3386; Baada ya wiki.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Mambo mengi ambayo tunajichosha na kujisumbua nayo kwenye maisha yetu, ni mambo ya kupita.
Yaani tunahangaika sana na mambo ambayo hata siyo ya kudumu.
Kwa njia hiyo tunapoteza muda na umakini wetu kwa mambo yasiyokuwa na tija kabisa.
Kuvuka hilo unapaswa kutumia kigezo cha wiki moja.
Kwa kila jambo ambalo linakuumiza, jiulize nini kitatokea baada ya wiki moja?
Yaani kama hutafanya lolote kabisa, baada ya wiki moja nini matokeo?
Na kama utachukua hatua na ukawa umekosea, nini matokeo baada ya wiki moja?
Kama baada ya wiki moja bado jambo hilo litakuwa linasumbua, iwe umechukua hatua au hujachukua, basi unapaswa kulipa umakini zaidi.
Lakini kama baada ya wiki moja jambo hilo utakuwa umelisahau kabisa, iwe umefanya au hukufanya kitu, basi hupaswi kuruhusu jambo hilo likusumbue hata sasa.
Unapaswa kulipotezea na kupeleka umakini wako kwenye yale ambayo ni muhimu zaidi.
Mambo mengi unayohangaika nayo kwenye maisha unapaswa kuyapotezea kabisa.
Hayana hadhi ya wewe kupoteza muda na nguvu zako katika kutahangaikia.
Ni sawa na mbio za panya, ambazo hata ukishinda, bado unabaki kuwa panya.
Kwa kila jambo pima ushindi na kushindwa vinakuwa na madhara gani kwako na kwa safari yako nzima.
Vitu ambavyo havina madhara makubwa, hupaswi pia kuvipa umakini mkubwa.
Hiyo ni kwa sababu kuna mambo mengi yanataka umakini wako, lakini mengi hayastahili kabisa.
Kama umeenda kwenye dimbwi kwa ajili ya kukausha maji, ni rahisi kupotelea kwenye kupambana na mamba uliowakuta pale.
Wakati hata ukishinda au kushindwa kwenye kupambana na mamba, bado maji yatakuwepo.
Lakini ukibaki kwenye lengo lako la kukausha maji, mamba hawatapata mahali pa kukusumbua.
Kumbe mambo mengine, na ambayo ni mengi, huwa yanatusumbua kwa sababu tunayapa nafasi sisi wenyewe.
Kama tukiyanyima nafasi, kwa kutingwa na yale ambayo ni muhimu zaidi kwetu tunayanyima nafasi ya kutusumbua.
Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, tunapeleka umakini wetu kwenye mambo makubwa na yenye madhara kwenye mafanikio makubwa tunayoyapambania.
Kila tunalokutana nalo tunalipima kwa madhara yake kwenye mafanikio tunayoyataka.
Kama lina madhara, yawe mazuri au mabaya, tunalipa umakini.
Kama halina madhara, haijalishi linaonekana ni muhimu kiasi gani, hatusumbuki nalo.
Kwa njia hiyo tunaacha kusumbuka na mengi yasiyokuwa na tija na kupeleka umakini wetu kwenye machache yenye tija kubwa.
Hatupotezi nguvu zetu kwa mambo ya mpito, mambo ambayo baada ya muda mfupi hayatakuwa na maana tena.
Tunakazana kujenga mafanikio ya kudumu na hivyo tunahangaika na yale yenye madhara ya kudumu pia.
Usiwasikilize watu pale wanapokuambia jambo ni muhimu au dharura, hicho ni kipimo unachopaswa kukipima wewe kulingana na malengo uliyonayo.
Kama kitu kina madhara kwenye malengo yako basi ni muhimu, kama hakina siyo muhimu, hata kama watu wengi kiasi gani wanasema ni muhimu.
Muda, umakini, nguvu na fedha ni rasilimali muhimu sana kwako ambazo zinawindwa na watu wengi.
Usipoweza kuzilinda vizuri, utaishia kuhangaika na mambo mengi na bado hutaweza kupiga hatua kubwa.
Peleka rasilimali hizo kwa mambo yenye madhara na siyo vinginevyo.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe