Habari matajiri wawekezaji,

Karibuni kwenye mwendelezo wa masomo ya uwekezaji ambayo tunayapata kwenye programu yetu ya NGUVU YA BUKU. Programu hii ni ya kujifunza na kufanya kwa vitendo uwekezaji kwa hatua ndogo ndogo, kwa muda mrefu na kwa msimamo bila kuacha.

Bilionea Mwekezaji Warren Buffett, mmoja wa wawekezaji bora kabisa wa zama hizi, alikuwa anaongea na wanafunzi wa chuo kikuu cha Columbia kuhusu uwekezaji. Mmoja wa wanafunzi hao alinyoosha mkono na kumuuliza Warren swali, afanye nini ili kujiandaa kuwa mwekezaji bora.

Warren alifikiria kwa muda mfupi, kisha akachukua karatasi za ripoti za uwekezaji alizokuwa amebeba na kumwambia; “Soma kurasa 500 kama hizi kila siku. Hivyo ndivyo ujuzi unavyofanya kazi. Unajijenga kama riba mkusanyiko. Wote mnaweza kufanya hivyo, lakini nawahakikishia wengi wenu hamtafanya.”

Kuna ukweli mwingi ambao Warren ameueleza kwenye jibu hilo fupi.

Ukweli wa kwanza ni kuhusu uwekezaji muhimu sana ambao kila mtu anapaswa kuufanya kwenye maisha yake. Na uwekezaji huo ni mtu kuwekeza ndani yake mwenyewe. Kuwekeza ndani yako mwenyewe ni kujifunza na kubobea kwenye kile unachofanya.

Kuwekeza ndani yako mwenyewe ndiyo uwekezaji ambao huwezi kuupoteza kamwe. Unaweza kupoteza uwekezaji mwingine wote unaofanya, fedha zikapotea, uchumi ukayumba, majengo yakaungua, ardhi ikataifishwa au hata ukafungwa. Lakini ujuzi ambao umeujenga kwa kuwekeza ndani yako, hakuna yeyote anayeweza kukunyang’anya. Huo ni uwekezaji utakaodumu nao mpaka siku unaingia kaburini. Tutaangalia zaidi kuhusu kuwekeza ndani yetu wenyewe kwenye somo hili.

Ukweli wa pili ambao Warren ameeleza ni uwezo wa kila mtu kuwekeza ndani yake mwenyewe. Hakuna kipindi ambacho kumekuwa na demokrasia kubwa ya maarifa na taarifa kama sasa. Miaka ya nyuma, kabla ya mapinduzi ya teknolojia kukua, upatikanaji wa maarifa ulikuwa mgumu sana. Maarifa mazuri yalikuwa siri ya wachache ambao waliweza kujinufaisha nayo huku wengine wakibaki bila fursa. Lakini kwa zama hizi, kuwa tu na simu yako ya mkononi, unaweza kupata maarifa yoyote unayoyataka. Ni zama bora sana tunazoishi ambapo mtu anaweza kujifunza chochote anachotaka bure kabisa au kwa gharama ndogo sana.

Ukweli wa tatu ambao Warren ameeleza kwenye jibu lake fupi ni uhakika ambao alikuwa nao kwamba pamoja na urahisi wa kuwekeza ndani yetu, bado wengi hawatafanya hivyo. Na hilo ndiyo tunaloliona kwa walio wengi, hawajifunzi vitu ambavyo vina manufaa kwao. Simu walizonazo, ambazo zina uwezo wa kuwapa ujuzi mkubwa, wanazitumia kupoteza muda kwa mambo yasiyokuwa na tija kabisa. Ni jambo la kushangaza, lakini ndivyo binadamu walivyo, wakiachiwa wachague kwa utashi wao, wanachagua vitu visivyokuwa na manufaa kwao.

KUHUSU KUWEKEZA NDANI YAKO.

Kuwekeza ndani yako, kama tulivyoona ni kujijengea ujuzi ambao unakulipa zaidi. Ujuzi unaokuwa unajijengea unakuwa mali ambao huwezi kuipoteza. Kwa ujuzi huo unaweza kufanya kwa ubora zaidi kile unachofanya na hivyo kunufaika zaidi.

Wale wanaowekeza ndani yao ndiyo wanaotengeneza kipato kikubwa kwenye yale wanayofanya. Kadiri watu wanavyokuwa bora, ndivyo wanavyotoa thamani kubwa zaidi na kulipwa zaidi pia.

SOMA; Mpango Binafsi Wa Uwekezaji Kupitia Mifuko Ya Pamoja Ya UTT AMIS.

MAENEO YA KUWEKEZA NDANI YAKO.

Uwekezaji wa ndani yako unagusa maeneo mengi, lakini haya ya msingi yanapaswa kupewa kipaumbele.

1. Kujijua wewe binafsi. Hitaji la kwanza kwenye maisha ni kujitambua, kujijua wewe mwenyewe, uimara na madhaifu yako ili uweze kuchukua hatua sahihi mara zote.

2. Ujuzi wa kujenga biashara. Biashara ndiyo njia bora ya kuingiza kipato ambacho hakina ukomo. Lakini wengi wanaoingia kwenye biashara wamekuwa wanajikuta kwenye utumwa na ukomo wa kipato. Hiyo ni kwa sababu wanakosa ujuzi sahihi wa kujenga biashara zinazowaweka huru.

3. Ujuzi wa mauzo. Kila mtu kwenye maisha ni muuzaji na wanaofanikiwa ni wale ambao wako vizuri kwenye mauzo. Jifunze mauzo na uwe na ushawishi mkubwa, utaweza kupata makubwa.

4. Ujuzi wa uwekezaji. Kila mtu anaingiza kipato kwenye maisha yake, lakini wengi hawafanyi uwekezaji na hivyo kuwa tegemezi wa kipato kwa miaka yao yote, kitu kinachowatesa sana. Wanashindwa kuwekeza siyo kwa sababu kipato hakitoshelezi, bali kwa sababu hawana ujuzi wa kutosha.

5. Ujuzi wa mawasiliano. Maisha ni mawasiliano, wekeza kwenye kujifunza namna bora ya kuwasiliana na wengine, kupitia kuongea, kuandika na kusikiliza. Huu ni uwekezaji ambao utaimarisha mahusiano yako na kuongeza ushawishi wako.

Wekeza kwenye maeneo hayo matano na utaweza kufanya makubwa kwenye maisha yako.

JINSI YA KUWEKEZA NDANI YAKO.

Njia ya kuwekeza ndani yako inaenda kwa kanuni hii; MAARIFA + VITENDO.

Moja ni kupata maarifa, kwa kujifunza kupitia kusoma, kusikiliza na kuangalia.

Mbili ni kuweka maarifa hayo kwenye vitendo kupitia kufanya.

Unaweza kusoma sana kuhusu kuogelea, lakini kama hutaenda kwenye maji, huwezi kuwa mwogeleaji mzuri.

Hivyo usiishie tu kuyapata maarifa, yaweke kwenye vitendo na utaona fursa za kuboresha zaidi uwekezaji wako ili kupata matokeo makubwa.

HASARA ZA KUTOKUWEKEZA NDANI YAKO.

Hasara ya kutokuwekeza ndani yako ni kurudi nyuma kadiri muda unavyokwenda. Watu wengi huwa wanadhani maisha yanasimama, kumbe siyo. Maisha yanaenda mbele, hivyo kama na wewe huendi nayo mbele, yanakuacha nyuma.

Kama unaanza kazi, biashara au chochote, muda unakwenda na hujifunzi vitu vipya, siyo kwamba umebaki pale ulipo, bali unakuwa umerudi nyuma. Kwa kasi kubwa ya mabadiliko ya teknolojia kwa sasa, kama hauendi na kasi hiyo, unaachwa nyuma na itakuwa hasara kubwa kwako.

Kila wakati fanya uwekezaji endelevu ndani yako ili uendane na kasi ya mabadiliko na uweze kufanya makubwa.

MJADALA WA SOMO.

Karibu kwenye mjadala wa somo, shiriki kwa kujibu maswali haya;

1. Kwa nini kuwekeza ndani yako ndiyo uwekezaji bora zaidi kwenye maisha yako?

2. Ni uwekezaji kiasi gani umekuwa unafanya kwenye maeneo matano muhimu ya kujijengea ujuzi?

3. Ni muda kiasi gani uliotenga kila siku na wakati gani kwa ajili ya kufanya uwekezaji endelevu ndani yako?

4. Karibu uulize swali kuhusu somo la leo au programu ya NGUVU YA BUKU.

Tuma majibu ya maswali hayo kama uthibitisho wa kusoma na kuelewa somo hili na kwenda kuweka kwenye matendo ili uwe mtu bora na mwekezaji bora pia.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.