Habari Njema Kwako Tajiri Mwekezaji,
Kila kitu kwenye maisha huwa kina gharama. Kinachotofautiana ni wakati gani gharama hiyo inalipwa.
Maisha huwa yanatupa nafasi ya kulipa gharama sasa au kulipa baadaye, lakini kamwe hayatuachi bila ya kulipa gharama. Kwa kuchagua kulipa gharama sasa, mambo yako yanakuwa rahisi baadaye. Na kwa kuchagua mambo yako kuwa rahisi sasa, unakuja kulipa gharama baadaye.
Changamoto ya kuja kulipa gharama baadaye ni kwamba unailipa pamoja na riba kubwa. Kama ambavyo ukikopa fedha unazilipa kwa riba, ndivyo pia unavyochelewa kulipa gharama za maisha unavyokuja kulipa kwa gharama.
Kufanya uwekezaji ni gharama, ambayo utachagua kuilipa sasa kwa kuwekeza au kuja kuilipa baadaye kwa kutokuwekeza. Kwa bahati mbaya sana, watu wengi bila ya kujua wamekuwa wanachagua kuja kulipa gharama hiyo baadaye na wanaishia kuilipa kwa riba kubwa.
Wewe kama Tajiri Mwekezaji wa programu ya NGUVU YA BUKU, unapaswa kujikumbusha mara kwa mara gharama za kutokufanya uwekezaji sasa ili uweze kukaa kwenye mpango wako wa uwekezaji bila kuyumba.

GHARAMA YA KUWEKEZA SASA.
Kwa kuwa tumechagua kuwekeza sasa, lazima tujue ni gharama gani tunayoingia ili tuwe tayari kuilipa bila ya wasiwasi wowote.
Gharama ya wewe kuwekeza sasa ni kuhitajika kujinyima baadhi ya vitu ambavyo unaweza kuwa unatamani kuwa navyo. Wakati wengine wakitumia vipato vyao kujifurahisha kwa kutimiza matamanio yao, wewe utalazimika kutokufanya hivyo ili uweze kufanya uwekezaji kwa ukubwa.
Hii ni gharama ambayo unailipa na usipokuwa imara kwenye kuilipa utakwama haraka sana. Kwani watu watakuita wewe ni bahili na usiyejua jinsi ya kuishi maisha mazuri. Watakuona una roho mbaya na usiyejali, kwa sababu watakapotaka fedha zako, hawataweza kuzipata.
Kwa kujibana kwako kwenye matumizi ili uwekeze, utaambiwa unaishi maisha ambayo siyo ya hadhi yako. Yaani watu wanakuwa wamekupangia kabisa unapaswa uyaishije maisha yako. Ni lazima uwe tayari kutokueleweka, kudharauliwa na hata kudhihakiwa kama unataka kuwekeza kwa msimamo.
Pia baadhi ya watu watakaojua kwamba unafanya uwekezaji, watakuwa wa kwanza kukukatisha tamaa. Wakikuambia utapoteza fedha zako au utakufa hujayafurahia maisha yako.
Wajibu wako ni kujua hizo ni gharama ambazo unapaswa uzilipe ili uweze kufanya uwekezaji sasa na kujenga utajiri wako wa baadaye.
GHARAMA YA KUCHELEWA KUANZA KUWEKEZA.
Wakati mzuri kwako kuanza uwekezaji ulikuwa miaka 10 iliyopita, lakini wakati mwingine mzuri ni sasa. Huenda unajiambia bado una muda, labda kwa sababu ya umri au kipato na hivyo kuchelewa kuanza kufanya uwekezaji.
Kuna gharama kubwa sana ambayo utailipa kwa kuchelewa kuwekeza kuliko ambayo utalipa kwa kuanza uwekezaji sasa. Gharama utakayolipa kwa kuchelewa kuanza uwekezaji ni ule ukuaji ambao ungekuwa unaupata tangu unapoanza kuwekeza.
Kwa kila muda ambao unakwenda hujafanya uwekezaji, ni faida unapoteza, tena faida ya bure kabisa ambayo haikulazimu wewe kufanya kazi. Ni kupoteza fursa ya uwekezaji wako kuendelea kukua kadiri muda unavyokwenda.
Hivyo usijicheleweshe kuanza uwekezaji, anza hata kama kipato ni kidogo au unaona una muda mwingi mbele yako.
Pia kwa wale ambao umri umekwenda na unaona umeshachelewa, hakuna kuchelewa kama utaanza mara moja. Kwa kutokuanza ndiyo unazidi kujichelewesha, hivyo anza mara moja na utaokoa hiyo gharama ya kukosa ukuaji wa thamani.
GHARAMA YA KUTOKUWEKEZA KWA MSIMAMO.
Unaweza kufanya uwekezaji mara moja na usifanye tena, au ukawa unafanya mara chache bila ya msimamo mzuri. Japo unakuwa umewekeza, lakini kuna gharama kubwa ambayo unakuwa unaingia kwa kufanya hivyo.
Unaposhindwa kuwekeza kwa msimamo, unalipa gharama ya kukosa mwendelezo kwenye ukuaji wa uwekezaji wako. Kwa sababu thamani ya uwekezaji inakua kidogo kidogo kwa muda, ni uwekezaji endelevu na kwa msimamo ndiyo unaoleta manufaa makubwa.
Lakini pia kwa kuwekeza kwa matukio badala ya kwa mwendelezo unajikuta unafanya uwekezaji kwa hasara. Kama unawekeza kila unaposikia uwekezaji unapanda thamani, maana yake unakuwa unanunua uwekezaji kwa bei ya juu. Unapokuwa unafanya uwekezaji kwa msimamo, kuna nyakati utanunua kwa bei ya chini na nyakati nyingine kwa bei ya juu. Hivyo kwa wastani unajikuta umefanya uwekezaji kwa bei ambayo siyo kubwa na hivyo kuwa na uwanja mpana wa ukuaji na kuweza kunufaika.
Kuliko kuwekeza mara moja na kuacha ni bora kuwekeza kidogo kidogo kwa msimamo bila kuacha. Msimamo kwenye uwekezaji una manufaa ya kuendeleza kukuza thamani ya utajiri wako kadiri muda unavyokwenda, kwa kile unachowekeza na thamani inayozalishwa.
SOMA; Msingi mkuu usiovunjika kwenye fedha, biashara na uwekezaji.
GHARAMA YA KUWEKEZA NA KUTOA.
Kuna ambao wanafanya uwekezaji, lakini wanautoa uwekezaji huo na kupeleka kwenye matumizi mbalimbali. Hili lina gharama kubwa ambayo mtu anaingia bila ya kujua.
Gharama ya kwanza ni kukosa ukuaji ambao ungeendelea kutokana na muda ambao uwekezaji umekaa. Tunajua faida ya uwekezaji inatokana na muda ambao uwekezaji huo umezalisha bila ya kuingiliwa.
Gharama ya pili ni makato yanayofanyika wakati wa kuuza uwekezaji. Kuwekeza huwa hakuna makato yoyote, lakini kutoa uwekezaji huo huwa kuna gharama. Hivyo kuwekeza na kutoa kunapelekea gharama zaidi ambazo zinampa mtu hasara.
Gharama ya tatu ni kununua wakati bei iko juu na kuuza wakati bei iko chini na hivyo kuwa umepoteza fedha kabisa. Mara nyingi watu husukumwa kuwekeza wakati bei ya uwekezaji inapanda na kushawishika kuuza wakati bei inashuka. Matokeo yake ni kununua uwekezaji kwa bei kubwa na kuuza kwa bei ndogo, kitu ambacho ni hasara ya moja kwa moja.
GHARAMA YA KUTOKUWEKEZA KABISA.
Gharama kubwa kabisa kwenye maisha ni kutokufanya uwekezaji kabisa. Kwani hii humweka mtu kwenye maisha ya mateso makubwa kwa baadaye, pale nguvu zake za kufanya kazi zinapokuwa zimepungua lakini mahitaji ni makubwa.
Gharama ya kwanza ya kutokuwekeza kabisa ni kukosa ukuaji ambao ungepatikana kama mtu angewekeza kwa kipindi chote cha maisha yake. Anakuwa ametumia kipato chake chote na hivyo anakuwa hana chochote cha kuonyesha.
Gharama ya pili ni kulazimika kufanya kazi hata katika umri wa uzee na nguvu zimepungua kwa sababu hakuna kipato cha kuweza kuendesha maisha.
Gharama ya tatu ni kunyanyasika na wale unaokuwa unawategemea kwa ajili ya kuendesha maisha pale nguvu zako zinapokuwa zimepungua na huwezi tena kufanya kazi. Unakuwa kama mtoto mdogo ambaye huwezi kuamua mambo yako mwenyewe.
Gharama ya nne ni makasiriko kwa wengine, hasa pale unapowategemea na wanashindwa kutimiza mahitaji unayokuwa nayo. Hapa unajikuta unagombana na watu wako wa karibu pale wanaposhindwa kukupa yale unayotaka kuwa nayo.
Gharama ya tano ni kifo cha mapema, pale unapostaafu kazi yako au huwezi tena kufanya shughuli zako na kipato cha kuendesha maisha ni cha kusua sua, hali ya maisha huwa mbaya, afya kudhoofu na kifo kutokea haraka.
Kama unazitaka hizo gharama, acha usiwekeze sasa, wewe jiendee na maisha yako kwa urahisi unaoutaka sasa. Muhimu ni wakati wa kulipa gharama utakapofika usiwalaumu watu, ilipe kama utakavyokuwa unaikwepa sasa.
TUMECHAGUA KULIPA GHARAMA SASA.
Tuko hapa kwenye programu ya NGUVU YA BUKU kwa sababu tumechagua kulipa gharama sasa na tumechagua kuilipa kwa ukubwa kabisa. Kwa miaka 10 ijayo na kuendelea, tumechagua kulipa gharama kubwa ya kuwekeza, ili baadaye tuyafurahie matunda ya hii gharama tunayolipa sasa.
Hatuna hofu na gharama za baadaye, kwa sababu tayari tunazijua na tumechagua kuziepuka kwa kuwekeza sasa na kuwekeza kwa msimamo bila kutoa uwekezaji huo.
Tukae kwenye hii safari kwa uaminifu, kutoka nje ni kujiweka kwenye wakati mgumu sana kwa baadaye.
MJADALA WA SOMO.
Karibu kwenye mjadala wa somo hili kwa kujibu maswali hayo hapo chini.
1. Ni gharama gani ambazo umeshaingia kwa kuchelewa kuanza kuwekeza au kuwekeza na kutoa?
2. Ni gharama zipi ambazo umeanza kuzilipa sasa baada ya kuwekeza kwa msimamo kwenye programu ya NGUVU YA BUKU?
3. Ni gharama zipi za baadaye ambazo unazikwepa sana na unapozifikiria unachagua kukaa kwenye huu mchakato bila kutoka?
4. Karibu uulize swali kuhusu somo hili au programu hii ya NGUVU YA BUKU.
Tuma majibu ya maswali hayo ya mjadala wa somo kama ushahidi wa kusoma, kuelewa na kwenda kutekeleza somo hili.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.