3392; Unapata kile unachovumilia.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye maisha, huwa hatupati kile tunachotaka.
Bali tunapata kile tunachovumilia.
Kama unavumilia watu wazembe, utaishia kuwa na watu wazembe wengi wanaokuzunguka.
Hiyo ina maana kwamba matokeo uliyonayo sasa, yanadhihirisha ni vitu gani umekuwa unavumilia kwenye maisha yako.
Matokeo unayopata sasa, ndiyo ambayo umekuwa unayavumilia.
Unachovumilia kinatokana na viwango unavyokuwa umejiwekea.
Kama una viwango vya juu na ambavyo unavisimamia mara zote, utapata matokeo mazuri.
Lakini kama huna viwango vyovyote unavyosimamia, utapokea matokeo ya kila aina na kuishia kuvumilia matokeo ambayo ni ya chini.
Pitia viwango vyote ambavyo umejiwekea kwenye yale unayofanya na uone kama vipo juu kiasi cha kutosha kuondoa kabisa matokeo ya chini. Maana hayo ndiyo unaishia kuyapata kwa wingi pale unapokuwa huna viwango vya juu.
Unachonyamazia, unakiruhusu.
Na unachoruhusu, unakikuza.
Pale kitu kisichokuwa sahihi kinapofanyika, unapaswa kukisemea.
Kwani unapokaa kimya, inatafsiriwa kwamba umeruhusu kitokee.
Na kama umeruhusu kitu kitokee mara moja, maana yake umekipa tiketi ya kuendelea kutokea.
Hilo linaenda hata kwenye mambo yako binafsi.
Afya yako ni matokeo ya yale unayovumilia.
Upo vile ulivyo kiafya kwa sababu ya yote ambayo umeyavumilia.
Kuanzia vile unavyokula mpaka uzito ulionao.
Kama usingekuwa unavumilia chochote ulichonacho sasa, usingekuwa nacho.
Kabla hatujalaumu wengine kuhusu matokeo tunayopata, tuanzie kwetu sisi wenyewe.
Tujiulize kwa nini tumeyaruhusu matokeo hayo yatokee.
Tuangalia ni kwa namna gani tumekuwa tunayavumilia matokeo hayo mpaka kuyapa nafasi ya kutokea kwa namna yanavyotokea.
Tukibadili viwango vyetu na yale tunayovumilia, tutabadili kabisa matokeo tunayoyapata.
Mafanikio ni kukataa kuvumilia chochote ambacho ni tofauti na matokeo unayoyataka.
Jua ni nini hasa unachotaka, kisha kataa chochote chini ya hapo.
Kwa kukataa chochote cha chini, unaishia kupata cha juu kabisa, ambacho ndiyo hasa unachotaka.
Kutoka kwa rafiki yako, Kocha Dr. Makirita Amani.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe