
Kiasili sisi binadamu ni viumbe wa mahusiano kadiri ya vinasaba yaani DNA. Alisema Mwl. Deogratius Kessy, katika kitabu cha “Mauzo Ni Mahusiano”. Hata pale tunapokuwa tunahitaji kitu fulani huwa tunaanza kuulizia kwa watu wetu kwa karibu kwanza. Huwa tunawaamini sana watu tunaohusiana nao. Pale wanapotupendekezea kitu, huwa tunaondoa hofu kabisa na kuchukua hatua mara moja.
Kuna nguvu kubwa sana ya mahusiano katika mchakato mzima wa mauzo. Watu ambao umejenga nao mtandao, wale ambao unawajua au wanakujua ndiyo watakuwa wa kwanza katika mchakato wa mauzo.
Mahusiano uliyonayo na mteja ndiyo yanayowashawishi watu kuja kununua kwako. Namna bora kujenga mahusiano ni kuzingatia yafuatayo ili kuwa na ufanisi mkubwa katika ufuatiliaji;
Moja; Salamu
Salamu ndiyo mlango wa mahusiano yoyote yale. Ukitaka kitu chochote kile katika jamii yetu tunayoishi basi salamu ndiyo kitu cha kwanza. Hata kama una hela yako mfukoni, salamu ndiyo ustaarabu wa kwanza kwenye mauzo na mahusiano kwa ujumla.
Kama husalimii watu, watu wanakuweka kando.
Mbili; Neno la shukurani
Kwa chochote kile ambacho mteja amenunua au hata kama hajanunua kitendo tu cha kufika kwenye huduma yako unapaswa kumshukuru mteja. Kushukuru ni kuomba tena, hivyo kuwa mtu wa kushukuru pale mtu anapokuwa anakufanyia kitu. Kusema asante ndiyo mshahara wa mteja au malipo kwa kile ambacho amekufanyia. Yaani mtu anakuletea fedha lakini wewe unamlipa kwa kumwambia neno dogo tu asante. Hapo ni rahisi kujenga mahusiano mazuri na wateja, hata ufuatiliaji unakuwa rahisi
Tatu; Uwepo wako eneo la biashara Kama mteja umemwambia nitakupigia saa tano akakubali mpigie muda huo. Kama ni kuwa dukani asubuhi, fungua muda huo. Wateja wanahitaji kuwa karibu na watu wanaopatikana muda wote. Hata ufuatiliaji unayofanya unakuwa na nguvu, maana mteja akihitaji huduma ni rahisi kumhudumia.
Nne; Uaminifu.
Mark Twain aliwahi kusema, “Mara zote sema ukweli, hutoweza kukumbuka chochote”. Kama bidhaa sio nzuri, usimpatie mteja kisa unataka pesa yake. Maana kwenye ufuatiliaji utapata shida. Wateja hawataweza kukupa ushirikiano.
Tano; Kutimiza ahadi
Katika kitabu cha “Wake Up and Sell” Mary Anne na wenzake wanaelezea namna gani wateja wanavyowaamini. Wanasema,”Wateja wanatuamini kwa sababu hatuogopi kusema ukweli, na kamwe hatutoi ahadi za uongo, na tunawaambia wateja ukweli kama bidhaa haiwafai”. Hii iko tofauti kwetu, tunajali pesa.
Hivyo, marafiki wananunua kwa marafiki zao. Ili liweke akilini. Ni wewe kuendelea kuwa na mahusiano mazuri na watu maana, watu wananunua kwa watu wanaowapenda na wanaohusiana nao. Ukifanya hayo hata suala zima la ufuatiliaji halitakupa shida.
Hitimisho; Kama una changamoto ya mauzo, kitu cha kwanza jiulize unahusiana na nani? Una mahusiano mazuri na wateja wako? Waswahili wanasema, “ongea na watu uvae na viatu”. Hii ina maana kwamba kuwa na mahusiano mazuri na watu nao wao watakuwa tayari kununua kwako na kukupa wateja wengi zaidi.
Imeandaliwa na Lackius Robert Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo na Mwandishi. Tuwasiliane 0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz.
Mauzo Ni Mahusiano.