Rafiki yangu mpendwa,
Watu wanaoanzia chini kabisa kifedha, yaani kwenye umasikini, huwa hawana namna bali kufanya chochote halali kinachowaingizia kipato.
Kupata fedha za kuendesha maisha yao ndiyo unakuwa msukumo mkubwa kwao, bila ya kujali kama wanapenda wanachofanya au la.
Hiyo ni hatua muhimu ya kuanzia, lakini kwa bahati mbaya sana wengi hujisahau na kujikuta wanabaki kwenye hali hiyo.
Wanapokazana kuongeza kipato chao kupitia kile walichoanza nacho, wanajikuta wakikosa uhuru na hata furaha. Hiyo inasababishwa na hali kwamba wanachofanya wanakuwa hawakipendi, hivyo maisha yao yanakuwa ya hovyo.
Kadiri unavyopiga hatua kwenye maisha yako, kutoka kwenye umasikini na kwenda kwenye utajiri, ndivyo pia unavyopaswa kuwa unabadili kile unachofanya, ili kiendane na wewe vizuri.

Kwenye kufanya na kupata fedha, mapenzi huwa yanahusika. Hilo linapelekea mapenzi na fedha kuwa na uhusiano ambao ni muhimu mtu kuujua ili kupata mafanikio na furaha.
Kwenye kufanya kunakuwa na hali mbili; KUPENDA na KUTOKUPENDA kile ambacho unafanya.
Kwenye fedha kuna hali mbili; KULIPA na KUTOKULIPA fedha nyingi.
Unapoleta vitu hivyo pamoja, unapata hali nne za mapenzi na pesa.
Hali ya kwanza ni KUTOKUPENDA na KUTOKULIPA.
Hapa mtu unakuwa hupendi kile unachofanya na pia hakikupi fedha za kutosha. Hii ni hali ya chini sana, hali ya mateso kwa sababu maisha yanakupiga kwenye kila kona.
Hii ni hali ambayo unapaswa kuondoka haraka sana, haina maana yoyote kufanya kitu ambacho hukipendi na pia hakikulipi.
Hali ya pili ni KUPENDA na KUTOKULIPA.
Hapa mtu unakuwa unapenda kile unachofanya, lakini hakikulipi. Hapa ndipo yanapokuwa mapenzi na hobi ambazo watu wanakuwa nazo. Ni vitu vizuri kufanya na vinavyokupa hali ya kupumzika na kuridhika.
Unapokuwa unaanzia chini kabisa hupaswi kuweka muda wako mwingi kwenye vitu vya aina hii. Ila kadiri unavyozidi kutoka kwenye umasikini, utaweza kuweka muda zaidi kwenye vitu unavyopenda kufanya, japo havikulipi. Unafanya kwa ajili ya kuvifurahia na siyo vikulipe.
Hali ya tatu ni KUTOKUPENDA na KULIPA.
Hapa mtu unakuwa hupendi kile unachofanya, lakini kinakulipa vizuri. Hapa ndipo unapopaswa kuanzia wakati uko chini kabisa, kwa sababu hitaji lako la kwanza ni kutoka kwenye umasikini. Umasikini unaumiza kuliko mapenzi yako kwenye kile unachofanya.
Unapokuwa hujafikia uhuru wa kifedha, usichague nini unafanya, kama ni halali kisheria na kimaadili na kinakuingizia kipato kikubwa, unapaswa kukifanya. Kwa sababu ni wajibu wako wa kimaadili, kwako na kwa watu wako wa karibu kutoka kwenye umasikini kwa njia zozote halali.
Hali ya nne ni KUPENDA na KULIPA.
Hapa mtu unakuwa unapenda kile unachofanya na kinakulipa vizuri. Hii ndiyo ngazi ya juu kabisa ya mapenzi na pesa, ambapo watu wanakuwa tayari kukulipa kufanya unachopenda kufanya.
Kwenye ngazi hii, unakuwa hufanyi tena kazi, bali unakuwa kama unacheza. Yaani unayafurahia maisha yako na watu wanakulipa kwa wewe kuyafurahia maisha. Kwa sababu hiyo unakuwa na msukumo wa kufanya kwa ukubwa ambapo inakuwa vigumu kwa watu kushindana na wewe.
Kwa bahati mbaya sana, unapokuwa unaanzia chini, ni vigumu watu kukulipa kwa kufanya unachopenda. Wakati wewe una mahitaji makubwa ya fedha. Hivyo unaanza na kile kinachotatua mahitaji yako, huku ukikumbuka kurudi kwenye kile unachopenda kadiri unavyoendelea kupiga hatua.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimefafanua kwa kina hali hizi za mapenzi na pesa ili uweze kuzitumia vizuri, hatua kwa hatua kujenga maisha yenye mafanikio na uhuru mkubwa. Karibu uweze kujifunza.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.