Rafiki yangu mpendwa,

Pata picha unapita nje ya duka la nguo na kuona tangazo la nguo nzuri likisema punguzo kwa asilimia 50, leo tu. Unavutiwa na kuingia kuangalia nguo hiyo, unaambiwa imebaki moja tu. Wakati unajishauri kama utaichukua au la, anakuja mwingine naye anataka kuiangalia. Ni hali gani inatokea hapo? Utajikuta unasukumwa kuchukua nguo hiyo haraka kwa sababu hutaki kuikosa. Lakini kumbuka hukuwa na ratiba ya kununua nguo kabisa, lakini sasa unagombania nguo.

Umewahi kubishana na mtu juu ya jambo lolote na ukajua kabisa kwamba wewe ndiye umekosea, lakini bado ukaendelea kubishana. Licha ya kujua kwamba wewe ndiyo haupo sahihi, hukuwa tayari kukiri hilo, badala yake ulitafuta njia nyingine za kuonyesha uko sahihi.

Mifano hiyo miwili, ambayo imekuwa inatokea kwenye maisha yetu ya kila siku, huwa siyo bahati mbaya, bali ndivyo binadamu tulivyo. Maamuzi mengi unayoyafanya kwenye hali za aina hiyo, huwa yanasukumwa na hali fulani za kisaikolojia tunazokuwa nazo. Kwenye mfano wa kwanza, unajikuta unakitaka sana kitu kwa sababu ya UHABA wake, unasukumwa kuchukua hatua ili usikipoteze. Na kwenye mfano wa pili, unaendelea na ubishi ili tu kuwa na MSIMAMO, licha ya kujua kabisa kwamba umekosea.

Rafiki, hizo ni hali za kisaikolojia ambazo tumekuwa tunazitumia kufanya maamuzi yetu mbalimbali. Mara nyingi huwa zinakuwa na msaada, lakini wakati mwingine huwa zinaishia kutugharimu, kama tunavyokwenda kujifunza hapa.

Mwandishi Robert Cialdini kwenye kitabu chake cha INFLUENCE ametushirikisha nyenzo saba za ushawishi ambazo tukiweza kuzitumia tutaweza kuwa na ushawishi mkubwa kwa wengine.

Kwenye masomo ya nyuma tumejifunza nyenzo nne ambazo ni ; FADHILA, KUPENDA, MKUMBO na MAMLAKA. Hapa tunakwenda kujifunza nyenzo ya tano ya UHABA na nyenzo ya sita ya MSIMAMO, ili tuelewe zinavyofanya kazi, jinsi ya kuzitumia kuwa na ushawishi na jinsi ya kuepuka zisitumike vibaya kwetu.

Nyenzo ya tano ni UHABA.

Watu huwa wanaepuka kupoteza vitu kuliko kuvipata. Hiyo ni kwa sababu kupoteza kunauma kuliko kupata. Yaani kupoteza kiasi fulani cha fedha kunauma kuliko kupata kiasi hicho hicho. Ndiyo maana kunapoonekana hatari ya kitu kupotea au kukosekana, watu husukumwa zaidi kuchukua hatua.

Uhaba huwa unatengenezwa kwa njia mbili. Moja ni ukomo wa namba au idadi, hapa kunakuwa na kiasi fulani cha vitu ambacho kiisha basi mtu hawezi kupata tena. Mbili ni ukomo wa muda, ambapo kitu kinapatikana ndani ya muda fulani tu, muda huo ukipita kitu hakipatikani tena.

Nyenzo ya uhaba huwa ina nguvu kubwa kwa sababu inagusa hisia moja kwa moja. Na mara nyingi pale hisia zinapoguswa, kufikiri kunakwama. Hisia zinapokuwa juu, kufikiri huwa kunakuwa chini. Mtu anapoona anapoteza kitu, cha kwanza ni kuhakikisha hapotezi. Hivyo hata ukitumika uwezo wa kufikiri kiasi gani, hauwezi kupenda kwenye hizo hisia.

Kutumia nyenzo ya uhaba kuongeza ushawishi, waonyeshe watu uhaba uliopo kwenye kile ambacho unawataka wakubaliane na wewe. Muhimu ni uhaba uwe wa kweli, kwani unaweza kudanganya na watu wakachukua hatua, ila wakishajua uhaba wako siyo wa kweli, watakuwa wanakupuuza.

Kuepuka kulaghaiwa na nyenzo ya uhaba ni kusubiri usifanye maamuzi pale unapokuwa na hisia kali juu ya kitu. Hata kama unaona unakipoteza, jipe muda kwanza ili uweze kufikiri vizuri. Lakini pia unapaswa kujihoji ni nini kinakusukuma upate hicho chenye uhaba, je ni kweli una matumizi nacho au hutaki tu kukipoteza? Ukijihoji na kuwa mkweli utaona jinsi ambavyo vitu vingi havihitaji kabisa kuhangaikia.

SOMA; Achana Na Hali Hii Ya Uhaba Unayotengenezewa Na Dunia.

Nyenzo ya sita ni MSIMAMO.

Binadamu huwa tunasimamia maamuzi ambayo tumeyafanya ili kuaminika na watu wengine. Watu wenye msimamo huwa wanachukuliwa wenye akili na wanaojitambua. Watu wasiokuwa na msimamo huwa wanachukuliwa wasio na akili na wasiojitambua.

Msimamo wa watu huwa mkali zaidi pale maamuzi wanayoyafanya yanakuwa hadharani, yaani yanajulikana na wengine. Hapo watu hupata msukumo wa kuyasimamia ili waaminike na watu wengine.

Msimamo ni njia ya mkato kwa watu kuepuka kufikiri na kufanya maamuzi kila mara. Hivyo mtu akishachagua kitu, anaenda nacho hicho kwa muda mrefu. Hali hii ina manufaa kwa mambo madogo madogo yasiyohitaji umakini mkubwa. Lakini ni ya hatari sana kwenye mambo makubwa yanayohitaji umakini mkubwa.

Kutumia nyenzo ya msimamo kuwa na ushawishi zaidi, washawishi watu wafanye maamuzi ya wazi na kuanza kuchukua hatua fulani, hata kama ni ndogo kabisa. Baada ya hapo wao wenyewe wataendelea kufanya ili kuwa na msimamo. Uzuri wa nyenzo ya msimamo ni kitu kinachojichochea chenyewe, kwa sehemu kubwa msimamo ni msukumo wa ndani ya mtu mwenyewe. Na pale mtu anapokumbushwa kwa nje, basi msimamo unakuwa mkali zaidi.

Kuepuka kulaghaiwa na nyenzo hii ya msimamo angalia dalili za aina mbili kwenye maamuzi yote unayofanya. Moja ni dalili za tumbo, hapa tumbo huwa linakukata au kukuuma pale unapokuwa umefanya maamuzi ambayo siyo sahihi. Kwa kujua hivyo hupaswi kuendelea na msimamo kwa sababu tu umeshaamua, jipe nafasi ya kubadilisha. Mbili ni dalili za rohoni, hapa ndani yako kunakuwa na sauti inayokuambia nini ni sahihi na nini siyo sahihi. Kwa kuisikiliza sauti hiyo utaweza kuepuka kuendelea na makosa kwa msimamo kwa sababu tu ulishayafanya huko nyuma.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA tumekuwa na mjadala mzuri juu ya nyenzo hizi mbili. Tumepata mifano na shuhuda mbalimbali za matumizi ya nyenzo hizo kwa manufaa na kuepuka kulaghaiwa nazo. Karibu uendelee kujifunza zaidi kutoka kwenye kitabu.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.