Habari njema wauzaji bora kuwahi kutokea.

Moja ya jukumu kubwa la biashara ni kuwafikia wateja wengi kila wakati. Na hilo linapawa kufanyika wakati wote na kwa njia mbalimbali ili wateja wote wanaolengwa waweze kufikiwa.

Pamoja na mabadiliko makubwa yanayotokana na zama hizi za maendeleo ya teknolojia, kuna njia za kutangaza biashara na kufikia wateja ambazo ni nje ya teknolojia lakini zina nguvu.

Moja ya njia hizo ni kutumia MABANGO. Mabango yanakuwa na maelezo ya biashara na kuweka kwenye maeneo ambayo ni rahisi kwa watu kuona na kujua kuhusu uwepo wa biashara. Mabango yakishawekwa yamewekwa na yataendelea kuwafahamisha watu kuhusu biashara husika kwa muda mrefu.

FAIDA ZA KUTUMIA MABANGO KUFIKIA WATEJA.

Mabango yana faida mbalimbali kwenye kuwafikia wateja kama ifuatavyo;

1. Gharama nafuu; kuandaa na kuweka bango la biashara kuna gharama nafuu ukilinganisha na manufaa yake. Japo kuna gharama za awali za kuandaa na gharama za kulipia kodi kwa baadhi ya mabango, bado ni nafuu ukilinganisha na matangazo mengine.

2. Kufanya kazi muda wote; mabango yakishawekwa yanawafikia watu muda wote, uwe wa kazi au siyo wa kazi.

3. Kutoa maelekezo ya ilipo biashara; baadhi ya mabango yanaweza kuelekeza biashara ilipo na kuwa rahisi kwa watu kuifikia.

MAENEO YA KUWEKA MABANGO.

Ili mabango yaweze kuwafikia wengi na kuwa na ushawishi, yanapaswa kuwekwa maeneo sahihi. Baadhi ya maeneo hayo ni kama;

1. Kwenye eneo la biashara ambapo bango linaitambulisha biashara na kufanya watu wajue iko hapo. Kuna wakati watu wanaweza kupita eneo fulani na wasijue kama kuna biashara ya aina hiyo, bango linawaonyesha kwa urahisi.

2. Maeneo yenye mzunguko mkubwa wa watu, hapo inakuwa rahisi kwa bango kuonekana na wengi na kuwaelekeza biashara ilipo.

3. Kwenye vyombo vya usafiri ambavyo vinazunguka maeneo mbalimbali na hivyo watu wengi zaidi kujua kuhusu uwepo wa biashara na mahali ilipo.

Ili mabango yawe na ufanisi mzuri, yanapaswa kuwafanya wengi wayaone.

SOMA; Kufikia Wateja Wengi Kwa Kutumia Vipeperushi.

MAMBO YA KUZINGATIA KWENYE KUANDAA NA KUWEKA MABANGO.

Ili mabango yaweze kuleta matokeo mazuri, yaani kuona na wengi wanaolengwa na kushawishika kuja kwenye biashara, mambo yafuatayo yanapaswa kuzingatiwa;

1. Bango linapaswa kuandaliwa kwa ubunifu ambao utawavutia watu kuangalia na hilo litawapelekea kupata ujumbe uliopo.

2. Maandishi yawe makubwa na yanayosomeka kwa mbali na yasiwe mengi sana maana hayatasomeka vizuri na hivyo kukosa ushawishi.

3. Maelekezo ya ilipo biashara na mawasiliano yaonekane kwa urahisi ili watu wanapoona wajue jinsi ya kuifikia biashara.

4. Mabango yawe na taa ili kuweza kuonekana wakati wa usiku na hivyo kuwafikia wateja usiku na mchana.

Kila biashara inapaswa kutumia mabango ambayo yatawawezesha wateja wanaolenga kujua kuhusu biashara na ilipo. Kuna wateja wengi ambao wanakuwa hawapatikani kwa sababu tu hawajui kuhusu uwepo wa biashara kwenye eneo husika, hata kama wanapita hapo kila siku. Mabango ambayo yameandaliwa na kuwekwa vizuri, yanapunguza hilo.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.