Rafiki yangu mpendwa,

Najua umewahi kukutana na mtu anayeuza karanga, au kitu kingine cha kula. Hukuwa na mpango wa kununua kabisa, lakini akakuambia kuonja ni bure. Nini kilitokea baada ya kuonja? Ulinunua, hata kama hukuwa na mpango wa kununua kitu hicho.

Lakini pia umewahi kwenda eneo ambalo ni mgeni kabisa, hakuna mtu unayemjua, halafu ukakutana na mtu anayezungumza lugha kama yako au amevaa nguo ya timu unayoshabikia. Hapo ulipata amani na kuona kuna mtu mnafanana.

Rafiki, hayo ambayo yamekuwa yanakutokea, siyo kwa bahati, bali ni kwa misingi ya kisaikolojia ambayo inatusukuma sisi binadamu kufanya maamuzi tunayoyafanya.

xr:d:DAGB2ZTEoeo:7,j:453036011382115962,t:24040818

Mwandishi Robert Cialdini kwenye kitabu chake cha INFLUENCE ametushirikisha nyenzo saba za ushawishi ambazo tukiweza kuzitumia tutaweza kuwa na ushawishi mkubwa kwa wengine.

Hapa tunakwenda kujifunza nyenzo ya kwanza ya FADHILA na nyenzo ya pili ya KUPENDA, ili tuelewe zinavyofanya kazi, jinsi ya kuzitumia kuwa na ushawishi na jinsi ya kuepuka zisitumike vibaya kwetu.

Nyenzo ya kwanza ni KULIPA FADHILA.

Sisi binadamu huwa tunasukumwa kuwatendea wema wale ambao wametutendea wema, kuwalipa wale ambao wamefanya kitu kwa ajili yetu. Huu ni msukumo wa ndani yetu kabisa ambao unatufanya tusiwe na utulivu kama hatujaweza kuwalipa wengine fadhila kwa yale ambayo wametufanyia. Hali hii ya kulipa fadhila ni muhimu kwenye jamii, kwani imekuwa inadumisha ushirikiano baina ya watu.

Ili kuweza kuwashawishi watu wengine wakubaliane na wewe, wajengee hali ya kuwa na deni la kusukumwa kukulipa wewe fadhila. Unaweza kufanya hivyo kwa kuwapa watu zawadi mbalimbali ambazo zitawafanya wajione wana deni kwako. Kwa kutanguliza kuwapa watu zawadi, hata kama ni ndogo, baadaye unapokuwa na kitu unachowaomba au kuwataka wafanye, watafanya kama sehemu ya kukulipa fadhila. Tumia njia hii yenye nguvu kuweza kuwashawishi watu wakupe unachotaka, kwa wewe kuanza kuwapa wanachotaka.

Kuepuka watu wasitumie njia hii ya fadhila kukulaghai, kwa sababu watu wanaotaka kupata vitu fulani kutoka kwako wanaitumia njia hii, kuwa makini na zawadi unazopewa. Epuka kujiweka kwenye hali au nafasi ambazo watu wanakupa zawadi kama mtego wa kuja kupata vitu vingi zaidi kwako. Kwa kuwa siyo rahisi kukataa zawadi unapopewa, ni muhimu uhakikishe unaondoa nafasi za watu kuweza kukupa zawadi kirahisi, hasa wale ambao hujuani nao.

SOMA; Jinsi Ya Kuwabadili Watu Unaowaongoza Bila Ya Kuchukiwa Nao.

Nyenzo ya pili ni KUPENDA.

Binadamu huwa tunashawishika na watu au vitu ambavyo tunavipenda na kuvithamini. Pale unaposhawishiwa kitu na mtu ambaye unamjua, kumpenda au kumkubali, unaona ndiyo kitu sahihi unachopaswa kufanya. Ile hali ya kujuana inaleta hali ya kuaminiana, ambayo inafanya ushawishi uwepo. Na hali ya kupenda huwa inajengwa kwa mwonekano, kufanana, kusifia, ukaribu na mahusiano.

Kuweza kuwashawishi watu, jenga hali ya wao kukupenda na kukukubali. Unafanya hivyo kwa kuwa na mwonekano mzuri, kuwaonyesha unafanana nao, kuwasifia na kujenga nao ukaribu. Yajenge hayo kwa uhakika na watu watakuamini na kushawishika na wewe.

Kuepuka kushawishika vibaya na nyenzo hii ya kupenda, chukua tahadhari pale unapojikuta umemkubali mtu kwa haraka kuliko kawaida. Kama kuna mtu ulikuwa hujuani naye kabisa, lakini ndani ya muda mfupi unajikuta umempenda na kumkubali sana, tafakari kwanza, huenda ametumia mbinu ya kupenda kuaminika kwa haraka na kujinufaisha kupitia wewe.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA tumekuwa na mjadala mzuri sana kuhusu nyenzo hizi mbili na washiriki wameweza kutoa mifano mingi na mizuri kwenye nyenzo hizi. Karibu usikilize kipindi hapo chini ili uendelee kujifunza.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.