Rafiki yangu mpendwa,

Maisha yana changamoto nyingi sana. Changamoto hizo zinamkabili kila mtu, bila ya kujali yupo kwenye ngazi gani. Watu wengi wamekuwa wanaruhusu changamoto wanazokutana nazo kuyavuruga maisha yao na hivyo kukosa utulivu. Hilo ni jambo ambalo hupaswi kuliruhusu kabisa kwenye maisha yako.

Wengi hudhani wakiweza kutatua changamoto zinazowakabili sasa, basi watakuwa wamemaliza kabisa changamoto na kuweza kuyafurahia maisha yao yote yaliyobaki. Wanakuja kushangazwa pale wanapotatua changamoto walizonazo, zinakuja changamoto nyingine kubwa zaidi.

Kuwa na maisha ya mafanikio na ambayo unayafurahia, haimaanishi kutokuwa na changamoto. Badala yake ni kuweza kuzikabili changamoto katika hali ya utulivu mkubwa.

Unashindwa kuzikabili changamoto za maisha kwa utulivu kwa sababu umekosa misingi sahihi. Hakuna mahali umewahi kufundishwa jinsi ya kuzipokea na kwenda na changamoto ambazo ni sehemu ya maisha yako.

Kwa bahati nzuri sana, falsafa ya Ustoa imeweza kuweka misingi hiyo, ambayo mtu yeyote akiifuata anaweza kuwa na maisha tulivu hata kama anakabiliana na changamoto kubwa na ngumu kiasi gani.

Kwenye kitabu cha Meditations, ambayo yalikuwa ni maandiko ya fikra za aliyekuwa mtawala wa Roma na mwanafalsafa wa Ustoa, Marcus Aurelisu, ameweza kushirikisha misingi sahihi ya kufuata katika kuyakabili maisha kwa utulivu.

Ipo misingi mingi ambayo Marcus ameshirikisha, hapa nakwenda kukushirikisha baadhi ambayo ukianza kuifanyia kazi, hakuna kitakachokuyumbisha kwenye maisha.

Maisha Ni Mieleka.

Marcus anatuambia maisha ni mieleka, ambapo kila wakati unapambana na mshindani anayetaka kukuangusha chini. Wajibu wako ni mara zote kusimama imara kwa kutumia miguu yako miwili ili usiangushwe.

Usitegemee kwamba maisha yatakuwa rahisi, badala yake jiandae na maisha magumu na hakuna kitakachokuyumbisha. Wengi wanaoanguka ni wale waliotegemea mambo yawe rahisi, wakati uhalisia haupo hivyo.

Hakuna Kinachoweza Kukuumiza Bila Ruhusa Yako.

Kila ambacho wanafanya wengine, hakipo ndani ya uwezo wako, lakini jinsi unavyopokea na kujibu kile wanachofanya wengine, ipo ndani ya uwezo wako. Huwezi kuumizwa au kukwazwa na kitu chochote kile kama wewe mwenyewe hujaruhusu kitu hicho kikuumize au kukukwaza.

Usiweke uzito usiostahili kwenye mambo unayokutana nayo kwenye maisha. Jua hakuna chochote chenye nguvu kwako kama wewe mwenyewe hutakiruhusu. Na hivyo usitoe nguvu kwa kitu chochote kukusumbua.

Ishi Kila Siku Yako Kama Ya Mwisho.

Hebu fikiria, kama unajua leo ndiyo siku yako ya mwisho hapa duniani, ni kitu gani kinachoweza kukuvuruga? Hakuna, kwa sababu unajua huna muda hapa duniani, hivyo utayapuuza yote yasiyo muhimu.

Unajua kuna siku ambayo itakuwa ya mwisho kwako hapa duniani, japo hujui ni ipi. Sasa kwa nini usiishi kila siku yako kama ya mwisho ili upuuze mambo madogo madogo yasivuruge utulivu wako?

SOMA; Tumia Falsafa Ya Ustoa Kukabiliana Na Mateso Ya Maisha.

Tenda Wema Kwa Sababu Ya Wema.

Ng’ombe wanatoa maziwa, lakini huwasikii wakijisifia au wakikutaka uwashukuru kwa maziwa ambayo unakunywa.

Kuku wanataga mayai, lakini unapokula mayai huendi kwa kuku na kuwashukuru.

Nyuki wanazalisha asali, pamoja na utamu wa asali, hujawahi kuwasifia na kuwashukuru nyuki kwa kazi kubwa wanayoifanya.

Lakini wewe, unapofanya wema kidogo tu, unataka dunia nzima ikusifie na kukushukuru. Na pale unapokosa hizo sifa na shukrani, unakwazika na kukosa utulivu.

Wajibu wako ni kutenda wema, hayo mengine achana nayo. Ukiweza hilo, utakuwa na utulivu mara zote.

Simamia Misingi Sahihi.

Watu wengi kwenye maisha huwa wanaiga yale ambayo yanafanywa na wengine na kudhani ndiyo sahihi. Matokeo yake huwa wanaishia kupata matokeo ambayo siyo sahihi na kuvurugwa.

Kuepuka hilo, simamia misingi sahihi na siyo kufuata mkumbo. Jambo sahihi kwako kufanya ni lile ambalo lipo kwenye misingi sahihi. Kitu hakiwi sahihi kwa sababu kinafanywa na watu wengi. Badala yake kinakuwa sahihi kama kipo kwenye misingi sahihi.

Kwa kuelewa na kuishi hii misingi uliyojifunza hapa, utaepuka mengi ambayo yamekuwa yanavuruga maisha yako.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA tumekuwa na mjadala mpana zaidi kuhusu misingi ya Ustoa ya kutuwezesha kuwa na maisha tulivu. Karibu ujifunze kupitia kipindi hicho hapo chini.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.