Rafiki yangu mpendwa,
Watu wanatofautiana kwenye mambo mengi sana, kuanzia nchi, dini, kabisa, rangi, jinsia na mengine.
Lakini kuna kitu kimoja pekee ambacho kinawaunganisha watu wote bila ya kujali tofauti zai.
Kitu hicho ni Pesa. Watu watakubagua kwa mambo mbalimbali ambayo uko tofauti, lakini hawatazibagua pesa zako. Watatumia kila namna kuhakikisha wanazipata.
Jambo moja la kushangaza sana ni kama wote tunaungana pamoja inapokuja kwenye pesa, kwa nini matokeo ya yanatofautiana sana?
Kwa nini watu ambao wamezaliwa familia moja, wamepata malezi ya aina moja, elimu sawa na kufanya shughuli zinazofanana, bado matokeo yao ya kifedha yanatofautiana?
Utakuta mmoja ameweza kujenga utajiri kwenye maisha yake wakati mwingine ameishia kwenye umasikini. Swali ni nini kinachangia yote hayo?

Mwandishi Morgan Housel kwenye kitabu chake kinachoitwa THE PSYCHOLOGY OF MONEY ametupa majibu ya kitendawili hicho.
Kupitia kitabu chake Housel anaeleza kwamba inapokuja kwenye pesa, mantiki huwa haina nafasi sana.
Maamuzi mengi tunayoyafanya kwenye fedha huwa yanasukumwa na hisia na tabia. Na kwa sababu watu wanatofautiana kwenye hisia na tabia, hata matokeo ya kifedha yanatofautiana pia.
Kwenye kitabu hicho, Housel ametupa masomo 20 ya msingi kuhusu fedha, utajiri, tamaa na furaha. Kupitia masomo hayo tunapata nafasi ya kujifunza mambo ya kuzingatia ili kufanya maamuzi bora kifedha kwetu na kujenga utajiri na furaha.
Utangulizi; Bonge La Shoo.
Mwandishi anatuambia kwamba kuna vitu viwili ambavyo vinawaathiri watu wote; AFYA NA FEDHA. Wakati maendeleo ya sayansi yakiboresha sana kwenye afya, upande wa fedha ni tofauti, kwani mambo mengi bado yanafanyika kwa mazoea.
Kumekuwepo na ushauri mwingi mzuri unaotolewa kwenye eneo la fedha, lakini bado inapokuja kwenye kufanya maamuzi, watu wanatumia hisia na tabia zao. Na hilo ndiyo limekuwa linapelekea watu kupata matokeo tofauti.
Ni kwenye fedha pekee ambapo mtu mwenye akili nyingi, aliyepata elimu kubwa na uzoefu anaweza kushindwa na mtu mwenye akili ndogo na asiyekuwa na elimu kubwa wala uzoefu.
Kwenye fedha, yule mwenye tabia sahihi na anayeweza kudhibiti hisia zake ndiye anayekuwa mshindi.
Hiyo ndiyo saikolojia ya pesa tunayopaswa kuijua ili kujenga utajiri na furaha kwenye maisha yetu.
1. Hakuna Mwenye Wazimu.
Ukiwaangalia wengine jinsi wanavyofanya maamuzi yao ya fedha, unaweza kuona wanayofanya ni ya ajabu sana. Unaweza kudhani watu hao wamepatwa na wazimu kiasi cha kufanya maamuzi ambayo yanawagharimu zaidi kifedha.
Lakini yule anayefanya maamuzi ya kifedha, anaona yuko sahihi kabisa. Hiyo ni kwa sababu anafanya maamuzi hayo kwa kutumia uzoefu wake binafsi, ambao hakuna mwingine aliyenao.
Maamuzi yetu ya kifedha yanaathiriwa sana na mtazamo tuliojijengea na uzoefu tuliopitia kwenye maisha yetu. Ndiyo maana watu wanatofautiana kwenye maamuzi ya kifedha, kwa sababu hakuna watu wawili wenye mtazamo unaofanana au uzoefu sawa.
Unapoona wengine wanafanya maamuzi ya kifedha ambayo ni mabaya kwao, usidhani wana wazimu, jua kwa upande wao wapo sahihi kabisa.
Hatua muhimu ya kuchukua hapa ni kuhakikisha unajijengea mtazamo sahihi kifedha na kujenga uzoefu mpya ambao unakuwezesha kufanya maamuzi bora. Uzoefu unaohitaji utajifunza kwenye kitabu hiki.
SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; The Psychology Of Money (Masomo Kuhusu Utajiri, Tamaa Na Furaha)
2. Bahati Na Hatari.
Matokeo tunayoyapata kwenye maisha, hayatokani na maamuzi na juhudi zetu kwa asilimia 100. Kuna nguvu nyingine nje ya maamuzi na juhudi zetu ambazo zinaathiri matokeo tunayoyapata.
Nguvu hizo ni bahati (luck) na hatari (risk), hizi ni nguvu mbili zinazopingana, lakini zinazoambatana pamoja. Penye bahati huwa pia pana hatari.
Bahati ni pale unapopata matokeo mazuri kuliko juhudi ulizoweka. Watu huwa hawapendi kukiri bahati imehusika kwenye matokeo yao. Hivyo hupata kiburi kwa matokeo waliyopata na hatimaye kuanguka kwa sababu wanashindwa kuyarudia matokeo hayo.
Hatari ni pale unapopata matokeo mabaya kuliko juhudi ulizoweka. Matokeo mabaya huwa yanaweza kusababishwa na hatari au uzembe. Kwa kuwa watu huwa hawapendi kuonekana ni wazembe, huwa wanaona ni hatari zilizokuwa nje ya uwezo wao.
Hatua za kuchukua;
Unapopata matokeo mazuri, jiulize ni asilimia ngapi ya matokeo hayo imesababishwa na juhudi zako na asilimia ngapi imetokana na bahati. Hilo litakufanya uwe mnyenyekevu.
Unapopata matokeo mabaya, jiulize ni asilimia ngapi ya matokeo hayo imesababishwa na uzembe wako na asilimia ngapi imetokana na hatari. Hilo litakuwezesha kufanya maamuzi bora zaidi.
3. Kutokutosheka.
Ubepari umefanikiwa kwenye mambo mawili; kuzalisha utajiri mkubwa na kuzalisha wivu. Uchumi mzima wa ubepari unachochewa na wivu. Ni pale watu wanapoona wengine wakiwa na vitu vizuri au wamepiga hatua kubwa, ndiyo na wao pia wanataka vitu hivyo.
Wivu unakuwa ni mzuri pale unapomsukuma mtu kutoka chini kwenda juu. Unapomfanya mtu kupata vitu ambavyo hana na ana uhitaji navyo. Hapo wivu unajenga na kuleta maendeleo.
Wivu unakuwa mbaya pale unapomsukuma mtu kutaka kuwazidi wengine kwa gharama yoyote ile. Pale mtu anapokuwa tayari kupoteza alichonacho na ambacho anakihitaji sana ili kupata ambacho hana na wala hakihitaji sana.
Wivu mbaya unatokana na hali ya kutokutosheka, mtu kutaka kupata zaidi na zaidi kwa gharama yoyote na hatimaye kuishia kupoteza hata kile ambacho alikuwa ameshapata.
Hatua ya kuchukua;
Usikubali kupoteza kile ulichonacho sasa na ambacho unakihitaji, kwa tamaa ya kupata ambacho huna sasa na huna uhitaji nacho. Haimaanishi usiendelee kujenga utajiri, bali usichukue hatari ambazo zitakupoteza kwa sababu ya tamaa ya kupata zaidi.
4. Nguvu Ya Mkusanyiko.
Vitu vinavyofanyika kidogo kidogo kwa muda mrefu bila kuacha, huwa zinazalisha matokeo makubwa sana. Hiyo ndiyo nguvu ya mkusanyiko, ambacho kila kinachofanyika kinaongezea kwenye kile ambacho kilishafanyika.
Nguvu ya mkusanyiko ipo kwenye muda, ni pale kitu kinapofanyika kwa muda mrefu zaidi ndiyo matokeo yake yanakuwa makubwa zaidi. Hivyo ndivyo ilivyo kwenye uwekezaji, kujenga biashara, kazi, ujuzi, mahusiano na mengine kwenye maisha yetu.
Mafanikio makubwa kwenye maisha siyo kupata marejesho makubwa zaidi ambayo hutokea mara chache, bali ni kupata marejesho ya kawaida kwa muda mrefu.
Hatua ya kuchukua;
Kwenye kujenga utajiri, fanya uwekezaji mdogo mdogo mara kwa mara kwa muda mrefu bila ya kuacha. Faida kubwa ya uwekezaji itatokana na muda ambao umewekeza.
Haya ni masomo manne ya kwanza kutoka kwenye kitabu cha THE PSYCHOLOGY OF MONEY kati ya masomo 20 yaliyopo. Kwenye makala inayofuata utajifunza masomo mengine.
Hapo chini kuna kipindi cha ONGEA NA KOCHA ambapo tumeweza kuwa na mjadala mzuri juu ya masomo haya. Karibu ujifunze kwa kina zaidi kupitia kipindi hicho.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.