3391; Gharama ya bure.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Hakuna vitu vyenye gharama kubwa kwenye maisha kama vitu ambavyo ni vya bure au vya gharama rahisi.
Pamoja na kujiona unapata kitu bure au kwa gharama rahisi, unaishia kulipa gharama kubwa zaidi.
Lakini kwa bahati mbaya sana, hivyo sivyo wengi wanavyoona mambo.
Wakishasikia neno bure au rahisi, akili zao zinaacha kufikiri na hisia zina tawala.
Hata wakati wanalipa gharama kubwa kutokana na bure waliyochagua, bado hawaoni ni gharama wanalipa.
Tunachoweza kuwa na uhakika nacho kwenye maisha ni hakuna ambacho ni cha bure kabisa.
Kila kitu kina gharama zake, zinaweza kuwa wazi au zimejificha. Pia zinaweza kuwa za sasa au za baadaye.
Kilicho na uhakika ni gharama lazima zilipwe na zitalipwa na mnufaika wa kitu husika.
Gharama zinaweza kulipwa kwa;
1. Muda; Chochote kinachoonekana ni bure au nafuu, kinachukua muda wako mwingi. Hivyo unaweza kuokoa fedha, lakini ukaishia kupoteza muda, ambao ni wa thamani kuliko fedha.
2. Ushawishi; Unaweza kupata kitu bure au kwa nafuu, lakini ikakuondolea ushawishi wako kwenye mambo mengine.
3. Upendeleo; Unapata kitu bure au kwa nafuu, halafu unalazimika kulipa fadhila fulani ambazo usingekuwa tayari kulipa kama hukupata cha bure.
4. Fedha; Unapata kitu bure au kwa nafuu, lakini baadaye unaishia kulipa gharama kubwa kuliko ambazo ungelipa mwanzoni.
5. Umakini; Mitandao ya kijamii unaitumia bure, lakini yenyewe inateka umakini wako na kuuza kwa wale wanaotangaza vitu vyao. Ukishapata bure, umakini unakuwa siyo wako tena.
6. Taarifa; Umewahi kugundua vitu unavyopata bure au kwa gharama nafuu unalazimika kutoa taarifa zako nyingi sana? Taarifa zako zina manufaa makubwa kwa wale wanaozikusanya.
7. Mamlaka; Anayelipia disko ndiye anayechagua nyimbo, kamwe usisahau hilo. Unaweza kupata kitu bure au kwa bei rahisi, lakini inakunyima mamlaka ya kufanya maamuzi.
Gharama ni nyingi na zipo kwenye kila eneo la maisha yetu.
Wajibu wako ni kujiuliza ni gharama gani ambazo hazipo wazi kwenye kitu ambazo utaishia kuzilipa.
Mara zote hakikisha unajua gharama halisi za kila maamuzi unayofanya ili uweze kuchagua kwa usahihi.
Ukijua gharama halisi, utaachana kabisa na kuhangaika na bure au rahisi ambazo zinakupotosha na kukugharimu zaidi.
Kutoka kwa rafiki yako, Kocha Dr. Makirita Amani.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe