Rafiki yangu mpendwa,
Watu wengi wamekuwa wanaingia kwenye biashara kwa kusukumwa na tamaa ya kupata vitu wanavyotaka. Kuna ambao tamaa yao ni kupata kipato kikubwa zaidi. Na wapo ambao wanataka kupata uhuru zaidi. Vyote hivyo vinawezekana kwenye biashara, lakini siyo kirahisi kama wengi wanavyodhani.
Kabla ya kupata kipato kikubwa na uhuru kwenye biashara ya aina yoyote ile, utapitia vipindi vya kipato kidogo na kutokuwa na uhuru kabisa. Hivyo ni vipindi vigumu sana kibiashara ambavyo wengi wamekuwa wanakata tamaa na kuishia njiani.

Kuna misingi ambayo ukiizingatia tangu mwanzo wa biashara yako, inakusaidia sana kupita vipindi hivyo vigumu na kuweza kupata mafanikio makubwa kwenye biashara yako.
Hapa nakwenda kukushirikisha misingi mitatu ambayo ukijenga biashara yako juu yake, itaweza kukupa mafanikio makubwa.
Moja ni uza kile ambacho watu wanakitaka.
Watu huwa wanahangaika sana ni biashara gani wafanye, wakijaribu kuja na mawazo mapya na ya kipekee ili wajitofautisha na wafanyabiashara wengine. Lakini mawazo mapya mara nyingi yamekuwa yanashindwa.
Wewe usihangaike kuja na vitu vipya, anza na mahitaji ambayo tayari watu wanayo. Anza kwa kuuza vitu ambavyo tayari watu wanavinunua, ila hawavipati kwa ubora, unafuu au uharaka.
Wewe ukiweza kuwapa watu kila ambacho wanakitaka, kwa ubora, unafuu au uharaka ambao haupo sokoni, utaweza kujenga biashara yenye mafanikio makubwa.
Mbili ni uza kwa wateja wenye fedha.
Wengi wanapoanza biashara huwa wanalenga kila anayeonekana kuwa na uhitaji, matokeo yake ni kujikuta wakiwa na wateja wengi ambao wanaishia kuwasumbua.
Wewe lenga aina ya wateja ambao tayari wana fedha za kuweza kumudu kununua kile unachouza. Lenga wateja ambao wanaweza kulipa gharama unazotoza na wakaridhika na thamani unayowapatia.
Haijalishi watu wana uhitaji wa kitu kwa kiasi gani, kama hawana uwezo wa kumudu, hawawezi kuwa wateja wazuri kwako na biashara haiwezi kufanikiwa.
Wauzie wateja ambao wanaweza kumudu kile unachowauzia ili uweze kujenga biashara yenye mafanikio makubwa.
Tatu ni kuwa na timu ya kuendesha biashara.
Kufanya kila kitu peke yako kwenye biashara ndiyo kanuni ya kushindwa kibiashara. Hiki ni kitu ambacho wengi wanakipenda kwa sababu ya urahisi wa kufanya wenyewe kuliko kufundisha wengine. Lakini pia kunakuwa hakuna gharama kubwa za uendeshaji.
Lakini ukweli ni kwamba huwezi kujenga biashara yenye mafanikio makubwa kwa kufanya kila kitu peke yako. Unapaswa kujenga timu bora ya kuendesha biashara yako ili majukumu ya biashara yaweze kutekelezwa kwa ukubwa. Wajibu wako mkubwa kwenye biashara ni kuhakikisha biashara inaweza kujiendesha hata kama wewe haupo moja kwa moja. Utaliweza hilo kwa kuwa na timu nzuri.
Jenga timu ya kuendesha biashara yako kwa kuajiri watu wenye uwezo wa kutekeleza majukumu unayowapa ili kuzalisha matokeo makubwa kwenye biashara na kufanikiwa kibiashara.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimefafanua zaidi mambo haya matatu na jinsi ya kuanza kuyafanyia kazi ili kujenga biashara yenye mafanikio makuba. Karibu ujifunze kwenye kipindi hicho hapo chini;
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.