Rafiki yangu mpendwa,

Huwa kuna kauli inayosema kimtokacho mtu ndiyo kimemjaa. Kauli hiyo ni ukweli mtupu kwa sababu kinachotoka kinategemea sana kile kinachoingia.

Inapokuja kwenye akili zetu, yale tunayofikiri na kusema, yanategemea sana ni nini tunazilisha akili hizo. Kwa bahati mbaya sana, wengi hawajui hata kama akili zinalishwa, hivyo hujikuta wakiruhusu kila kitu kuingia kwenye akili zao na kuwavuruga.

xr:d:DAGBqkNIeLQ:7,j:5235858609596092491,t:24040618

Rafiki, kama unavyolisha mwili wako, ndivyo pia akili yako inavyokwenda. Ukiulisha mwili wako vyakula ambavyo siyo vya afya, unapata utapiamlo. Unakuwa na uzito uliopitiliza ambao unakuletea magonjwa sugu kama kisukari na shinikizo la damu.

Kadhalika ukilisha akili yako vyakula ambavyo siyo vya afya, unapata utapiamlo wa akili. Utapiamlo wa akili ni kuwa na mtazamo hasi, kushindwa kufikiri kwa usahihi na kutokuwa na malengo na mipango ya maisha yako.

Chakula kisichokuwa cha afya kwa akili yako ni taarifa zote hasi na zisizokuwa na mchango wowote kwako. Habari mbalimbali na mambo yanayoendelea kwenye maisha ya wengine ndiyo sehemu kubwa ya taarifa hizo.

SOMA; Tano Za Juma Kutoka Kwenye Kitabu Cha Tabia Za Ubongo Wenye Furaha (Jinsi Ya Kupata Furaha Ya Kudumu Kwenye Maisha)

Taarifa yoyote ambayo ni hasi, haina mchango kwenye malengo yako, huna cha kufanya kuiathiri na inachukua muda wako, ni chakula kibaya kwa akili yako. Hizo ni taarifa ambazo unapaswa kuziepuka kama ukoma ili uweze kujenga maisha ya mafanikio makubwa.

Ili kurekebisha akili yako ambayo umeshailisha chakula kisichokuwa sahihi kwa muda mrefu, kuna dayati unayopaswa kuifanya. Dayati hiyo inakwenda kurekebisha akili yako ili uweze kuitumia vizuri kujenga mafanikio unayoyataka.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimekueleza kuhusu dayati hiyo na jinsi unavyopaswa kuifanya ili iweze kuwa na manufaa kwako. Umeshajikwamisha sana kufanikiwa kwa sababu ya mambo ambayo umeruhusu yaingie kwenye akili yako kiholela. Sasa ni wakati wa kuleta uwajibikaji mpya kwa kuzuia yote yasiyo sahihi yasiingie na kukukwamisha. Angalia kipindi hicho hapo chini na utoke na zoezi la dayati ya kufanya ili uboreshe akili yako na uweze kufanya makubwa kwenye maisha yako.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.