Habari Njema Wauzaji Bora Kuwahi Kutokea.
Mafanikio kwenye kila eneo la maisha yako, yanachangiwa na vitu vingi vidogo vidogo ambavyo unaweza usione nguvu yake. Hakuna mafanikio makubwa yanayotokana na vitu vichache. Ndiyo maana wale wanaokazana na vitu vichache pekee, huwa hawapati mafanikio na hata wakiyapata hayadumu kwa sababu vitu vidogo vidogo ambavyo hawakuzingatia vinawaangusha.
Moja ya vitu vidogo vidogo vinavyoathiri mafanikio yako ni mazingira yanayokuzunguka. Unaweza kuyachukulia mazingira kwa hali ya ukawaida, ila yana mchango sana kwenye mafanikio yako.
Kwenye mauzo, mazingira yako yana mchango kwako kuweza kuuza zaidi au kukuzuia usiuze zaidi. Kwenye somo hili tunakwenda kujifunza jinsi ya kutengeneza mazingira sahihi ambayo yatakufanya wewe uwe muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa.

Katika kutengeneza mazingira sahihi ili kufanya mauzo makubwa, mazingira yamegawanyika kwenye sehemu mbili; mazingira binafsi na mazingira ya mauzo. Karibu ujifunze mambo ya kufanya kwenye kila aina ya mazingira ili uweze kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa.
Mazingira binafsi.
Mazingira binafsi ni yale yanayokuzunguka kwenye maisha yako binafsi. Haya ni mazingira muhimu kwako na yana athari kwenye mtazamo unaokuwa nao kitu kinachoathiri mauzo.
Katika kujenga mazingira binafsi sahihi ili kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa, fanya yafuatayo;
1. Ishi sehemu safi na yenye mpangilio mzuri. Hili ni muhimu kwenye kuhakikisha unakuwa na usafi na utulivu binafsi ambao unakupa utulivu kwenye mauzo pia.
2. Lala sehemu tulivu na inayokupa mapumziko ya kutosha kwenye muda unaolala. Hili linahakikisha mwili wako unakuwa na nguvu wakati wa mauzo ili kuweka umakini mkubwa kwenye mauzo badala ya kukosa umakini kunakoletwa na uchovu.
3. Ondoa kwenye mazingira yako vitu vyote ambavyo vinahusiana na tabia unazotaka kuvunja. Kama kuna tabia ambazo unataka kuachana nazo, hatua muhimu ni kujenga mazingira ambayo hayachochei tabia hizo. Kwa mazingira kutokuwa na kichocheo cha tabia inakuwa rahisi kutokufanya kuliko kichocheo kikawepo halafu ukawa unakazana kujizuia. Kama kuna vitu unavyotaka kuacha kutumia, visiwepo kwenye mazingira yako huku vile unavyotaka uwe unatumia viwepo kwenye mazingira yako.
SOMA; Zungukwa Na Watu Sahihi Ili Uweze Kuwa Muuzaji Bora Na Kufanya Mauzo Makubwa.
Mazingira ya mauzo.
Mazingira ya mauzo ni yale unayoyatumia wakati unafanya mauzo. Mazingira haya huwa yana athari za moja kwa moja kwenye mauzo unayoyafanya. Ili kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa, zingatia yafuatayo kwenye mazingira ya mauzo;
1. Usafi na mpangilio. Eneo lako la mauzo linapaswa kuwa safi na lenye mpangilio mzuri. Usafi unapaswa kuwa wa eneo husika na vitu vilivyopo kwenye eneo hilo. Vitu vinavyouzwa viwe kwenye hali ya usafi. Pia mpangilio uwe mzuri kwa kila kitu kujulikana mahali kilipo. Hilo linapunguza muda wa kutafuta kitu mahali ambapo kipo.
2. Uwepo wa vyote unavyohitaji. Vitu vyote unavyokuwa unahitaji ili kukamilisha mazungumzo ya mauzo na mteja unapaswa kuwa navyo na kuviandaa vizuri. Kama ni vielelezo au vitu vya kutoa mfano au majaribio, viwepo tayari na kuwa vinafanya kazi ili zoezi liende vizuri. Kukosa maandalizi sahihi ya mazungumzo ya mauzo imekuwa chanzo cha mauzo mengi kushindwa, usiruhusu hilo litokee kwako.
3. Mwonekano wenye ushawishi kwa wateja. Lifanye eneo lako la mauzo kuwa na ushawishi kwa wateja kununua. Hii inatofautiana kulingana na aina ya biashara na wateja wanaolengwa. Biashara ambazo zinauza vitu vya bei kubwa, eneo la biashara linapaswa kuwa linaonyesha thamani ya juu. Kadhalika mpangilio wa bidhaa au huduma zinazotolewa, unapaswa kuwafanya wateja waweze kuona vitu vingine vingi, hata ambavyo hakuwa amepanga kununua ili ajue vipo na kushawishika kununua. Kwa biashara zinazouza bidhaa na wateja kufika eneo la biashara, mpangilio wa bidhaa unapaswa kuwa wenye ushawishi mzuri kwa wateja.
4. Uwepo wa vitu vinavyokuhamasisha. Kila mtu ana vitu ambavyo vinamhamasisha kuweka juhudi kwenye kazi zake. Kuna ambao picha za wapendwa wao zinawahamasisha, hivyo wakiwa nazo karibu inawasukuma kufanya kazi kwa juhudi. Kuna ambao rangi au vitu fulani vikiwepo inawahamasisha. Na kuna ambao picha za waliofanikiwa na nukuu mbalimbali zinawahamasisha. Kulingana na aina ya biashara uliyopo na yale yanayokuhamasisha, tengeneza mazingira yanayokuwa na vitu hivyo.
5. Zana zako za kazi ziwe vizuri. Zana unazotumia kwenye kufanya mauzo zinapaswa kuwa vizuri wakati wote. Simu kama zana kuu lazima iwe na chaji na iwe na kifurushi cha kuwezesha mawasiliano yote unayofanya na wateja wako. Ni uzembe wa hali ya juu kwa simu yako kuishiwa chaji wakati ambao ni wa mauzo, wakati hiyo ndiyo zana kuu. Kadhalika kwa zana nyingine unazotumia kulingana na biashara yako, hakikisha zipo vizuri na tayari kwa matumizi ili usikwame.
Kwa nguvu ambayo mazingira yanayo kwako binafsi na kwenye mauzo yako, hakikisha unatengeneza mazingira yanayokuwezesha kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa zaidi. Kuna ambayo kwenye mazingira yapo nje ya uwezo wako, lakini wewe fanyia kazi yote yaliyo ndani ya uwezo wako ili uwe na mazingira yanayokuchochea kufanikiwa.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.