Habari njema wauzaji bora kuwahi kutokea.

Kufikia wateja wengi na kwa msimamo ni hitaji muhimu kwenye biashara ili kuweza kufanya mauzo makubwa zaidi.

Zipo njia nyingi za kuwafikia wateja, kama ana kwa ana, simu, jumbe, matangazo na mitandao ya kijamii.

Kwa zama tunazoishi sasa, ambazo ni za kidijitali, mambo mengi yanafanyika kwa njia ya mtandao. Hivyo hata njia zinazotumika kuwafikia wateja, nyingi ni za mawasiliano na mtandao. Njia za kidijitali zimekuwa na nguvu kwa sababu ya wateja wengi wanaolengwa kuwa wanatumia njia hizo.

Lakini hilo haliondoi nguvu na umuhimu wa kutumia njia za kianalojia za kufikia wateja wanaolengwa na biashara. Zipo njia nyingi za kianalojia za kufikia wateja na moja ya njia hizo ni matumizi ya VIPEPERUSHI.

Vipeperushi ni njia ya kuwafikia wateja, ambayo ina nguvu ya kusambaa kwa ukubwa na kwa gharama ndogo ikaweza kuleta wateja wengi.

Karibu kwenye somo hili ujifunze kuwafikia wateja wengi kwa kutumia vipeperushi ili kuweza kutengeneza wateja wapya tarajiwa wengi zaidi na kukuza mauzo.

VIPEPERUSHI KAMA NJIA YA KUFIKIA WATEJA.

Vipeperushi ni kurasa zenye ujumbe wa kuwashawishi watu ambazo zinasambazwa kuwafikia wengi na kuwapa taarifa kuhusu uwepo wa kitu au tukio fulani.

Vipeperushi vinatumika kutangaza biashara na matukio mbalimbali ambayo yanahitaji kuwavutia watu wengi.

Vipeperushi vikiweza kuandaliwa na kusambazwa vizuri, vina nguvu ya kuwafikia wengi kwa gharama nafuu na kuwa na ushawishi mkubwa kwao kuchukua hatua.

KUANDAA VIPEPERUSHI VYENYE USHAWISHI.

Ili vipeperushi viweze kuwa na ushawishi mzuri kwa wateja wanaolengwa, vinapaswa kufanyiwa maandalizi mazuri. Ubunifu unapaswa kutumika kwenye kuandaa vipeperushi ili watu wavutiwe kupokea na kusoma na kupata ujumbe uliolengwa.

Katika kuandaa vizuri vipeperushi, yafuatayo yanapaswa kuzingatiwa.

1. Kichwa cha habari kinachonasa umakini.

Kitu cha kwanza kitakachomsukuma mtu kuangalia kipeperushi ni kichwa cha habari ambacho kinanasa umakini wake. Kichwa cha habari kinapaswa kugusa kitu ambacho mtu anakifiria kwenye akili yake ili kunasa umakini wake. Hiyo ni kwa sababu watu huwa wanaona zaidi vitu ambavyo tayari wanavifikiria.

Katika kuandaa vipeperushi, anza kwa kufikiria wateja unaowalenga huwa wanafikiria nini kinachohusiana na biashara yako kisha kutumia hayo kwenye kichwa cha habari.

2. Picha inayovutia.

Huwa kuna kauli inasema picha moja ni sawa na maneno elfu moja. Kwa sababu kipeperushi hakikupi nafasi ya kuweka maelezo mengi, unapaswa kuweka picha ambayo inamvutia mtu kuangalia, lakini pia inampa maelezo mengine anayopaswa kuyajua ili ashawishike.

Katika kuandaa vipeperushi, chagua picha nzuri na halisi za biashara ambazo zina ushawishi na zinazowafanya wateja kuelewa zaidi. Maana wanasema kama mtu hawezi kusoma, basi aweze kuona picha. Yaani picha iwe inajieleza kiasi kwamba hata kama mtu hatasoma maelezo, atakuwa ameelewa.

3. Maelezo yanayoibua tamaa.

Kutokana na udogo wa nafasi ya vipeperushi, huwezi kuweka maelezo mengi sana. Hivyo maelezo machache utakayoyaweka yanapaswa kuwa na ushawishi mkubwa kwa watu. Yawe ni maelezo yanayoibua tamaa kwa watu kuchukua hatua mara moja. Hapo inaweza kuwa ni ofa fulani iliyopo ambayo ina ukomo na hivyo mtu kusukumwa kuchukua hatua mara moja ili asikose.

Katika kuandaa vipeperushi, weka maelezo mafupi ambayo yanaibua tamaa kwa mtu kuchukua hatua. Weka ofa yenye ukomo ambayo itawasukuma watu kuchukua hatua mara moja.

4. Hatua ya mtu kuchukua.

Kipeperushi kinapaswa kueleza wazi hatua ambayo mtu anapaswa kuchukua, baada ya tamaa yake kuwa imeibuliwa. Hatua za kuchukua zinaweza kuwa tofauti, kupiga simu, kutuma ujumbe, kutembelea tovuti, kufika eneo la tukio na kadhalika. Kwa sababu watu hawana muda mwingi wa kusoma maelezo na kuchukua hatua nyingi, hakikisha hatua ya kuchukua ni rahisi kwa mtu kutekeleza.

Katika kuandaa vipeperushi, chagua hatua ya mtu kuchukua na ielezwe kwa namna inayoonekana kwa haraka. Hatua ya kuchukua iwe rahisi kwa mlengwa kufanya hivyo.

5. Mawasiliano yanayoonekana kwa urahisi.

Pamoja na hatua za kuchukua zinazokuwepo, mawasiliano ni muhimu kuwepo kwenye vipeperushi na yanapaswa kuonekana kwa utahisi na hata kwa mbali. Kwa kuwa njia za kusambaza vipeperushi zinahusisha kubandika maeneo mbalimbali, mawasiliano yanapaswa kuwa yanaonekana hata kwa mbali ili mtu aweze kuyatumia kupata taarifa zaidi.

Katika kuandaa vipeperushi, weka mawasiliano yanayoonekana kwa urahisi hata kwa mbali ili watu waweze kuyatumia kupata taarifa zaidi.

SOMA; Wateja tarajiwa wapo wengi zaidi.

KUSAMBAZA VIPEPERUSHI NA KUWAFIKIA WENGI.

Baada ya kuandaa vipeperushi vizuri, hatua inayofuata ni kuvisambaza kwa namna ambayo vitaweza kuwafikia wengi wanaolengwa. Kulingana na aina ya wateja wanaolengwa, njia kuu za kusambaza zinaweza kutofautiana baina ya wateja. Zifuatazo ni njia kuu za kusambaza vipeperushi ili kuwafikia wengi zaidi.

1. Kugawa kwa mtu mmoja mmoja.

Hii ni njia ya kupita na kugawa vipeperushi kwa mtu mmoja mmoja. Hii inaweza kuwa nyumba kwa nyumba, ofisi kwa ofisi, maeneo ya mikusanyiko na hata kwenye usafiri. Njia hii ina nguvu kwa sababu mtu anakabidhiwa kabisa kipeperushi, hivyo kama kina ushawishi mzuri, mtu anaweza kukitunza na kukitumia hata baadaye.

2. Kugawa maeneo yenye watu wengi.

Hii ni njia ya kugawa vipeperushi kwenye maeneo ambayo yana watu wengi. Tofauti na kutoa kwa mtu mmoja mmoja, hapa vipeperushi vinaweza kuwekwa eneo ambalo mtu anachukua au vikatawanywa kwa njia ambayo vitawafikia watu, iwe ni kwa kupeana au kuokota chini. Njia hii inarahisisha kugawa vipeperushi vingi, japo vingi vinaweza visiwafikie watu sahihi.

3. Kuweka kwenye maeneo ambayo watu wataviona.

Hii ni njia ya kuviweka vipeperushi maeneo ambayo hayana watu wakati unaviweka, lakini baadaye wataviona. Kwa mfano ukitembelea kwenye nyumba za watu na wakawa hawapo, ukaweka kipeperushi chini ya mlango, anapokuja na kufungua mlango anakikuta. Au kuweka kwenye vioo vya magari wakati watu hawapo, wanapokuja wanakuta vipeperushi. Njia hii ina nguvu ya kuwafikia watu moja kwa moja, na kama vimeandaliwa kwa ushawishi, vitasomwa kwa wingi.

4. Kubandika maeneo yanayoonekana.

Hii ni njia ya kubandika vipeperushi kama matangazo kwenye maeneo ambayo watu wanaweza kuona kwa urahisi. Mfano kwenye mbao za matangazo, vituo vya basi, nguzo za umeme, mapipa ya taka, kuta za nyumba, milango, vyombo vya usafiri n.k. Pale vipeperushi vinapowekwa maeneo ambayo watu wengi wanaviona na vikawa na ushawishi mzuri, wengi wanapata taarifa na kuweza kuchukua hatua.

5. Kusambaza kwa njia za mtandao.

Pamoja na kwamba vipeperushi ni njia ya analojia, bado vinaweza pia kusambazwa kwa njia za kidijitali. Hapa picha ya vipeperushi inaweza kusambazwa kwa njia ya mitandao kama barua pepe, mitandao ya kijamii, mitandao ya mawasiliano ya moja kwa moja (kama wasapu), kwenye tovuti na blog na njia nyinginezo. Njia hii inakuwa rahisi zaidi kwa sababu haihusishi gharama za uchapaji wa vipeperushi. Kikishaandaliwa kinaweza kusambazwa kwa ukubwa bila ya kuingia gharama kubwa.

Matumizi ya vipeperushi yana nguvu ya kuweza kuwafikia wateja wengi kwa gharama nafuu na kuwashawishi kuwa wateja. Kwa kufanyia kazi haya uliyojifunza hapa, kwenye kuandaa na kusambaza vipeperushi, utaweza kufikia wengi na kutengeneza wateja tarajiwa wengi zaidi na hatimaye kukuza mauzo kwenye biashara.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.