Rafiki yangu mpendwa,
Kuwa na maisha tulivu, ambayo tunaridhishwa nayo ni kitu kigumu sana. Hiyo ni kwa sababu huwa ni rahisi kwetu kujilinganisha na wengine na kuona kuna namna ambavyo hatujakamilika kama wao.
Kutokukamilika kwetu kunatunyima utulivu na hivyo kushindwa kuwa na maisha ya mafanikio. Ni labda tunakazana sana kupata ukamilifu ili turidhike, kitu ambacho huwa hakitokei. Au tunakata tamaa na kuona hatuyawezi maisha kwa sababu hatujakamilika.
Hizo zote siyo njia sahihi za kukabiliana na mapungufu ya maisha yetu. Falsafa ya Ustoa inatupa mwongozo sahihi wa kukabiliana na madhaifu tuliyonayo na kuweza kuyaishi maisha yetu kwa utulivu na mafanikio makubwa.

Mwanafalsafa Marcus Aurelius kwenye kitabu cha nane cha Meditations ameshirikisha baadhi ya mambo ya kufanya ili kuweza kukabiliana na madhaifu na kuyaishi maisha yetu. Karibu ujifunze mambo hayo na hatua za kuchukua ili uweze kujenga maisha ya mafanikio makubwa kwako.
Moja; kubali madhaifu yako na uishi maisha yako.
Badala ya kukazana kuwa na ukamilifu, kubali kwamba hujakamilika. Tambua una madhaifu ambayo unayo kwenye baadhi ya maeneo ya maisha yako. Hupaswi kuhangaika na madhaifu hayo, badala yake kubali kwamba unayo. Kisha chagua kuyaishi maisha yako kwa kufanya yale ambayo una uimara nayo.
Hapa pia unapaswa kuacha kufikiria wengine wanakuchukuliaje, badala yake fikiria ni nini unachofanya chenye mchango kwa wengine. Wengine wanafanya nini au kusema nini juu yako hilo siyo tatizo lako. Unachopaswa ni kuwa wa manufaa, kwa kutumia uimara wako kufanya mambo yanayotoa thamani kwa wengine.
Mbili; jiulize madhara ya kitu kabla hujafanya.
Kabla ya kufanya kitu, kwanza jiulize; Nini madhara ya hiki ninachofanya? Mara nyingi sana watu wamekuwa wanafanya mambo, halafu wanashangaa pale wanapopata matokeo ya aina fulani. Ni kama vile walijipa uhakika matokeo wanayotaka wao ndiyo yatakayotokea.
Ukweli ni kwamba kwa kila jambo tunalofanya, kuna madhara mbalimbali yanayoweza kujitokeza. Hata kama kuna matokeo tunayotaka kupata, bado kuna matokeo mengine usiyoyataka ambayo pia yana nafasi ya kutokea. Kwa kujua matokeo yote yanayoweza kutokea na kujiandaa nayo vizuri, hutashangazwa pale yanapotokea.
Kama unataka uwe na maisha tulivu, hupaswi kushangazwa na jambo lolote linalotokea kwenye maisha. Kwa sababu unapaswa kuwa unatarajia lolote kutokea na hivyo wajibu wako ni kuchukua hatua sahihi kulingana na matokeo yaliyopatikana.
SOMA; Mazoezi 10 Ya Falsafa Ya Ustoa Yatakayofanya Uwe Na Maisha Bora.
Tatu; huwezi kuwabadili watu.
Marcus Aurelius ameandika sentensi moja ambayo tunapaswa kuikariri kwa herufi kubwa. Sentensi hiyo inasema; ‘UNAWEZA KULIPUKA KWA HASIRA, LAKINI WATU WATAENDELEA KUFANYA YALE AMBAYO WAMEKUWA WANAFANYA.’
Tumekuwa tunajihangaisha sana na kutaka kuwabadili watu, wawe vile tunavyotaka sisi. Tunaweza kutumia ushawishi au kutumia nguvu, kutumia zawadi au adhabu. Lakini watu huwa hawakubali kubadilishwa, bali wanabadilika kama wataamua wenyewe.
Unaweza kulipuka kwa hasira sana juu ya yale ambayo watu wanafanya, ukitegemea watakuelewa na kubadilika. Lakini utashangazwa na jinsi ambavyo baada ya hapo watarudi kwenye mazoea yao. Yaani wataendelea kama vile hakuna kilicho tokea.
Swali ni je tukubaliane na watu wazembe kwa sababu hawawezi kubadilika? Jibu ni hapana, tunapaswa kuweka viwango vya juu kwa watu tunaojihusisha nao, tujihusishe na wale tu ambao tayari wako vile tunavyotaka na hivyo hatuna haja ya kuwabadili. Ukishajikuta uko na watu ambao unalazimika kuwabadilisha, jua tayari umechagua maisha yanayokosa utulivu.
Nne; majuto ni lawama za kujikosesha fursa.
Majuto ni lawama unazojipa wewe mwenyewe pale unapojikosesha fursa nzuri ambazo ungeweza kuzitumia kwa manufaa. Hilo hutokea pale unapochelewa kuchukua hatua sahihi na hivyo kuzikosa fursa.
Hivyo basi, ili kupunguza lawama kwenye maisha, unapaswa kuchukua hatua kwenye fursa zote zinazokuja mbele yako na ukaona zina manufaa kwako. Hii haimaanishi ukimbizane na kila fursa, bali uchague zile fursa ambazo zinakufaa kwenye yale ambayo tayari unayafanya na kuweza kukupa matokeo makubwa zaidi.
Tano; usingizi hata wanyama wanao.
Marcus anatupa nukuu nyingine yenye nguvu sana, anasema; “Unapoona ugumu kuamka, kumbuka kufanya kazi ndiyo kuendana na asili ya binadamu na yako, wakati kulala ni kitu ambacho hata wanyama wanafanya.”
Ujumbe mkubwa sana wa kuondoka nao kwenye hiyo nukuu ni kuwa na maisha tulivu na yenye mafanikio, ishi kwa asili ya binadamu ambayo ni kufanya kazi zenye manufaa kwa wengine. Usijiendee tu kama wanyama ambao wapo kwa ajili ya uhai wao.
Usipende usingizi au vitu vingine ambavyo hata wanyama wanavifanya. Onyesha utofauti wako wewe binadamu na wanyama wengine ili uweze kuyaishi maisha yako kwa usahihi na kufanya makubwa.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeshirikisha mambo mengine mengi zaidi kutoka falsafa ya Ustoa yanayotuwezesha kuwa na maisha tulivu na ya mafanikio. Karibu ujifunze kwenye kipindi hicho hapo chini.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.