Rafiki yangu mpendwa,
Akili zetu huwa zina nguvu kubwa sana, ambayo sisi wenyewe huwa hatuwezi hata kuielezea. Kwanza hatujui ukubwa wa uwezo huo ni kiasi gani. Na pili tunatumia sehemu ndogo sana ya uwezo huo mkubwa.
Chukua mfano nimekuambia magari ya rangi nyekundu ni mengi. Ghafla unaanza kuona magari ya rangi nyekundu kila unakopita. Unaweza kudhani kwamba ni kweli magari hayo ni mengi au yameongezeka. Lakini ukweli ni kwamba magari hayo yamekuwepo muda wote, ila akili yako haikuwa na umakini kwenye hilo. Ni pale ulipoanza kufikiria magari mekundu, ndiyo akili inayapa umakini na hivyo kuyaona zaidi.

Rafiki, akili yako imekuwa inakuonyesha vile vitu unavyotaka kuona na kuhakikisha huoni vile ambavyo hutaki kuviona. Kwa sababu taarifa ambazo akili inapokea ni nyingi sana na huwezi kuchakata zote kwa wakati mmoja, inazochuja na kukuletea zile ambazo unazitaka tu.
Hilo la akili kuchuja na kukupa kile unachotaka ni zuri na muhimu, lakini lina madhara makubwa, hasa kwa upande wa mafanikio. Pale unapokuwa na mtazamo ambao siyo mzuri kwa mafanikio, unakuwa kikwazo kwako kupata mafanikio makubwa. Ndiyo maana watu wawili wanaofanana kwenye mambo yote, wanakuwa na mafanikio tofauti, kwa sababu hawaioni dunia kwa namna moja, bali kila mmoja anaiona dunia kivyake.
Moja ya eneo ambalo limewakwamisha wengi kufanikiwa ni kutokuwapenda watu waliowazidi mafanikio. Wivu ni asili yetu binadamu, pale tunapoona mtu mwingine amefanikiwa kuliko sisi, hali ya wivu huwa inatuingia. Kama wivu utakuwa mzuri, kwamba na sisi tunataka kuwa kama wao, inatusaidia kufanikiwa. Lakini kama wivu utakuwa mbaya, kwamba kwa nini wao wamefanikiwa kuliko sisi, inatuzuia kufanikiwa.
Ili kuhakikisha unakaa upande mzuri wa wivu na kufanikiwa, jijengee tabia ya kuwapigia makofi wale ambao wamefanikiwa kuliko wewe. Unapokutana na mtu yeyote ambaye amekuzidi mafanikio, mpigie makofi. Kumpigia makofi maana yake ni kumpenda na kumkubali, kitu ambacho kitaifungua akili yako nayo ipate mafanikio kama yake.
Kwa kuwapenda na kuwakubali watu waliofanikiwa kuliko wewe, unakuwa tayari kujifunza kutoka kwao na kuweza kuchukua hatua sahihi na wewe kufanikiwa. Kwa kuwa akili yako inakuwa inatafuta mafanikio, fursa nzuri za kufanikiwa zitajitokeza. Hivyo ndivyo na wewe unavyoweza kufanikiwa kwa kuyafurahia mafanikio ya wengine.
Lakini kama utachukia mafanikio ya wengine, kwa kuwasemea maneno mabaya, kwamba hawakustahili mafanikio hayo, hutajifunza kwao na hutafanikiwa. Kwa kuwachukia wale waliofanikiwa, akili yako inajifunza na kukuepusha na fursa zote za mafanikio ili usijichukie na wewe pia. Kwa kuwachukia waliofanikiwa unakuwa umejizuia na wewe kufanikiwa, kitu kinachokukwamisha sana.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeeleza kwa kina dhana hii ya kuwapigia makofi wale waliokuzidi mafanikio ili uweze kujenga mafanikio kama yao. Karibu ujifunze hapo chini.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.