Rafiki yangu mpendwa,
Unapokuwa eneo geni, ambalo huna uhakika wa kitu gani sahihi cha kufanya, huwa unafanyaje? Unaangalia wengine wanafanya nini na kisha kufanya hicho, kwa sababu tunaamini kinachofanywa na wengi ndiyo sahihi.
Vipi je ukikutana na mtu amevalia sare ya polisi na akakupa maelekezo ya kufuata, je utaanza kumhoji kama kweli ni polisi? Kwa sehemu kubwa unaamini ile sare na kuona ni polisi kweli. Lakini tumekuwa tunasikia taarifa za watu wasio polisi wanaovaa sare za polisi na kujinufaisha kupitia wengine.
Rafiki, mambo hayo mawili tuliyoanza nayo somo hili, yamekuwa hayatokei tu, bali yamejengeka ndani yetu na tumekuwa tunayatumia kufanya maamuzi. Kuangalia wengine wanafanya nini na sisi tukafanya, ambayo ni kufuata MKUMBO na kutii wenye MAMLAKA ni nyenzo za ushawishi zenye nguvu kwa watu.

Mwandishi Robert Cialdini kwenye kitabu chake cha INFLUENCE ametushirikisha nyenzo saba za ushawishi ambazo tukiweza kuzitumia tutaweza kuwa na ushawishi mkubwa kwa wengine.
Kwenye masomo ya nyuma tumejifunza nyenzo mbili za kwanza; FADHILA na KUPENDA. Hapa tunakwenda kujifunza nyenzo ya tatu ya MKUMBO na nyenzo ya nne ya MAMLAKA, ili tuelewe zinavyofanya kazi, jinsi ya kuzitumia kuwa na ushawishi na jinsi ya kuepuka zisitumike vibaya kwetu.
Nyenzo ya tatu ni KUFUATA MKUMBO.
Sisi binadamu huwa tunapima usahihi wa kitu kwa kuangalia wingi wa watu wanaokifanya. Kile kinachofanywa na watu wengi tunaamini ndiyo sahihi zaidi. Hii ni njia ya mkato ambayo imekuwa inatumiwa na wengi kwenye kufanya maamuzi.
Ni asilimia 5 tu ya watu ndiyo huwa wanafanya maamuzi yao kwa kufikiri wao wenyewe, hawa ndiyo viongozi. Asilimia 95 iliyobaki huwa wanafanya maamuzi yao kwa kufuata mkumbo, hawa ni wafuasi ambao wanaangalia kinachofanywa na wengine na wao kukifanya.
Nyenzo hii ya kufuata mkumbo huwa inapata ya ushawishi katika nyakati tatu;
1. Pale mtu anapokuwa hana uhakika wa nini cha kufanya, anaangalia wengine wanafanya nini.
2. Pale kitu kinapofanywa na watu wengi zaidi kinaonekana ndiyo sahihi.
3. Pale kitu kinapofanywa na watu wanaofanana na sisi, huwa tunaona ndiyo tunapaswa kufanya pia. Hapa tunaongozwa na mazoea; ‘Watu kama sisi wanafanya vitu kama hivi.’
Kile kinachofanywa na wengi huwa kina nguvu ya ushawishi kwa sababu;
1. Kinaonekana ndiyo sahihi.
2. Kinaonekana kuwezekana.
3. Kinaleta kukubalika na wengine.
Kutumia nyenzo ya MKUMBO kuwa na ushawishi mkubwa, waonyeshe watu kile unachowataka wakubaliane nacho ndiyo kinakubalika na wengi zaidi. Hapa kuwa mkweli badala ya kulaghai, kama kitu hakikubaliki sasa, onyesha kama kuna fursa ya kukubalika zaidi baadaye.
Kuepuka kulaghaiwa na nyenzo hii, mara zote hoji ukweli wa umaarufu unaosemwa kuhusu kitu. Mara nyingi taarifa zinazokuwa zinatolewa siyo za kweli. Fanya maamuzi kwa taarifa sahihi ili yawe bora kwako.
SOMA; Jifunze Kuwa Na Ushawishi Mkubwa Kutoka Kitabu HOW TO WIN FRIENDS AND INFLUENCE PEOPLE.
Nyenzo ya nne ni KUTII MAMLAKA.
Malezi tuliyopata kwenye kila ngazi ya maisha yetu yametujenga kuwatii wale wenye mamlaka. Na hilo lina manufaa kwa sababu wenye mamlaka wanakuwa na taarifa nyingi kuliko sisi. Kwa mfano unapoenda kwa daktari, utalazimika kufanya yale anayokuelekeza kwa sababu anajua zaidi kuhusu afya kuliko wewe.
Hivyo kutii mamlaka ni moja ya njia za mkato kwetu kufanya maamuzi bila ya kulazimika kujua vitu vingi. Lakini kama tunavyojua, penye fursa ya aina hii, watu hutafuta jinsi ya kujinufaisha.
Watu wanaotaka kuwa na ushawishi huwa wanaigiza mamlaka, kwa kuonyesha wana mamlaka ya aina fulani ili wasikilizwe na kuweza kujinufaisha. Njia za kuigiza mamlaka ambazo watu wamekuwa wanatumia ni;
1. Vyeo; watu wamekuwa wanajipachika vyeo ambavyo vinawafanya watu wawaamini.
2. Mavazi; kwa mamlaka ambazo zina sare ya aina fulani, watu hutumia sare hizo kuaminika.
3. Mwonekano; watu hutengeneza mwonekano, hasa ambao ni wa gharama ili kukubalika zaidi.
Ili kujenga mamlaka sahihi ambayo yatakufanya uwe na ushawishi mkubwa kwa wengine, fanya mambo haya mawili;
1. Jenga ubobezi kwenye kile unachofanya. Kadiri unavyojua zaidi kile unachofanya, ndivyo unavyokuwa na mamlaka zaidi na kuwa na ushawishi.
2. Jijengee kuaminika kwa kuwa mkweli mara zote. Kamwe usidanganye au kuongeza chumvi, na pale kunapokuwa na udhaifu, useme wazi. Watu wanapoona unaaminika, wanakuwa tayari kufuata yale unayowaambia.
Kutumia nyenzo ya mamlaka kuwa na ushawishi ni kujenga UBOBEZI na KUAMINIKA. Hayo yatawafanya watu wakuamini na kushawishika na wewe.
Kuzuia wengine wasitumie nyenzo ya mamlaka kujinufaisha na wewe, kwa kuigiza mamlaka, hoji UBOBEZI na KUAMINIKA kwao. Hoji kama kweli mtu ana ubobezi kwenye eneo husika na kama taarifa anazotoa ni za kweli. Pale kunapokuwa hakuna ukweli, usikubaliane nao.
Rafiki, kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA tumekuwa na mjadala mzuri kuhusu nyenzo hizi mbili na kupata mifano mbalimbali ya jinsi zilivyo na nguvu. Karibu ujifunze zaidi kwenye kipindi hicho hapo chini.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.