila ya kuchelewa.
Tunajua utayari wa kulipa gharama hizo una mchango kwenye mafanikio tunayoyapata.
Ni mwenendo huu ndiyo unaotupa uhakika wa kuyapata mafanikio makubwa.
Kwa kila mafanikio unayoyataka, anza kwa kujua gharama zote unazopaswa kulipa ili kuyapata mafanikio hayo, kisha zilipe kwa haraka bila ya kusubiri chochote.
Jua huwezi kuyapata mafanikio kwa haraka kama unachelewa kulipa gharama. Hivyo kadiri unavyoyataka mafanikio kwa haraka, lipa gharama kwa haraka pia.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe