Habari njema wauzaji bora kuwahi kutokea.
Kufikia wateja wengi na kwa msimamo ni hitaji muhimu kwenye biashara ili kuweza kufanya mauzo makubwa zaidi.
Zipo njia nyingi za kuwafikia wateja, kama ana kwa ana, simu, jumbe na mitandao ya kijamii.
Barua pepe ni moja ya njia za kuwafikia wateja, njia ambayo ikifanyiwa kazi vizuri matokeo yake yanakuwa mazuri.
Karibu kwenye somo hili ujifunze kuwafikia wateja wengi kwa kutumia barua pepe.

NJIA KUU YA MAWASILIANO BAINA YA BIASHARA.
Siyo biashara zote zinaweza kutumia barua pepe kwenye kuwafikia wateja. Lakini kwa biashara ambazo zinalenga biashara nyingine, yaani biashara ambayo inauzia biashara, matumizi ya barua pepe ni muhimu.
Barua pepe ndiyo njia kuu ya mawasiliano baina ya biashara. Hiyo ni kwa sababu ya urahisi wake wa kutumia na utunzaji wa kumbukumbu kwa muda mrefu. Tofauti na njia nyingine za mawasiliano ambapo upande mmoja unaweza kufuta mawasiliano kwa pande zote, kwa barua pepe hilo haliwezekani.
Mawasiliano kwa njia ya barua pepe yanaweza kubaki kwa muda mrefu na yakawa kama ushahidi wa mawasiliano yaliyofanyika.
Lakini pia uwezo wa kuwaunganisha watu wengi kwenye mawasiliano ya barua pepe ni kitu kinachofanya iwe njia inayopendwa kwa mawasiliano ya biashara. Kulingana na hitaji la mawasiliano, watu wanaweza kuongezwa kwenye hatua mbalimbali za mawasiliano hayo.
Mawasiliano ya barua pepe pia yanaweza kutumika kwenye biashara zinazolenga watumiaji wa mwisho, hasa pale biashara inapohusisha maarifa na taarifa. Kwani wale wanaosoma barua pepe huwa na utulivu na umakini mkubwa na hivyo kuwa wateja wazuri.
Kama wateja unaowalenga huwa wanatumia barua pepe kwenye mawasiliano yao, tumia njia hiyo pia katika kuwafikia na utaweza kuwa na ushawishi mkubwa kwao.
TOFAUTI YA BARUA PEPE NA MITANDAO YA KIJAMII.
Uwepo wa mitandao ya kijamii na urahisi wake wa kuwafikia wateja umefanya wengi waone mawasiliano ya barua pepe hayana umuhimu mkubwa. Wanaona mitandao ya kijamii inaweza kumaliza kila kitu.
Lakini ukweli ni mawasiliano kwa barua pepe ni bora kuliko mawasiliano kwa mitandao ya kijamii kwa sababu zifuatazo;
Moja ni utulivu wa mawasiliano, watu wengi kwenye mitandao ya kijamii hawana utulivu. Wanakutana na kelele nyingi kitu ambacho kinawafanya wasiwe na umakini mkubwa. Lakini kwenye barua pepe, watu wanakuwa na umakini mkubwa zaidi.
Mbili ni umiliki wa mawasiliano, kwenye mitandao ya kijamii unakuwa huna umiliki mkubwa wa mawasiliano unayofanya, mitandao hiyo inaweza kukufungia na ukashindwa kuwafikia wateja. lakini kwenye barua pepe, unaweza kumiliki mawasiliano hivyo huwezi kufungiwa na kushindwa kuwafikia wateja. Kutumia mitandao ya kijamii ni sawa na kukodi wakati kutumia barua pepe ni sawa na kumiliki.
Tatu ni kujitofautisha na kutumia mawasiliano kujitangaza, kwenye mitandao ya kijamii siyo rahisi kujitofautisha, kwa sababu unatumia jina la mtandao husika. Lakini kwenye barua pepe, unatumia jina la biashara yako hivyo mawasiliano yanakuwa ya kujitofautisha na yenyewe tu yanakuwa sehemu ya kujitangaza. Barua pepe inakuwa imebeba jina la biashara ndani yake. Kwa mfano kama jina la biashara ni SISI na jina lako ni JOHN, barua pepe yako inaweza kuwa john@sisi.com Hayo yanakuwa ni mawasiliano, lakini pia yanaonyesha jina la biashara.
Hivyo pamoja na matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii na kuzoeleka huko, usijisahau na kuacha kutumia barua pepe. Unakuwa na umiliki mkubwa wa mawasiliano kwa barua pepe kuliko kwenye mitandao ya kijamii.
SOMA; Kufikia Wateja Wengi Kwa Kutumia Matangazo Ya Mitandao Ya Kijamii.
BARUA PEPE KWA MTU MMOJA MMOJA.
Mawasiliano ya barua pepe kwa mtu mmoja mmoja ni pale unapotuma ujumbe kwa mtu mmoja peke yake. Hii ni njia ya mawasiliano kama zilivyo njia nyingine. Lakini pia ni njia rahisi kuwasiliana na wengi kwa haraka kwa sababu ya wepesi wake kutuma.
Mawasiliano kwa mtu mmoja mmoja yanaleta mjadala ambao unamlenga mtu moja kwa moja na hivyo kuwa na ushawishi zaidi. Hapa mawasiliano yanakuwa yanawagusa wahusika moja kwa moja kitu kinachoongeza ushawishi.
Katika kuwafikia wateja, kuwa na mpango wa kuwasiliana na mtu mmoja mmoja kwa barua pepe ili kuwa na majadiliano yanayowalenga na kuweza kuwashawishi.
BARUA PEPE KWA WENGI KWA PAMOJA.
Mawasiliano ya barua pepe kwenda kwa wengi kwa pamoja ni kutuma barua pepe moja kwa watu wengi. Unaweza kufanya hili kwa kuweka barua pepe za wengi kwenye ujumbe mmoja unaotuma. Hapa unaandika ujumbe ambao unatuma, kisha kuweka barua pepe nyingi na unapotuma ujumbe unaenda kwa wote.
Njia nyingine ya kutuma barua pepe moja kwa watu wengi ni kutumia mifumo maalumu ya kuwezesha hilo (email campaigns). Kwa mifumo hiyo, barua pepe moja inaweza kutumwa kwa watu wengi na bado kila anayepokea akaona kama ametumiwa yeye peke yake. Kwa hii mifumo, licha ya barua pepe kuwa moja, inaweza kutaja jina la kila anayeipokea na hivyo kumfanya aone kama ujumbe umetumwa kwake tu. Lakini pia kwa mifumo hii, unaweza kufikia maelfu ya wateja kwa mara moja, kulingana na gharama unayoweza kulipa.
Moja ya mifumo inayowezesha kutuma barua pepe moja kwa watu wengi ni MAILCHIMP (www.mailchimp.com), ambapo kwa gharama mbalimbali unapata idadi tofauti za kufikia wateja kwa ujumbe mmoja. Mifumo hiyo ina mambo mengine mengi ya kuongeza ushawishi kwa wateja wanaofikiwa kwa mawasiliano ya barua pepe.
Kila biashara ambayo inalenga wateja wanaotumia barua pepe, inapaswa kuwa na hiyo mifumo ya kutuma barua pepe kwa wengi na mara kwa mara kuitumia kuwafikia wateja kwa njia ambayo inakuwa na ushawishi mkubwa kwao.
BARUA PEPE ZA BARIDI (COLD EMAIL).
Barua pepe za baridi (cold email) ni njia ya kuwafikia wateja ambao hawakujui kwa kutumia barua pepe. Kwa sababu mawasiliano ya barua pepe ni rahisi kuyapata kuliko mawasiliano mengine, pale unapokuwa unatafuta njia ya kuwafikia wateja lakini hupati, unapaswa kutafuta barua pepe zao na kisha kuwatumia ujumbe.
Kwa sababu hawakujui, barua pepe yako inaweza isipewe uzito. Lakini kama utatuma vizuri, kwa kutoa thamani kubwa kwenye barua pepe unazotuma na kuzituma mara kwa mara, unaweza kuwashawishi wale wanaopokea na kuanza kuwasiliana na wewe.
Hapa kilicho muhimu ni kutoa thamani kwenye barua pepe hizo za baridi, kwa kuwafanya watu wajifunze na kupata taarifa muhimu. Kuwashawishi wachukue hatua kwa kukujibu na hapo unakuwa umefungua mawasiliano na wao.
Ukiingia kwenye tovuti za biashara, matangazo ya biashara pamoja na kadi za biashara, mawasiliano ya barua pepe yanapatikana kwa urahisi. Pia kwa kutumia anwani ya mtandaoni ya biashara, ni rahisi kubuni barua pepe inavyoweza kuwa. Na hapo unaweza kutuma barua pepe kwa wale unaokuwa unawalenga hata kama hawakujui kabisa.
Kwa biashara zinazolenga wateja wanaotumia barua pepe, kila wakati tafuta mawasiliano ya barua pepe ya wateja walengwa ambao bado hawajaijua biashara na kuwatumia taarifa mbalimbali kwa barua pepe. Wape thamani kubwa kwa njia hiyo ya barua pepe na utaweza kuwapata kama wateja tarajiwa na hatimaye kuwakamilisha kwa kuwauzia.
MAMBO YA KUZINGATIA KWENYE BARUA PEPE.
Ili kuwa na ufanisi mzuri kwenye kuwafikia wateja wengi kwa barua pepe, zingatia mambo yafuatayo;
1. Kwa biashara inayolenga biashara nyingine, biashara inayohusisha maarifa na taarifa au biashara ambayo wateja wanatumia barua pepe, hakikisha unawasiliana na wateja wako kwa njia ya barua pepe, ina nguvu na ushawishi mkubwa.
2. Tengeneza kanzi data (database) ya taarifa za wateja wako ambayo inahusisha barua pepe zao na kuitumia kwenye kuwasiliana nao mara kwa mara na kwa ukubwa.
3. Kila siku tuma barua pepe za baridi (cold email) kwa wateja unaowalenga wawe wateja wako, tumia njia hiyo kuwafanya wakujue na kushawishika kujibu barua pepe zako kitu ambacho kitafungua mawasiliano nao.
4. Epuka kuonekana msumbufu kwa barua pepe unazotuma, ili usifungiwe na wale unaowatumia jumbe kwa barua pepe. Kama unatuma jumbe nyingi na ambazo hazina thamani kwao, ni rahisi kukufungia ili usiweze kuwafikia. Wewe wasiliana na watu kwa njia ya barua pepe kwa kuwapa thamani kubwa ili wafurahie kupokea mawasiliano yako.
5. Tumia mfumo wa kutuma barua pepe kwa watu wengi kwa pamoja na pangilia vizuri mawasiliano yako na wateja unaowalenga na hata ambao ni tarajiwa ili uwaweke kwenye mchakato mzuri ambao unakuwa na ushawishi mzuri kwao kukufuatilia na hata kununua.
Pamoja na maendeleo makubwa kwenye eneo la mawasiliano, barua pepe bado imebaki kuwa njia ya msingi ya mawasiliano kwenye biashara. Tumia njia hii vizuri ili uweze kuwafikia wateja wengi na kuwashawishi kufanya nao biashara.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.